Tukatae kuwa taifa la ovyo


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 07 July 2009

Printer-friendly version
Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa akinadi saa yake ya mkononi

WATANZANIA tumeamua kuwa taifa la watu wa ovyo! Ni watu wa ovyo hasa. Kutotaka kutenda kwa kufuata sheria wala taratibu katika taifa linalojivuna kwa umaarufu miongoni mwa mataifa yanayoendelea, ni kitu cha ovyo kabisa.
 
Ukifuatilia mijadala katika mkutano wa 16 wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma, utakubali Watanzania wamechagua kutambulika hivyo.
 
Kuna hili suala la Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa; kwamba je, akiwa madarakani kipindi cha miaka kumi – 1995-2005, alivunja kiapo chake cha uaminifu kwa kujitumbukiza katika mambo binafsi na kustahili kushitakiwa?

Je, Rais aliyepata umaarufu nchini na duniani kote hata kuteuliwa kuongoza kundi la wapiga debe wa itikadi ya kimagharibi ya utandawazi, kwa makusudi au kwa bahati mbaya alitumia Ikulu kwa manufaa binafsi?
 
Ndiyo maswali yanayoulizwa kwa mdua sasa kuhusu mwenendo wa Mkapa. Wapo wanaomtaja kama mmoja wa viongozi wastaafu fisadi. Wanatazama madudu aliyojitumbukiza na sasa yanampa tabu.

Kwamba akiwa mkuu wa dola, kwa kipindi hicho, Mkapa alijihusisha na biashara kwa kujimilikisha shirika la umma akishirikiana na Daniel Yona, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini katika serikali yake.
 
Mkoani Mbeya, serikali ikimiliki mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira ambao wakati huo ulithaminiwa kwa kiasi cha Sh. 4 bilioni, kama ilivyothibitishwa na serikali.

Hata Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, hivi karibuni alisema serikali inataka kufanya mazungumzo na Mkapa ili kuchukua hisa za mgodi huu, hatua inayoonekana ni ya kumwepusha Mkapa na tuhuma za kuitwa fisadi.
 
Mkapa na Yona walinunua mgodi huu kwa Sh. 700 milioni tu; kibaya zaidi walilipa Sh. 70 milioni tu kati ya hizo. Ili kufanikisha mipango yao, waliingia mkataba na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuuza kwao umeme utakaozalishwa hapo.

Ni kweli Mkapa kwa bahati mbaya (kwa mujibu wa Pinda) au kwa makusudi alijitumbukiza katika biashara akiwa Ikulu; si ya Kiwira tu; kuna suala la kukopa fedha benki bila ya kuwa na dhamana na kununua nyumba ambayo hati yake ndiyo iligeuzwa dhamana; kuna kusajili kampuni binafsi wakiwa Ikulu na mkewe, Anna, ANBEN.

Kwa kiwango chochote kile cha uadilifu, haya yanamweka pabaya Mkapa kwamba alitenda uovu kwenye ofisi ya umma. Na ingekuwa faraja iwapo watu wangeepuka kutumia Bunge kusafisha mambo haya, kwani si jambo zuri na ni kudhalilisha Bunge.

Sasa katika haya yote, kwa nini tumeamua kuwa watu wa ovyo? Ni kwasababu ndani ya Bunge kuna watu wanataka Watanzania wasadiki kuwa Mkapa anaonewa kwa vile ni kiongozi safi; mbaya zaidi kuna wabunge wanapiga kelele wakimtaka Spika azuie wabunge kumtaja Mkapa kwa matendo hayo.
 
Wiki iliyopita, Peter Serukamba (Kigoma Mjini), alifikia hatua ya juu alipoasa Mkapa alindwe. Alitaka Spika azuie wabunge kumjadili Mkapa kwa kuwa “dunia haitawaelewa Watanzania.”

Kwa aina ya kauli ya Serukamba (CCM), ni vema kufumba macho na kusahau kabisa kuwapo tuhuma dhidi ya Mkapa. Anaamini Mkapa anachafuliwa tu isivyostahili.

Serukamba angesimama kumtetea Mkapa kwa hisia zake binafsi bila ya kushawishi Bunge lipigwe kufuli, ingeeleweka, lakini anapotaka kufunga midomo ya wabunge wote wasimtaje Mkapa haiwezekani.

Haiwezekani kutaka kufanya Watanzania watu wa ovyo. Kwamba wote wapuuze tuhuma za kuibiwa au kuporwa kwa mali yao huku wakimuacha mhusika kwa sababu ni kiongozi wa juu mwisho katika taifa.

Serukamba hazingatii kamwe kuwa Mkapa hakuwa na sababu yoyote ya kupanga utajiri usiokuwa halali kutokana na mafao makubwa anayopata baada ya kustaafu yatakayomwezesha kuishi kwa raha mustarehe pamoja na mkewe hadi watakapoingia kaburini.
 
Mkapa, kama walivyo viongozi wengine wakuu wastaafu kitaifa, hana shida yoyote, iwe safari za nje za kutanua au za matibabu; iwe ni ulinzi, usafiri wa ndani, au mayaya na maboi wa nyumbani. Mafao yake yanagharamia vyote hivyo na vinginevyo. Ni tamaa tu!

Akiwa kijijini kwake Lupaso, wilayani Masasi, Mkapa alituhumu magazeti kuwa yanamchafua kwa kuandika tuhuma za alivyojipatia mali isivyo halali. Alisema anaishi kwa pensheni na kutaka wananchi wapuuze tuhuma hizo kwa kuyachanachana magazeti husika. Hadi anatetewa bungeni, Mkapa hajatoka hadharani kuzungumzia kwa undani hasa tuhuma zake, ingawa amekuwa akisema, “Nimestaafu siasa. Mkitaka hayo muulizeni rais Kikwete maana mimi nimebaki tu mtu wa kanisa.”

Wakati akilalama kuchafuliwa, sasa ndani ya Bunge wanaibuka watu na kampeni ya kumsafisha japo wanajua wazi si kawaida mtu kumuombea msamaha mtuhumiwa wakati mwenyewe hajaonyesha uungwana na kujuta.

Mkapa anaweza kuamini anaandamwa na wale waliotarajia kupata upendeleo wa vyeo wakati wa utawala wake na huo ukawa ni sehemu ya mkakati wa kujitetea, lakini kosa lake kubwa ni kushindwa kukiri kushiriki kumega mali ya umma kwa hila.

Kwa hapo, kila anayethubutu kumtetea anaonyesha tu kuwa Mkapa anaonewa; ni msafi asiyestahili kusulubiwa kwani kama kuna baya alilofanya ni la bahati mbaya. Yote hayo, mhusika amebaki kimya na sasa Watanzania waone serikali inamsafisha hadi ndani ya bunge.

Ni kwa nini akina Serukamba wameamua kulazimisha Watanzania kuwa taifa la ovyo kwa kutaka Bunge lao lionekane la ovyo kwa kumuomba Spika azibe watu midomo? Alichofanya Serukamba na wengineo ni kudharau utawala wa sheria na hivyo kutaka Tanzania lionekane taifa la watu wasiofuata sheria na taratibu.

Wapambe wote wa Mkapa wazingatie ushauri wa bure huu: Wamshauri mpendwa wao atoke kwenye gome na ajitetee, au atubu hadharani ili kutaraji msamaha wa umma.

Watanzania ni waungwana watamsamehe tu Mkapa, lakini njia hii ya kujisafisha kupitia wapambe kama akina Serukamba kamwe haitafanikiwa kumvua na tuhuma kwani Watanzania hawataki kuwa watu wa ovyo!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: