Tujifunze kutoka kwa Maria Nyerere


Nkwazi Mhango's picture

Na Nkwazi Mhango - Imechapwa 21 April 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

NAKUMBUKA. Nilianzisha mjadalala juu ya utata kuhusu shughuli na maisha ya wake wa marais – First Ladies – katika nchi za Afrika.

Mwandishi Ezekiel Kamwanga wa gazeti lenu hili ameuboresha kiasi cha kunishawishi nirejee kwenye hoja hii.

Hata hivyo, marejeo yangu si historia, bali kinachotendeka katika nchi ninayoishi – Canada. Hapa maisha ya mke wa waziri mkuu, Stephen Harper hayana tofauti na maisha ya raia wengine wa kawaida.

Kanada ni nchi ambayo muundo wake wa utawala ni ule wa kuwa na waziri mkuu ambaye ni kiongozi wa serikali. Hivyo mke wa waziri mkuu anasimama sawa na mke wa rais – First Lady – kule ambako mfumo wa utawala unaruhusu kuwepo rais.

Ukimuuliza raia wa kawaida wa Canada, jina la mke wa waziri mkuu, ataishia kukuuliza, “Mke wa waziri mkuu ni nani katika nchi hii hadi nipasue kichwa?”

Hii ni kwa sababu, mke wa waziri mkuu siyo sehemu ya utawala wa nchi. Yeye ni raia sawa na wengine.

Kimsingi mke wa waziri mkuu hapa nchini hana mamlaka yoyote kikatiba na kimaisha. Kama anajulikana, kwa kiwango chochote kile, basi siyo kwa sababu mumewe ni kiongozi wa nchi. Wala hana misafara ya magari kama ilivyo Afrika.

First Lady huyu hana walinzi wala ukwasi; hatoi kauli za kisiasa au kuonekana kwenye vyombo vya habari. Ni mara chache sana huandamana na mumewe.

First Ladies wa Afrika humiliki mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGOs) au asasi nyingine za kijamii. Mara nyingi hutumia asasi hizo kuhudumia wanawake wenzao au watoto kupitia mgongo wa ikulu.

Kwa njia hiyo, inafikia mahali wake wa marais au mawaziri wakuu wanataka kuwa wanasiasa na kuingia moja kwa moja katika mbio hizo za kutafuta utukufu wa kisiasa. Hii ni kwa kuwa wana nyenzo za ikulu.

Chukua mfano wa mke wa rais wa Argentina, Cristina Fernández de Kirchner ambaye sasa ni rais baada ya kuchukua madaraka kwa kuchaguliwa kikatiba toka kwa mumewe, Fernández de Kirchner.

Bali katika Canada, kama First Lady alikuwa mwalimu, daktari, mhasibu au mama wa nyumbani, ataendelea kuwa hivyo. Utamuona mitaani akipishana na wananchi wa kawaida.

Kuna kipindi wakosoaji wa waziri mkuu, Stephen Harper waliwahi kumrushia kijembe kuwa mkewe Laureen Teskey Harper, ni mpanda pikipiki. Lakini Harper alijibu kwamba ni kweli mke wake ni mpenzi wa kupanda pikipiki na hayo ni maisha yake.

Hili liliwajengea heshima kubwa Harper na mkewe. Kwani walipakodi wa Canada wasingevumilia kuona mke wa mkuu wa serikali akifyonza kwenye hazina ya nchi au akifanya biashara ambayo haiingizii kodi serikali au akilipa kodi ya “upendeleo.”

Kwa mke wa waziri mkuu wa Canada, cheo cha mumewe ni cha mumewe siyo chake wala hana haja ya kukidandia.

Mke wa waziri mkuu wa Canada hufanya shughuli zake kama mke wa mume mwingine. Hutumia pikipiki yake hata kubebea watoto wake, Benjamin na Rachel, kwenda na kutoka shuleni.

Hata wananchi wanampenda na kumheshimu mke wa kiongozi wao kwa vile siyo mzigo kwao na wala haonekani kutumia cheo cha nafasi ya mumewe ya waziri mkuu.

Je, kwanini wake wa watawala wa Afrika wasifuate mfano huu maridhawa ambao unawaongezea heshima badala ya kuonekana kama wadandizi?

Mke huyu wa waziri mkuu wa Canada anaishi maisha yake sawa na alivyokuwa akiishi kabla ya mumewe kuingia madarakani. Hahitaji misafara na walinzi.

Mke wa waziri mkuu wa zamani wa Uingireza Tony Blair, Bi. Cherie Blair ni mwanasheria kama alivyokuwa kabla ya mumewe kuwa kiongozi.

Aliwahi kushitakiwa na kupigwa faini kwa kutolipia tikiti kwenye treni jijini London. Je, ni mke wa mtawala gani Afrika anapanda treni na kujilipia nauli?

Je, tunawafadhili wake wa wakubwa kwa utajiri gani wakati sisi ni ombaomba wa kunuka tunaotegemea wafadhili?

Kimsingi nimelazimika kuandika makala hii baada ya kuona utata unaozunguka tabia na maisha ya wake wa watawala wa Afrika. Kwa mfano, nchi ya jirani ya Kenya, mke wa rais, mara mbili, alifikia hatua hata ya kuwazaba makofi waandishi wa habari.

Kingine kilichonisukuma, ni misafara ya wake wa marais wa Afrika ambayo nimewahi kushuhudia. Misafara hii huwa mirefu na ya gharama kubwa.

Pengine huacha wanawake na wanaume wakisonya na kulaani baada ya kusubirishwa kwa zaidi ya saa nzima kwa madai ya kusubiri mke wa rais au waziri mkuu apite. Ni karaha tupu.

Najiuliza: Hivi akina mama hawa wanapata wapi fungu la fedha kuhudumia misafara na walinzi wao namna hii wakati katiba za nchi zao hazina kipengele hata kimoja kinachotaja mamlaka ya mke wa mtawala?

Je, marais wa Afrika wanajua kuwa hali hii inachafua madaraka yao? Mbona wakati wa kuchagua na kuapa kutumikia taifa, huwa wanachaguliwa pekee yao?

Kuna kitu kingine kuhusiana na mke wa waziri mkuu wa Canada. Yeye haandamani na mumewe katika kila ziara za kiserikali ndani na hata nje ya nchi. Hii ni kwa sababu inaeleweka na kuaminika, kuwa kufanya hivyo ni kutwisha mzigo wananchi.

Pamoja na kwamba Canada ni tajiri kuliko nchi zote za Afrika, lakini bado wananchi wake wanapinga viongozi wao kutumia raslimali na madaraka yao vibaya.

Mke wa aliyekuwa rais wa Nigeria, Jina la 1 Babangida, alifahamika kwa kukusanya michango mingi kwa njia ya asasi ya kijamii na kutumia ofisi na madaraka ya mumewe kufanya biashara.

Ukiacha wake za marais, kuna tatizo hata la watoto wa marais. Mfano hai ni nchini Kenya ambako wakati wa utawala wa Daniel arap Moi, watoto wa rais walikuwa kama “marais wadogo” kiasi cha kujichotea mabilioni ya shilingi kutoka kwenye hazina ya nchi.

Ni muhimu kujitazama upya katika hili. Baba wa taifa hili hakuwahi kumruhusu mkewe, Mama Maria Nyerere, kudandia madaraka yake wala kuanzisha NGO. Hadi leo, Mama Maria anaheshimika kuliko wake wa marais wote waliwahi kuitawala nchi hii.

Mwandishi wa makala hii ni mwandishi wa habari, mwalimu, mwanaharakati na mshairi. Anaishi nchini Canada. Anapatikwa kwa email: nkwazigatsha@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 4 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: