Tujisahihishe tucheze Kombe la Dunia 2018


Maurice O. Gama's picture

Na Maurice O. Gama - Imechapwa 07 September 2011

Printer-friendly version
Michezo

HAYATI Shaban Robert aliwahi kuandikA, “Ng’ombe avunjikapo mguu malishoni, hujikokota zizini apate kusaidiwa.” Msemo huu ndio unafaa kutumika kuijenga Taifa Stars iliyojeruhiwa na kushindwa kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2012.

Baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Algeria katika mechi muhimu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Stars haina nafasi tena isipokuwa, kama ilivyo kwa timu nyingine za mpira wa miguu, inapaswa ikokotwe zizini ili isaidiwe.

Kusaidiwa hapa ni kuzijenga timu zetu kwa ukamilifu ili taifa lichukue nafasi yake kati ya mataifa yaliyo huru na yenye heshima sawa kupitia michezo. Makala haya yatajikita kwenye ujenzi wa Taifa Stars.

Kila mmoja ameona udhaifu wa Taifa Stars uko wapi. Ujenzi wake uzingatie kikosi cha kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2016 na Kombe la Dunia 2018.

Vijana wengi walioko Stars sasa wanaweza kusaidia timu kufuzu kwa fainali hizo lakini kufikia mwaka 2016 au 2018 ama watakuwa wamezeeka au wameshuka kiwango.

Hivyo basi ujenzi uanze sasa na kikosi cha wachezaji wa umri wa chini ya miaka 14 na chini ya miaka 17. Tuna uwezo mkubwa wa kujenga timu makini, lakini tunaponzwa na namna tunavyouchukulia mchezo huu.

Kweli mpira ni mchezo wa kustarehesha, lakini kuna tofauti namna ya kustarehe. Tucheze kuburudika na kupitia hiyo burudani tupate pia vikombe vya ushindi, na kwa vikombe hivyo tujitambulishe duniani.

Siku Rais Jakaya Kikwete anapokea Kombe la Dunia, 13 Januari 2006 alisema, “Maendeleo ya mpira na kwa kweli maendeleo ya michezo ipo juu kwenye ajenda yetu. Tunataka kuiona Tanzania ikijengeka na kuwa nchi yenye timu bora ya mpira barani Afrika na ikiwezekana duniani. Najua inawezekana ikiwa kila mmoja wetu akitenda lililo sahihi kuelekea lengo hilo…..”

Rais aliposema “kutenda lililo sahihi” alikuwa na maana kwamba jambo linalotendwa kwa usahihi linapimika. Kipimo chetu cha ufanisi katika kuwa nchi yenye timu bora ni kushinda mechi dhidi ya timu zilizojuu yetu kiufundi.

Tulitenda lililosahihi mpaka tukafuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980 lakini miaka yote iliyofuata hatukutenda sahihi. Hivyo basi, tuanze sasa safari ya kuipeleka Taifa Stars kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2016 na Kombe la Dunia 2018.

Rais Kikwete alipomleta Marcio Maximo mwaka 2006 kwa kampeni za kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2008 na 2010 na fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika mwaka jana Afrika Kusini ilikuwa hatua ya kwanza kwenda kileleni.

Kilichofuatia maji yalizidi unga. Kwa uelewa wangu, mapungufu kadhaa yalijitokeza. Kwanza ‘uongozi’ na uhamasishaji aliachiwa Rais peke yake. Safari hii viongozi wengi tutawataka  wajihusishe. Mashindano haya yachukuliwe kama juhudi za taifa kuonyesha utashi wake mbele ya mataifa yaliyosawa. 

Pili mikakati ya ushindi ilitegemea ufundi na aliachiwa Maximo. Hapakuwa na hatua thabiti kuwajenga vijana kiakili, kiutashi na kizalendo. Uhamasishaji uliishia Dar es Salaam tu.

Uhamasishaji ninaouzungumzia hapa nalinganisha na Mwalimu Nyerere alivyowaandaa vijana kisaikolojia na kiuzalendo dhidi ya adui. Alipotoa hotuba yake alisema “Nia ya kumpiga tunayo, uwezo wa kumpiga tunao, na sababu ya kumpiga tunayo...”  vijana walihamasika sana. Biblia inasema, ukiwa na imani timilifu, hata mlima utauondoa.

Tatu Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo iandae bajeti itakayokidhi mahitaji. Tuondokane na visingizio. Bajeti ya mwaka 2011/12  ni Sh. 14 bilioni, ukitoa matumizi ya kawaida, posho na safari kiasi kinachobaki hakitoshi kuhudumia michezo yote.

Kuwe na kongomano la wadau wa soka kujadili suala la kuendeleza timu. Mawazo yatakayopatikana yafanyiwe kazi na serikali.

Nne TFF iwe na kitengo kushughulikia mechi za kimataifa, wakiwemo na wadau wa mpira wenye upeo na utashi thabiti kuendeleza soka. Tuwaepuke watu wanaotafuta nafasi ya soka kwa malengo ya kutawala na sio kuongoza. Angalia yanayofanyika kwenye baadhi ya klabu hapa nchini.

Tano walimu wa ndani wajipange upya kufundisha mpira. Nakumbuka kufundishwa “one touch, center ball”. Mfumo huo na mengi wanayofundishwa vijana hayasaidii. Bila kuwa na ufundi binafsi, bila washambuliaji, viungo, mabeki kupata ufundi wa nafasi zao huwezi kufundisha timu, hili ni kosa linalofanywa na makocha wazalendo.

Sita wachezaji waliochaguliwa kwenye timu ya taifa walitokana na wale waliojifunza wenyewe; wenye mapungufu ya kinidhamu, kutokujiamini, ubabe na imani potofu.  Tabia hizi ni ngumu kuzibomoa na ndio mara nyingi hawakufundishika.

Ikiwezekana Maximo arudishwe. Huyu kwa mtazamo wangu ni kocha, ambaye pamoja na ufundi wake anaweza kuwahamasisha wachezaji kwa kiwango cha ushabiki. Ni katika hulka kama hizo wachezaji wengi hufanikiwa zaidi ya kawaida.

Tunataka vijana wahamasike kiasi kwamba kwa hiari yao, kwa nafasi zao waendelee na mazoezi. Kuumudu mchezo wa mpira kwa kiwango cha kimataifa ni suala zaidi la mchezaji mwenyewe, na sio kocha. 

Mafanikio ni mapenzi ya Mungu lakini kuhangaika ni juu yetu wenyewe. Vijana wafundishwe, wawezeshwe, wahamasishwe, tuwajali, tuwapende na wao watajituma, wataleta heshima kwa taifa letu. Sasa iwe basi kucheza kwa hasara yetu wenyewe. Wenye maamuzi watusikie.

 “Anayejua amepotea njia anajua aendako, asiyejua hawezi kupotea.”

0
No votes yet