Tume ya Warioba


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 18 April 2012

Printer-friendly version

JAJI Joseph Warioba anaweza kukwama kuunganisha tume ya kuratibu maoni ya katiba mpya ambayo ameteuliwa kuiongoza, MwanaHALISI linaweza kuripoti.

Warioba atalazimika kwanza kutafuta sauti ya pamoja katika tume hiyo kwa sababu ina wajumbe wenye mitizamo tofauti kuhusu masuala yanayopaswa kujadiliwa.

Mvutano unatarajiwa kutokea pale wajumbe wa upande wa Zanzibar watakaposhikamana na kushinikiza msimamo wa Wazanzibari wa kutaka mfumo mpya wa Muungano wa Tanzania.

Ufuatiliaji wa maoni yanayoendelea kutolewa na wananchi sehemu mbalimbali za nchi tangu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilipopitishwa na bunge mwaka jana, umebaini hatari ya mwenyekiti kukabiliwa na upinzani.

Warioba, mtaalamu wa sheria aliyewahi kuwa waziri mkuu na makamu wa rais na mwenyekiti wa tume ya kuchunguza tatizo la rushwa nchini, mwenyewe ana msimamo wake kuhusu mfumo wa uendeshaji Muungano.

Kwa nyakati mbalimbali, Warioba amenukuliwa akitetea, kwa kauli nzito, mfumo uliopo wa Muungano wa serikali mbili, kiasi cha kushangaa watu wanaotaka mabadiliko.

Amekuwa akiwataja watu hao kuwa ndio wenye tatizo na ingefaa wakasema tu wanataka kuuvunja Muungano na kwamba wengi wao ni wanasiasa wanaowania madaraka.

Julai mwaka jana alikaririwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) akisema Muungano uliopo bado ni imara lakini wanaosaka madaraka ndio wanaoufanya uonekane una matatizo.

Warioba alisema baadhi ya watu wanasema mfumo wa serikali tatu ndio utamaliza kero za Muungano. Yeye anasema hilo halina ukweli wowote.

Amesihi wale wanaotaka serikali tatu ndani ya Muungano wasijidanganye, kuwa ikiwepo serikali ya aina hiyo, kero hizo zitamalizika.

“Wapo wanaohitaji serikali tatu; eti wanaona hilo ndilo jawabu, hawajiulizi, je, serikali tatu hazitakuwa na changamoto zake? Na kama zikija, changamoto hizo zinamalizwaje,” alihoji.

Oktoba 2011, alinukuliwa akirudia kauli hiyo kwa gazeti moja nchini akisema, “(Watanzania) tusipokuwa makini kwa maneno yanayozungumzwa sasa, tutavunja Muungano.”

“Tunayo matatizo ya madaraka… unazo serikali mbili kwa hiyo yale yaliyomo kwenye orodha ya Muungano ni kuonyesha serikali hii ina madaraka gani. Wanagombania madaraka.

“Kama suala ni mafuta au mengine, tuzungumze. Inategemea mnavyokubaliana, tusije kuongeza au kupunguza kwenye orodha mambo ambayo yatakuja kuwatenganisha wananchi.

“Sasa hivi kiini ni ugomvi wa madaraka kati ya serikali ya Muungano na serikali ya Zanzibar. Hivi ukileta serikali tatu, ugomvi huu hautakuwapo?

“Ukileta serikali ya Tanganyika yenyewe haitadai madaraka? Mwisho wataomba madaraka hadi serikali ya Muungano isiwe na chochote,” amewahi kueleza.

Warioba amewahi kuhoji, “…hivi serikali ya Tanganyika kwa mfano ikiwapo, ikataka iwe na wimbo wake wa taifa, bendera yake, nembo yake, kisha inadai ifanye biashara ya nje, unafikiri tutakuwa tumefika wapi?

“Ni kwamba tutakuwa tunaondoa Muungano na kurudisha Tanganyika na Zanzibar. Lakini kama wananchi wanataka hivyo, sawa,” amesema kwa msononeko.

Amesema: “Lakini tukivunja Muungano madhara yake ni makubwa sana kwa pande zote mbili. Mimi naamini wale wanaotaka serikali tatu wanajua nia yao ni kuvunja Muungano na huu ndio ukweli. Ukianzisha serikali tatu, maana yake unavunja Muungano.”

Msimamo wa Muungano wa serikali mbili unaweza kuridhiwa na Watanzania wa Bara. Kwa Wazanzibari, mfumo huo haukubaliki ingawa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikishajiisha watu wauendeleze.

Hali hiyo ndiyo hasa inayotazamwa kuleta uwezekano wa kuwepo mvutano ndani ya tume hiyo ambayo ina wajumbe 15 kutoka Bara na 15 kutoka Zanzibar.

Baadhi ya wajumbe wa Zanzibar wamezungumza na MwanaHALISI na kueleza wazi kuwa watataka jambo hilo liwekwe wazi “mapema hata kabla ya tume kuanza kazi.”

Kwa muda mrefu sasa, wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakihoji mfumo wa serikali mbili kwa kusema umenyang’anya mamlaka ambayo Zanzibar ilipaswa kuwa nayo katika mambo kadhaa yakiwemo yasiyo ya Muungano.

Historia ya Muungano ulivyoanzishwa na ulivyoendeshwa, imeleta utata mkubwa kwa wananchi. Tangu Rais Kikwete alipotangaza ujio wa katiba mpya, hisia za Wazanzibari zimezidi kuguswa. Wanataka mabadiliko.

“Mmekuwa mkiona kwenye vyombo vya habari namna Wazanzibari wanavyopinga mfumo uliopo. Wanataka mabadiliko na sasa kumeibuka hoja mpya ya kutaka Muungano wa Mkataba. Jambo hili linahitaji kuwekwa sawa,” amesema mjumbe mmoja.

Mjumbe mwingine ambaye naye ametaka asitajwe jina gazetini, amesema kinyume na kauli ya Rais Kikwete kuwa Muungano usijadiliwe katika mwelekeo wa kusema uwepo au usiwepo, bali katika “kuuimarisha tu,” anaona suala hilo halijawekwa vizuri.

Amesema, “Huwezi kuimarisha Muungano usioridhika na mfumo wake. Lazima useme ni mzuri au mbaya. Lakini Wazanzibari ambao ndio tunaowawakilisha, wanapinga mfumo wa serikali mbili kwa kuamini umewakandamiza.

“Pia hawataki mfumo wa serikali moja maana utawamaliza. Hapo lazima wasikilizwe na maoni yao yazingatiwe kama tunataka Muungano wenye maridhiano.”

Katika wajumbe wa Zanzibar, yumo Dk. Salim Ahmed Salim, waziri mkuu wa zamani ambaye mwishoni mwa mwaka jana alikaririwa na gazeti moja nchini akisema, Watanzania wa pande zote mbili wanayo nafasi ya kutoa maoni kwa uhuru ikiwemo kuamua wanataka muungano wa aina gani.

“Zanzibar wana dukuduku lao; Tanzania Bara wana dukuduku lao; ni muhimu wakubaliane kikatiba,” alisema Dk. Salim katika mahojiano yaliyofanyika mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema jambo la msingi kwa sasa ni wananchi kupewa nafasi ya kutafuta ufumbuzi wa dukuduku hizo kwa njia ya mjadala utakaoendeshwa kupitia mchakato wa kuratibu maoni ya wananchi juu ya katiba mpya.

Amesema itakuwa vizuri vyama vya siasa vikikaa kando ili kuwaachia wananchi waeleze vile wanavyotaka katiba iwe; na ni muhimu maoni yao yakaheshimiwa na kuzingatiwa.

“Watanzania siyo roboti, kila mmoja ana akili na fikira zake; muhimu ni kulinda umoja wetu na wananchi hasa wa vijijini kupewa nafasi zaidi ya kutoa maoni juu ya katiba yao,” alisema Dk. Salim.

Mwezi uliopita, Awadh Ali Said, mjumbe kutoka Zanzibar, akiwa kwenye mhadhara wa kuhimiza watu kutoa maoni ya katiba alisema, “Tukizingatia ukweli kuwa wananchi wa nchi mbili hizi hawajawahi kupata fursa ya kutoa maoni juu ya suala la Muungano, ilitegemewa Muungano uwe ndio hoja kuu ya mjadala wa katiba.”

Alisema sio tu kwamba suala la Muungano liwe msingi katika mjadala wa katiba; bali linastahili kuamuliwa mwanzo na ndiyo baadae lije suala la katiba. Muungano ndio uliozaa katiba tulizonazo: Katiba zote mbili (ya Zanzibar 1984 na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977),” ameeleza.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: