Tujifunze kutokana na makosa


editor's picture

Na editor - Imechapwa 16 June 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

SERIKALI imetangaza rasmi kumalizika kwa muda wa mpango maalum wa kukuza uchumi na kuondoa umasikini. Mpango huu ndio umekuwa ukiitwa MKUKUTA-I.

Mambo mengi ambayo yalikuwa yafanywe chini ya mpago huu hayakukamilishwa; hivyo malengo hayakufikiwa; tena kwa kiasi kikubwa.

Kwa mfano, chini ya MKUKUTA-I, ukuaji wa sekta ya kilimo ulikadiriwa kukua kutoka asilimia tano hadi asilimia 10 ifikapo mwezi huu.

Ukuaji katika sekta ya mifugo ulipangwa kukua kutoka asilimia 2.7 mwaka 2005/2006 hadi asilimia 9 mwaka huu.

Ongezeko la uzalishaji chakula lilipangwa kuongezwa kutoka tani 9 milioni hadi tani 12 milioni na kufanya nchi, wakati wowote ule, kuwa na akiba ya chakula cha miezi minne.

Malengo yote hayo hayakufikiwa. Katika baadhi ya maeneo, malengo hayakufikiwa hata kwa nusu.

Sasa serikali imetangaza kuwa inaanzisha hatua ya pili ya mpango wake – MKUKUTA-II. Kwa mujibu wa ratiba, mpango huu unatarajiwa kuanza mwaka huu.

Je, serikali inaelewa vema pale ilipojikwaa na kusababisha kutofikia malengo ya mpango huu? Je, inaweza kukiri kuwa imepata somo la kutosha katika mpango wa kwanza?

Chukua mfano wa utekelezaji katika eneo la kilimo. Ni kilimo kilichotakiwa kuwa chachu ya mpango mzima kwa kuwa ndicho kinaajiri wananchi wengi.

Lakini wakati wa utekelezaji wa mkakati huo, kilimo hakikupata bajeti yake yote iliyokuwa ikipangwa. Tunashuhudia mapungufu makubwa katika kila bajeti tangu 2005/2006 hadi 2009/2010.

Matokeo ya uwekezaji huu mdogo katika kilimo yamesababisha kuongezeka kwa idadi ya wananchi masikini.

Si ajabu basi, kwamba kati ya wananchi masikini milioni 12.9, asilimia 83 ambayo ni sawa na masikini 10.7 wanaishi vijijini. Hii ndiyo athari ya kutowekeza ipasavyo katika kilimo.

Serikali inatakiwa pia kuangalia ni jinsi gani imeathirika kwa kutoihusisha ipasavyo sekta binafsi katika MKUKUTA-I na jinsi gani hatua hiyo imeathiri ukuaji wa uchumi.

Kuna haja kwa serikali kupunguza matumizi makubwa na yasiyo ya lazima kwa manufaa ya wananchi na serikali yenyewe, kwani ni matumizi hayo ambayo yameathiri zaidi malengo ya mpango wa kuondoa umasikini.

Kutokuwa na tathmini sahihi ya MKUKUTA-I, tathmini ambayo ingekuwa dira sahihi ya utekelezaji katika MKUKUTA-II, itakuwa sawa na kuandaa mpango wa kuendeleza umasikini.

0
No votes yet