Tume ya uchaguzi ya Z’bar imepata, ikapatikana


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 13 October 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imepata na papo hapo ikapatikana. Katikati ya wiki iliyopita, ililitoa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar.

Haijapata kutokea. Tume kulitoa daftari la wapiga kura imekuwa kama ni jambo la najisi kama siyo dhambi kubwa. Visingizio vingi hutolewa kulizuia, lakini kutobanwa na sheria ya uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 1985, kulitumika kama mwanya.

Imeshazoelezeka kwa vyama vya kimageuzi kupatiwa daftari la wapiga kura siku tatu au mbili kabla ya siku ya upigaji kura. Ndivyo ilivyofanyika katika uchaguzi uliopita. Siku mbili tu.

Hapo daftari huwa halina manufaa kwani hakuna muda wa kulihakiki kwa mujibu wa watu walioandikishwa vituoni wakati wa uandikishaji.

Daftari la wapiga kura ni orodha ya wananchi wote walioandikishwa na tume kwa ajili ya kupiga kura siku inapowadia, husaidia kugundua majina bandia au batili yaliyoingizwa kwa lengo la kuharibu uchaguzi.

Ukijiuliza ni kwa nini hasa Tume inazidi kulidhibiti daftari badala ya kulitoa kwa vyama ambavyo vinasikilizwa na wananchi wengi, hupati jibu muafaka.

Ukitafakari sana utaishia kudhani kwamba labda kuna mipango ya kuvuruga uchaguzi na kusaidia wanasiasa waliopo madarakani dhidi ya hatari ya kupoteza uchaguzi. Ukiyaona majina ya wapiga kura katika muda mzuri, maana yake watachunguza na kugundua uchafu ndani yake.

Katika nchi zisizofuata vizuri misingi ya utawala bora na utawala wa sheria, hasa barani Afrika, inajulikana namna tume za uchaguzi zinavyosaidia mikakati ya ushindi inayoandaliwa na vyama viliopo madarakani.

Kuna watu hupandikizwa ili kuja kupiga kura. Katika nchi hizi, utamaduni wa “Mtu mmoja kura moja” haujazoeleka na hautakiwi na watawala. Na hii ndio njia ya kuiba kura kwa sababu daftari linapofichwa, ni kuongeza usiri kwenye uchaguzi.

Mwisho wa siku kitakachofahamika na kushutumiwa kutendeka, ni kwamba tume imebeza sauti ya wananchi na kuamua, iwe kwa makusudi au kwa kulazimishwa na watawala, kukibeba chama kilicho madarakani. Ni kukihifadhi na aibu ya kushindwa uchaguzi.

Baada ya uchaguzi wa 2005, tume ilikuja kutangazia wananchi kwamba daftari lilikuwa na wapiga kura waliobainika kuwa walijiandikisha kwa zaidi ya mara moja. 

Tayari hapo, haiwezekani kuwa na uchaguzi huru, wa haki na ulio wazi. Hautakuwepo kamwe.

Lakini, siku zinapita na mambo yanabadilika. Safari hii, baada ya madai ya viongozi wa vyama vya kimageuzi kuimarika na shinikizo zinazotolewa na asasi za kiraia zilizopo ndani na nje ya nchi juu ya tume kutakiwa itende haki kwa kusimamia uchaguzi kwa uadilifu, tume imelitoa daftari la wapiga kura kwa vyama vya siasa.

Ilikuwa ni katikati ya wiki iliyopita. Mwenyekiti wa Tume, Khatibu Mwinchande, aliitisha mkutano na viongozi wa vyama vya siasa na kuwakabidhi daftari baada ya kuwahutubia kwa saa nzima akihimiza umuhimu wa kulitunza.

Tangu hapo, vyama vimekuwa vikilipitia na kuangalia majina ya wapiga kura huku wakilinganisha na majina yaliyoandikishwa vituoni ambako walikuwa na mawalaka wao wakati wa uandikishaji wapiga kura.

Mapitio kama hayo ndiyo huthibitisha uhalali wa majina. Bali pia kwa kupata orodha ya wapiga kura mapema namna hiyo, vyama vitaweza kujenga uwezo wa mawakala wao ili kuwa makini siku ya upigaji kura wasije kupenya wapiga kura mamluki.

Kwa kutoa daftari mapema hivi, tume imepata alama nyingi kwamba imekusudia kuthibitishia wananchi kuwa haina nia mbaya uchaguzi huu. Kwamba itatenda haki na kwa mujibu wa sheria hadi siku ya utangazaji matokeo ya uchaguzi.

Lakini, baada ya alama hizo nyingi ambazo zingesaidia watu kujenga imani zaidi kwa tume yao inayosimamia uchaguzi, kuna mapya yanatokea mitaani ambayo najua yanaishusha hadhi ya tume.

Kuna shahada za wapiga kura zinatembea kwenye mamlaka ya masheha na haijulikani zimewafikaje masheha ingawa kuna fununu kuwa wamekabidhiwa na tume yenyewe ya uchaguzi.

Ndani ya jimbo la Kwamtipura, katika manispaa ya mji wa Zanzibar, idadi fulani ya shahada zimekutwa na sheha wa eneo husika anaeleza kuwa amepewa na “watu wa tume ya uchaguzi.” Alipoulizwa alipopewa aliambiwa afanye nini, akasema, “niwagawie watu wangu katika shehia.”

Inawezekana majibu yake yasiwe ya kweli. Lakini amekutwa na shehena ya shahada zisizojulikana idadi yake. Swali hapa ni je hizi shahada za wapiga kura ni za nini kwa sheha yeyote yule? Kwani dhamana ya shahada si wanayo tume ya uchaguzi? Sasa imekuaje shahada zikutwe kwenye mamlaka ya sheha, kiongozi wa mtaa ambaye ni kada wa CCM?

Haya yanatokea wiki tatu hivi tangu wakuu wa tume watangaze kwamba bado kuna shahada 10,234 hazijachukuliwa na wenyewe.

Tume ilipokutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi katikati ya mwezi uliopita, ilisema katika idadi ya wapiga kura 407,075 walioandikishwa, 10,234 hawajafika ofisi za wilaya za tume kuchukuwa shahada zao.

Wakati huo walisema walikuwa wanatarajia kuzihodhi shahada hizo makao makuu ya tume na zitakuwa tayari kuchukuliwa na wenyewe wakitokea.

Siku chache tunashuhudia shahada za wapiga kura zikiishia mikononi mwa viongozi wa mitaa. Tume haijasema lolote wakati kwa wiki nzima taarifa hizi zimezagaa mitaani mjini Zanzibar.

Mbaya zaidi ni hizi taarifa kwamba kuna vijana waliokuwa safarini nje ya nchi wameshindwa kupata shahada zao walipokwenda ofisi za Tume zilizopo Maisara. Walijibiwa kuwa hazionekani baada ya kutafutwa kila kipembe na wenyewe wakiona hamkani za watumishi wa tume hiyo.

Kinachoshangaza, mmoja wa vijana hao, aliporudi mtaani kwao, ghafla alihadithiwa kuwa shahada yake ya kupigia kura imekutwa kwa sheha wa shehia yake. Shahada haipo tume bali ipo kwa sheha. Miujiza au nini? Lahaula.

Hili linahitaji maelezo yakinifu ya mkurugenzi wa uchaguzi katika tume. Haiwezekani libaki katika kitendawili namna hii kwa sababu kuliachia ni kufuga uovu.

Tume wangejua kwamba wananchi wanasimuliana kwamba “watu wa rais” wameshika baadhi ya shahada na kuzipeleka kwake na kumkabidhi wasingefanya mzaha na suala hili. Laiti tume ingejua – na inawezekana wakuu wake wanazo taarifa hizi – kuwa mitaani wananchi wanaelezana kuwa hata na viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) wanazo shahada hizi, wasingetulia vitini mwao. Kwanini wametulia hawaelezi kilichofanyika?

Kuacha ukungu huu kunaipunguzia alama za imani tume. Haitaaminika na haitaaminiwa; na kwa hivyo; tume itakuwa haijajisafisha kutoka mizengwe iliyoshuhudiwa katika uchaguzi mkuu wa 2005 ambapo mtu mmoja alipiga kura atakazo halafu uchaguzi ukaitwa huru na wa haki.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: