Tukijiuliza maswali hatutaichangia CCM


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 14 April 2010

Printer-friendly version
YUSUF Makamba

MWISHONI mwa juma lililopita Rais Jakaya Kikwete alizindua utaratibu wa kuchangia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu; utaratibu ambao kwa siasa za Tanzania uliasisiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mwaka jana.

Kwa mujibu wa viongozi wa CCM, lengo la uzinduzi huo ni kukiwezesha chama kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 40 kwa ajili ya kutimiza malengo yafuatayo:

Kununua magari 60 kwa ajili ya kampeni, kununua pikipiki 170, baskeli 23,000, kukodi helikopta na ndege na matumizi mbalimbali ya makabrasha ya kampeni na uchaguzi.

Kila atakayetuma ujumbe husika kwa namba walizopewa atakuwa amechangia chama ama Shs 300, au Shs 500 au Shs. 1000, kulingana na namba atakazotumia.

Lakini kila mmoja anajua kuwa CCM hawategemei njia hii kupata mabilioni hayo. Watatumia mbinu nyingine mbalimbali zitakazowawezesha kufikia lengo hilo.

Walau wamejitahidi kutujulisha ni kiasi gani kinahitajika, kitatumika vipi, na namna gani kuweza kuchangia. Baada ya kuyajua hayo hatuna budi kujiuliza kama tuchangie au tusichangie.

Jiulize kabla ya kuchangia

Mashabiki wa CCM watakuwa tayari kuchangia kwa vile tu “Rais kasema.” Nimeona ni vema niwasaidiewatu hawa ambao wana fedha na vitu mbalimbali ambavyo wako tayari kuviweka kwenye miguu ya CCM; wajiulize maswali kadhaa ambayo wanapaswa kuyajibu yote mawili kabla hawajatoa michango hiyo.

Kwanza, ni lazima wajiulize, je wanakubali utawala wa miaka mingine mitano ya CCM? Pili, wameridhika na utawala wa CCM ilivyo sasa? Kama hawaoni tatizo lolote la CCM kuendelea kuongoza miaka mitano, waichague tena. Na kama wameridhika na uongozi wa CCM hadi hivi sasa basi ni jukumu lao vile vile kutoa fedha nyingi, muda, na vitu mbalimbali kukisaidia chama kuzidi kuongoza. Lakini kama mtu anajibu “hapana” kwa swali lolote kati ya hayo, basi uamuzi wa kuchangia au kutochangia vile vile utakuwa rahisi kwake.

Je umeridhika?

Kama umeridhika na jinsi ambavyo chini ya utawala wa CCM Tanzania imegeuzwa kuwa tegemezi zaidi na yenye kutegemea uombaomba wa kudumu, basi changia CCM.

Kama umeridhika na jinsi serikali ya CCM ilivyojitahidi kuua viwanda vyetu vya ndani, mashirika yetu ya umma na kufungua mlango mpana kwa wawekezaji wa kigeni kufanya hata vile ambavyo tayari tulikuwa na uwezo wa kuvifanya sisi wenyewe; changia CCM

Kama umeridhika kuona kuwa CCM inataka muichangie ili inunue magari, pikipiki, na baskeli kwa ajili ya kampeni zake wakati madaktari, walimu, polisi na watumishi mbalimbali wa umma hawana uhakika wa usafiri au huduma nyingine muhimu, basi changia CCM.

Kama umeridhika na hali ya vituo vyetu vya afya, kama ambavyo tumeona katika vipindi kadhaa vya runinga siku chache zilizopita, kina mama wajawazito wakirundikana kwenye chumba kimoja; ichangie CCM.

Kama umeridhika na jinsi ambavyo shule zetu zimeendelea kufanya vibaya na kufelisha kwa kiwango cha kupewa tuzo na kusababisha kizazi cha wasomi wetu kuwa chenye “utata” muda si mrefu ujao, basi changia CCM.

Kama umeridhika na jinsi serikali ilivyoweza kuondoa tatizo la umeme nchini kwa miaka yote hii, na jinsi ambavyo wameshughulikia suala la Richmond na sasa Dowans hadi kampuni hiyo imeweza kuuza mitambo bila kujali au kuulizwa na mtu yeyote, basi changia CCM.

Kama umeridhika na kauli kuwa “serikali iko mbioni” au “serikali imedhamiria” au “Tumeanzisha mchakato” au “tuna nia nzuri kabisa” ya kufanya mambo ambayo wameshindwa kuyafanya miaka nenda rudi, basi changia CCM

Kama umeridhika na jinsi gani serikali imefuta haki za raia kwa sababu haizipendi au kwa sababu haiamini Watanzania kuwa wana uwezo wa kuamua wao wenyewe nani anawafaa, na hivyo kutaka kupewa haki ya kugombea kama wagombea huru au binafsi, basi ,changia CCM.

Kimsingi kila Mtanzania na mwana CCM anatakiwa kutafuta majibu ya maswali haya ya kuridhika na mengine mengi. Kama mfumo wa kifisadi umekufanya ufanikiwe na ufanikishe maisha ya watoto wako, ni wazi kuwa ili kulinda maslahi yako utapenda kuona mfumo huu wa utawala wa kifisadi unaendelea.

Kama mazingira ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ambayo tumeyashuhudia ndani ya miaka hii michache iliyopita kwako hayana tatizo kwani “kila mtu na lwake” basi huna budi kuendelea kuiwezesha CCM. Kama unaamini kuwa chama kile kile, chenye watu wale wale, sera zile zile na itikadi ile ile ya kibepari kinaweza kuja na matokeo tofauti, basi endelea kuchangia fedha zako ili uone kama mtu anayepanda mpunga huvuna mahindi.

Ndugu zangu, uamuzi kwenye swali hili kama nilivyosema ni rahisi sana. Ukichangia CCM unakiwezesha na kukipa uwezo ili kiendelee kutawala kwa sera zile zile, na kwa namna ile ile.

Kutochangia CCM ni kukipunguzia uwezo wa kuendelea kuongoza na kututawala kwa namna ile ile. Katika kufikia uamuzi huu inampasa mtu kutoka nje ya ushabiki wa kisiasa, maslahi binafsi au kutafuta.

Swali hili nalo lijibiwe: Je, uamuzi wangu katika kuunga mkono chama au mgombea fulani utasaidia vipi taifa na jamii ya kizazi kijacho? Je, kwa kuchangia chama au kikundi ambacho kimeshashindwa kuonyesha njia, naweza vipi kuleta mabadiliko?Au ndiyo naendeleza zile itikadi zilizoshindwa za ufisadi?

Ni katika kupata majibu ya maswali hayo ndipo mtu anaweza kufikiria kama yuko tayari kuchagua CCM.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: