Tuishi kama Nyerere


editor's picture

Na editor - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

WATANZANIA tunamkumbuka sana Mwalimu Julius Nyerere. Alijenga taifa lenye mshikamano. Hata makabila yake mengi yametumika kuibua utani miongoni mwa wananchi na siyo mifarakano.

Mwalimu alijenga uongozi madhubuti, japo ulimletea matatizo katika suala la uwajibikaji. Alisamehe wengi wa wasaidizi wake baada ya kuharibu kazi, badala ya kuwafukuza.

Wakati tunatimiza miaka 10 ya kumkosa Baba wa Taifa, akiwa amefariki dunia 14 Oktoba, 1999, hospitalini London, nchini Uingereza, kipo kitu hatutakisahau.

Alifanikiwa kujenga mfumo mzuri wa maadili miongoni mwa viongozi wa umma. Alistawisha uongozi uliotukuka.

Viongozi walikuwa bora siyo bora- viongozi. Kila mmoja alifunzwa kutumikia umma kwanza kwa manufaa ya jamii na taifa.

Tunamkumbuka tukimlilia. Wala si kuwa tunatamani angekuwepo nasi leo. Hilo haliwezekani. Hakuna binadamu ataishi milele duniani. Hata tuliobaki tutakufa.

Tunamlilia kwa kuwa ule uongozi uliotukuka alioustawisha, umekufa naye. Sasa hakuna uongozi wa umma kwani viwango vyake vinashuka mwaka hadi mwaka. Serikali inathibitisha ukweli huu kwa takwimu.

Kipindi hiki cha kumbukumbuka ya Mwalimu Nyerere, Watanzania wanaumia kwa sababu taifa lao linakaribia kufilisika kwa kukosa siasa safi.

Wananchi wanashuhudia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinachoshika hatamu ya uongozi wa dola, kikiwa taabani. Si chama cha wanyonge tena, kama ilivyokuwa awali. Kimepoteza dira.

Mwalimu alitamani kiongoze kwa kila jema. Wapi? Mwaka 1995 alipokuwa anaanzisha mjadala wa namna ya kupatikana mgombea urais, Mwalimu aliorodhesha matatizo mengi ya kiuongozi.

Maelezo yake yaliashiria kulalamika kuwa hata wale makada aliojitahidi kuwajenga, wamekosa busara na hekima kama viongozi wengine.

Alitaja rushwa, ukabila na udini. Mwalimu alitaka kiongozi mpya awe yule anayechukia yote hayo. Awe mlinda Muungano wa Tanzania na mtetezi mkubwa wa Katiba.

Mwalimu alitaka kiongozi ambaye atachukia hayo hadharani na ndani ya moyo wake; aonekane hasa ana msimamo wa kukataa maovu.

Alitaka kiongozi mwenye uwezo wa kujenga uchumi ambao matunda yake yatafikia wanyonge wa mwisho walioko vijijini.

Alijaribu. Hakufanikiwa sana. Hata yule aliyempigia kampeni nchi nzima, alijitahidi tu; hakufanikiwa. Athari za uongozi mbaya uliojaa kiburi zinaendelea kugharimu Watanzania.

Hapa ndipo pa kuanzia. Watanzania tumkumbuke Mwalimu kwa kupenda yale aliyoyapenda ambayo yana maslahi nasi na taifa letu.

Hii ndiyo changamoto kubwa inayokabili Watanzania: Kuchagua viongozi wanaojali wananchi; wenye uchungu na maendeleo ya wote; na wasio wepesi kulaghaiwa na mafisadi wa kimataifa kwa jina la wawekezaji.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: