Tume huru lazima


editor's picture

Na editor - Imechapwa 05 October 2011

Printer-friendly version

UCHAGUZI mdogo wa ubunge, jimbo la Igunga, mkoani Tabora, wa Jumapili ya 2 Oktoba, 2011, umemalizika na kuwaachia Watanzania maswali mengi.

Kwanza, wako wapi wapigakura wa Igunga? Takwimu zinaonyesha daftari la wapigakura lililoandaliwa kwa uchaguzi mkuu wa 2010, lina zaidi ya wananchi 170,000 walioandikishwa.

Waliopiga kura uchaguzi ule uliompa ushindi Rostam Aziz wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hawakuzidi 50,000.

Katika uchaguzi wa kujaza kiti kilichokuwa wazi baada ya mbunge huyo kujiuzulu akisingizia “siasa uchwara” ndani ya chama chake, wapigakura hawakufika idadi hiyo.

Ina maana zaidi ya wapigakura 120,000 hawapo. Hawapo kwa sababu haikubaliki kwamba hao wote wamesusa kutumia haki yao ya kuchagua kiongozi wamtakaye.

Igunga hakukuwa na mazingira mabaya hivyo ya kumtisha mtu kutoka kupiga kura yake, tunathubutu kuuliza tena, “wako wapi wapigakura hawa?”

Huu ndio utata tunaoeleza. Kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilipoandikisha wananchi katika daftari, iliandikisha watu 170,000; basi lazima ieleze walipo wapigakura wengine.

Pili, matokeo ya uchaguzi mdogo yametangazwa karibu saa 24 kamili tangu upigaji kura ulipomalizika saa 10 alasiri, Jumapili 2 Oktoba.

Kama watu 170,000 walioandikishwa wangejitokeza na kupiga kura, maana yake Tume ingehitaji zaidi ya saa 72 kutangaza matokeo.

Kama hivyo ndivyo, ni dhahiri mfumo wetu wa kuendesha uchaguzi haufai. Katika dunia ya leo, ni uwendawazimu kutaraji kitu kama hicho.

Tunataka marekebisho ya mfumo wa uchaguzi – kuanzia daftari la wapigakura, upangaji vituo vya kupigia kura, kupeleka vifaa wakati wa uchaguzi, kuhesabu kura vituoni, kusafirisha masanduku ya kura hadi kwenye kata na kituo kikuu aliko msimamizi wa uchaguzi.

Tatu, tunauliza ni nini hasa sababu ya Tume kuchelewa kutangaza matokeo iwapo tangu Jumapili usiku, viongozi wa vyama vilivyoshiriki walikuwa wakitaja kura za vituoni?

Kwani kuchelewesha matokeo kunamnufaisha nani? Je, hii ndio kasi yetu ya kukomaza demokrasia Tanzania ? Na je, hii ndio misingi ya mfumo wa vyama vingi wanayoiamini viongozi wakuu wa serikali ya CCM?

Falsafa ya uchaguzi inasema kuchelewesha matokeo ya uchaguzi ni kutengeneza mazingira ya kupika matokeo, mbinu inayosaidia utawala kung’ang’ania madaraka.

Huko ni kuvuruga misingi ya uchaguzi huru na wa haki. Lazima tukomeshe mbinu chafu kama tunalenga kuzuia hasira za wananchi. Wakikasirika, watakataa haki zao kukandamizwa.

Tunataka sheria ya uchaguzi irekebishwe. Tuwe na sheria itakayotupatia tume huru kwelikweli; tume itakayoajiri watumishi wake siyo wakurugenzi wa halmashauri.

Tutapata tume itakayopanga bajeti yake na kuhifadhi fedha zake yenyewe. Na hii ndio huitwa tume huru inayochochea ukuaji wa misingi ya demokrasia na hatimaye maendeleo ya nchi.

0
No votes yet