Tume ya Haki za Binadamu yapeta


Alloyce Komba's picture

Na Alloyce Komba - Imechapwa 18 February 2009

Printer-friendly version

MAHAKAMA ya Rufaa Tanzania imetoa uamuzi wa kihistoria inaoipa hadhi inayostahili Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (Tume).

Katika hukumu yake ya hivi karibuni, mahakama ya rufaa imesema Mahakama Kuu ya Tanzania ndiyo yenye uwezo wa kuamuru mamlaka yoyote iliyobainika kuvunja haki za binadamu, kutekeleza maamuzi na, au mapendekezo ya Tume.

Uamuzi huo umetia mkazo nguvu ya kisheria katika utendaji kazi wa Tume ambayo hivi sasa inaongozwa na Jaji Kiongozi Mstaafu, Amiri Ramadhani Manento.

Watetezi wa haki za binadamu nchini wamesema hukumu hiyo imeipa meno Tume ingawa itang’ata kwa kupitia mahakama yenye wajibu wa kutoa amri kwamba mapendekezo yake yatekelezwe na mamlaka husika.

Jopo la majaji watatu wa mahakama ya rufaa, likiongozwa na Jaji Mkuu Augustino Ramadhani, limetoa hukumu hiyo katika Shauri la Madai la Rufaa Na. 88 la Mwaka 2006.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ndicho kilikata rufaa kwa niaba ya wananchi 135 wa kijiji cha Nyamuma katika wilaya ya Serengeti dhidi  Thomas Ole Sabaya na wengine wanne akiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Shauri hilo la rufaa lilitokana na kupinga uamuzi wa Jaji Projest Rugazia aliyekuwa ameamua kwamba Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi haina uwezo wa kutoa amri ya kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki za Binadamu.

Kituo cha sheria na haki za binadamu kilikwenda mahakama kuu, kitengo cha ardhi kuomba itoe amri ya kuitaka mamlaka husika itekeleze mapendekezo ya Tume.

Wakati huo Tume, baada ya uchunguzi, ilikuwa imetoa maelekezo kuwa walalamikaji waliofukuzwa kwenye eneo lao (Nyamuma Iliyobaki, Musoma mkoani Mara) warudishwe katika makazi yao na kulipwa fidia ya zaidi ya jumla ya Sh. 800 milioni.

Uamuzi wa Tume unaendana na kifungu cha 17 (1) cha Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Sura ya 391 na una hadhi ya “Mapendekezo.”

Lakini Jaji Rugazia wa mahakama kuu, aliyesikiliza shauri hilo lililowasilishwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, aliamua kuwa Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, iliyokuwa inasikiliza kesi hiyo, haikuwa na uwezo wa kutoa amri ya utekelezaji wa mapendekezo ya Tume.

Alikubaliana na Mwanasheria Mkuu wa serikali kwamba amri ya kukaza hukumu yoyote mahakamani hutolewa baada ya kusikilizwa kesi yote; hatua ambayo ilimaanisha kuwa shauri hilo lingekuwa limesikilizwa kwanza mahakamani na siyo maamuzi kutoka Tume.

Ndipo kituo cha sheria, kikishirikiana na mawakili Francis Stolla na Alex Mgongolwa, walikata rufaa mahakama ya rufaa.

Shauri hili linahusu malalamiko ya wanakijiji kwa Tume ya Haki za Binadamu dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Kamanda wa Polisi wa Wilaya na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mwaka 1993 eneo katika wilaya ya Serengeti, liliandikishwa kuwa kijiji. Mwaka 1994, sehemu kubwa ya ardhi ya kijiji hicho ikachukuliwa na kufanywa Hifadhi ya Wanyama ya Ikorongo na kijiji kubaki na eneo lililoitwa Nyamuma.

Tarehe 8 Oktoba 2001 tangazo kupitia kipaza sauti liliamuru kuwa ifikapo tarehe 12 Oktoba 2001 wananchi wawe wamehama kutoka sehemu waliyokuwa wamebaki nayo (Nyamuma Iliyobaki).

Ilipofika tarehe hiyo wakazi wa eneo hilo waliondolewa kwa nguvu huku nyumba zao zikichomwa moto ambapo msimamizi mkuu wa operesheni hiyo alikuwa Mkuu wa Wilaya, Thomas Ole Sabaya.

Katika shauri hili la wanakijiji, Kituo cha Sheria na mawakili wao Francis Stolla na Alex Mgongolwa, walikuwa wanataka iamuliwe kuwa wanakijiji warejeshwe kwenye maeneo yao. Tume ilikubaliana na walalamikaji.

Tume ilielekeza mapendekezo yake kwa mamlaka husika ambayo ilikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyetokea kuwa mlalamikiwa wa tatu. Tume ilisubiri kuona utekelezaji wa mapendekezo yake ndani ya miezi mitatu, kwa mujibu wa kifungu cha 28 (2) cha sheria, Sura 391.

Badala ya kuona utekelezaji, Tume ilipokea, tarehe 18 Mei 2005, majibu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (wakati huo Andrew Chenge) akisema serikali haitatekeleza mapendekezo husika.

Hatua hii ilifuatwa na walalamikaji kukata rufaa Mahakama ya Rufaa. Jopo la majaji watatu lilisikiliza shauri hili. Nao ni Jaji Mkuu Agustino Ramadhani, Jaji Damian Lubuva na Jaji Harold Nsekela.

Mahakama ya rufaa ilipitia uamuzi wa mahakama kuu pamoja na hoja za mawakili wa pande zote mbili na kujiridhisha kwamba kwanza, Tume ilikuwa na wajibu wa kupokea malalamiko ya uvunjwaji wa haki za binadamu, na kuyachunguza, ikiwa ni moja ya majukumu yake kwa mujibu wa kifungu cha 6 (1) cha Sura ya 391.

Pili, majaji wa mahakama ya rufaa walitambua kwamba Tume ikifanya uchunguzi inaweza kubaini moja ya mambo sita yanayotajwa katika kifungu cha 28 (1) (a) – (f) cha Sura ya 391 ambayo ni pamoja na kuvunjwa kwa haki za msingi, kukiukwa kwa sheria, uonevu, na kutumia madaraka vibaya.

Tatu, majaji walisema Tume ikibaini moja ya mambo hayo, lazima uamuzi wake upelekwe kwa “mamlaka husika” kwa mujibu wa kifungu cha 28 (2) cha Sura ya 391.

Nne, mamlaka husika inabidi itoe taarifa katika Tume ndani ya miezi mitatu ikieleza hatua ilizochukua kurekebisha suala lililokiukwa, kama ni la haki za binadamu au utawala bora.

Tano, iwapo mamlaka husika ikikataa kutoa taarifa au kutekeleza maelekezo ya Tume, ndipo kifungu cha 28 (3) kinapotumika kwa kuiomba mahakama itoe amri ya kutekelezwa kwa mapendekezo hayo.

Mfano fundisho ni ule wa Ghana. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Ghana ilitoa uamuzi kwamba kampuni iliyofutiwa leseni ya madini na Waziri wa Madini na Nishati irudishiwe leseni. Mamlaka husika haikufanya hivyo. Tume ikapeleka uamuzi wake mahakamani ili ukazwe. Mahakama ikakubali.

Mahakama ya rufaa imeamuru shauri la wanakijiji cha Nyamuma Iliyobaki lirudi mahakama kuu mbele ya jaji mwingine ambapo waombaji wawe ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na wananchi 135 wa Kijiji hicho. 

Aidha, Tume imetakiwa kumshauri Waziri wa Sheria na Katiba kutunga kanuni za utaratibu wa utekelezaji wa mapendekezo/maamuzi yake.

Mawakili Francis Stolla na Alex Mgongolwa ndio waliowasilisha maombi hayo Mahakama Kuu.

0
No votes yet