Tumbili watangaza ‘ufalme’ Bukoba


Trasease Kagaruki's picture

Na Trasease Kagaruki - Imechapwa 21 April 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Wananchi walalamikia halmashauri
Wadai serikali imewachimbia kaburi

“ENKENDE zatulambaza” – tumbili watatuua kwa njaa. Hizo ni kauli za vilio zinazotolewa na wananchi wa kata Kanyangereko na Maruku katika wilaya ya Bukoba Vijijini.

Ni umbali wa kilometa 12 kusini mwa mji wa Bukoba mjini. Wananchi wamekata tamaa. Wanalima, hawavuni. Tumbili ndio wanavunia matumboni mwao.

Wakazi wengi wa maeneo haya ni vijana wakulima wadogo ambao wanategemea kipato cha kujikimu kutokana na kilimo cha nyanya, nyanya chungu, karoti, pilipilihoho na kabeji.

Mmoja wa wakulima wadogo Cyridion Mutasi wa Kitongoji Lyagama, kijiji Bwizanduru, Kata Maruku anasema, “Tumbili wanakula karibu aina zote za mazao tunayolima hapa. Hakuna tunachovuna na tunadidimia katika umasikini ambao tulitaka kuepuka.”

Awali wakulima walikuwa wakishirikiana kuwinda tumbiri. Walitumia mbwa, mikuki, mishale na mapanga. Hivi sasa tumbili wamezaliana na kuwa kama majeshi makubwa.

“Bila msaada wa serikali, hatuwezi kukabiliana na tumbiri wengi namna hiyo na hatuwezi kuvuna chochote,” analalamika Mutasi.

Wakazi wa hapa wanatupia lawama serikali – viongozi wa kata wakiwemo madiwani na mbunge wa jimbo la Bukoba vijijini.

Wanasema wamekuwa wakifanya vikao vya maendeleo kuanzia kwenye vitongoji, vijiji na kata hatimaye kuwasilisha kero hii kwao, lakini hakuna hatua ambazo zimechukuliwa kunusuru mazao yao.

Kata Maruku inaundwa na vijiji Bwizanduru, Maruku, Kyansozi na ina kaya zipatazo 1,733. Kata Kanyangereko ina kaya zipatazo 1,500 katika vijiji vya Bulinda, Butayaibega na Bulambizi.

Tumbiri wa Maruku na Kanyangereko wanakula matunda mabichi na yaliyokomaa. Wanakula ndizi changa pia. Kwa hiyo, licha ya migomba kushambuliwa na ugonjwa unaofanya ikauke na kuanguka, tumbiri wanakula kile kidogo kilichosalia kabla hakijakomaa.

Bw. Stansilaus Mkwenda, mkulima na mkazi wa kitongoji Nkimbo kijiji Butayaibega anasema, “Katika hali hii, dhana ya KILIMO KWANZA haina pa kupenyeza. Viongozi hawatusikilizi. Wametuingiza katika umasikini wa kupindukia.”

Analaumu halmashauri ya wilaya kwa kushindwa kutumia wataalamu wake wa maliasili kuwaangamiza tumbili. “Labda tusubiri uchaguzi unaokuja. Silaha iliyopo ni kutowachagua tena,” amesema Mkwenda kwa sauti ya kuonyesha uchungu.

Wakazi wa kata Kanyagereko hususani wa vitongoji Lwazi, Kasha, Kalimi, Bugera na Katembe ambao wanaishi karibu na mwambao wa Ziwa Viktoria, wanaongoza kwa kuathiriwa na wanyama hawa waharibifu.

Hawana hamu ya kupanda tena migomba, viazi vitamu, mihogo, mahidi na mazao mengine ya mboga. Wanasimulia jinsi tumbili walivyopiga kambi mapema katika eneo lao hata kabla vijiji vingine kuanza kushambuliwa.

Naye Kasota Lwamugira, mkazi wa kijiji Kanyangereko anasema, “Angalia mgomba huo ambao umetunga. Nimezungushia gunia nikijaribu kuweka kinga. Hata hivyo, tumbiri wamerarua gunia na kuanza kula hizo ndizi zinazochomoza... ni tatizo.”

Tumbili wanakula ndizi na matunda mengine, lakini pia wameanza kushambulia watu. Matukio kadhaa yameripotiwa ya tumbili kukwaruza watoto wa umri mdogo pindi wanapokutana nao au wanapowakuta wakicheza nje ya nyumba.

Mibuni iliyokuwa zao kuu la biashara katika eneo hili sasa imezeeka na mingine kushambuliwa na magonjwa ambayo wananchi wameshindwa kukabiliana nayo.

Lwamugira hakomi kulalamika. “Sasa hatuna zao la kutuingizia kipato na tunakoelekea umasikini utatukumba wengi na njaa itatuua,” anasimulia.

“Miaka ya nyuma tulitegemea uvuvi; uliboresha maisha yetu, lakini kwa sasa, ziwa hilo... (akionyesha kwa kidole). Linamilikiwa na wawekezaji. Masharti hatuyawezi. Tumefukuzwa. Watoto wanakaa zaidi ya wiki bila mboga. Utawala huu umetuchimbia kaburi,” anasema kwa sauti ya maombolezo.

Bibi Elizabeth Augustine Kabakama (74) wa Kitongoji Iyagama, akinitembeza katika shamba lake la migomba, anaeleza anavyohenyeshwa na tumbili.

“Huu ni mwaka wa tano toka niache kupanda mazao ya muda mfupi shambani. Tumbili wanakula kila zao, liwe limekomaa au bado. Sasa nimeinua mikono. Hakuna ninachoambulia.”

Elizabeth anasema, “Hapo awali tulijua tunagawana na tumbili, lakini sasa wamekuwa wengi mno na kuwa katili kupindukia. Wakikosa matunda wanang‘oa miche hovyo. Najiuliza watawala wako wapi? Tumbili sasa wawindwe kwa bunduki; wametusababishia njaa.”

Katika kitongoji Kazilabatemi kuna taarifa za mbunge wa Bukoba vijijini, Nazir Karamagi, kutoa Sh. 40,000/= ili zigawanywe sawa kwa kata mbili za Maruku na Kanyangereko, kuwawezesha kununua risasi za kuua tumbili. Fedha hizo zilitolewa mwaka juzi.

Wanakijiji wanalalamika kuwa fedha hizo hazitoshi kununua hata risasi tano na kwamba mbunge aliwafanyia kejeli.

Naye diwani wa Kata Kanyangereko, Mutagahywa Dezi, amekiri vijiji vyake kukumbwa na janga hili ambalo amesema limechangia kwa kiasi kikubwa, upungufu wa mazao ya chakula na hivyo kuongeza umasikini.

Dezi ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Bukoba Vijijini alijitetea kuwa tatizo la tumbiri amekuwa akiliwakilisha katika vikao vya wilaya lakini halipatiwi ufumbuzi kutokana na madai ya ufinyu wa bajeti.

Diwani wa Kata Maruku, Bw. George Mbezi, hakutofautiana na jirani yake wa Kata Kanyangereko. Amekiri kuona tatizo la tumbili ingawa hakueleza mkakati mpya wa kupambana nalo, mbali na kudai kwamba wanaendelea kushinikiza halmashauri kuwajibika.

Mbinu za kale za “omuhigo” – uwindaji au msako wa pamoja, sasa hazifui dafu. Licha ya tumbili kuwa wengi, wamekuwa wajanja pia. Hawali chakula au tunda lililotegwa sumu, anaeleza Deogratias Bigirwa, mkulima wa kitongoji Bibanja, kijiji Bulinda.

Karibu kila mwananchi niliyeongea naye kuhusu tatizo la tumbili, aliishia kulalamika kuwa watawala wanafuata kodi tu vijijini; lakini hawaendi kutatua matatizo yao.

Wengine walilalamika kuwa watawala wanakwenda kukagua miradi inayoendeshwa kwa ubia na serikali au kati ya jamii husika na wahisani, lakini siyo kutatua matatizo yao, hata yale ambayo sasa yamekuwa donda ndugu.

0
No votes yet