Tumebana bajeti ya kilimo ili iweje?


Joseph Mihangwa's picture

Na Joseph Mihangwa - Imechapwa 01 July 2008

Printer-friendly version
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira

KILIMO na maji ndiyo sekta zilizopangiwa fungu dogo zaidi kibajeti kwa mwaka wa fedha ulioanza jana, Julai mosi.

Sekta ya maji imepewa Sh. 230 bilioni na kilimo ikapewa Sh. 460 bilioni. Uchungu wangu uko zaidi kwenye sekta ya kilimo, iliyopewa sawa na asilimia 6.4 ya bajeti yote ya jumla ya Sh. 7.216 trilioni.

Sekta nyingine zimepewa: Elimu Sh. 1.43 trilioni; Miundombinu Sh. 973. 3 bilioni; Afya Sh. 803.8 bilioni na Nishati Sh. 388.4 bilioni.

Kilimo kimedharauliwa. Mgao kiliopatiwa ni matokeo ya kuonekana hakisaidii ukuaji wa uchumi wa taifa. Kwa miongo 20 mfululizo, taifa letu limekuwa likikabiliwa na uhaba wa chakula, licha ya kuendelea na kaulimbiu ya 'kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi wetu.'

Mwaka 2006, serikali ililazimka kuagiza chakula nje na ikatumia fedha nyingi. Kwa miaka yote, nchi yetu imekuwa mbele katika kuomba chakula. Ni matokeo ya sera mbovu dhidi ya kilimo. Inasikitisha viongozi wetu hawajifunza kitu, kiasi cha mtu kuthubutu kusema 'labda kuna mkono wa mtu anayeshirikiana na mataifa makubwa ili kutuangamiza.'

Nchi tajiri hupenda kushauri nchi masikini ikiwemo Tanzania namna ya kutibu tatizo la uhaba wa chakula ambao wanasema husababishwa na majanga, ongezeko la idadi ya watu, uvivu na ukosefu wa utawala bora.

Sababu hizi hazikubaliki kwa baadhi yetu. Wengine tunaamini kuwa Benki ya Dunia na Shirika la Chakula Duniani (FAO) ndio yanachangia tatizo hili.

Wachumi wa Benki ya Dunia ndio hushinikiza uzalishaji wa mazao ya biashara kwa gharama ya mazao ya chakula; ni wao waliorahisisha kukopa fedha benki kwa ajili ya kilimo cha chai au kahawa badala ya kilimo cha mpunga au mahindi; wao ndio walioweka vivutio kwa maisha ya mijini badala ya vijijini na kusababisha nguvu kazi kubwa ambayo ni vijana, kukimbilia mijini.

Kwa sababu ya kujua au kutojua au kwa kutii masharti ya nchi tajiri na mashirika yao, viongozi wetu wamepokea na kutekeleza sera shinikizo na kuzitumia kama msingi wa mipango ya maendeleo.

Haishangazi sasa kuona serikali inatenga fungu dogo kuhudumia kilimo. Viongozi wanaamini au pengine wanalazimishwa na nchi tajiri, kuamini kilimo si kipaumbele.

Hakuna tatizo katika ongezeko la idadi ya watu. Tatizo ni watu kupungua maana nguvu kazi inapungua. Tanzani tuna raslimali nyingi ambazo zikitumika vizuri, tutapata chakula cha kutosha kuliko ilivyo sasa.

Kinachokosekana ni kiongozi mwenye utashi wa kuonyesha njia na kuzingatia mahitaji halisi ya nchi. Hebu tutazame, Afrika yenye watu wachache zaidi duniani kwa kuzingatia mita za mraba, ingali inatishiwa na tatizo la chakula, lakini Ulaya yenye idadi kubwa zaidi ya watu kwa kuzingatia mita ya mraba, inazalisha chakula cha kutosha na cha ziada.

Tatizo letu ni uzalishaji mdogo. Na utaendelea iwapo serikali haitoi fungu la maana ili kukuza uzalishaji mazao ya chakula. Ikisikiliza masharti ya Benki ya Dunia na nchi tajiri, itaendelea kutilia mkazo uzalishaji mazao ya biashara ambayo yanatakiwa na nchi tajiri kwa maslahi yao.

Nchi nne za Asia zilizojijengea jina la Four Tigers kwa sababu ya uzalishaji chakula kingi zaidi duniani; China, Vietnam, Korea Kusini na Taiwan zina maeneo madogo ya ardhi kuliko ilivyo Tanzania. Wanazalishaje chakula kingi?

Viongozi wao wamezingatia mahitaji ya nchi zao na kudharau mapendekezo ya matajiri. Wachumi wa Benki ya Dunia wanaokubalika Marekani pamoja na wale wa Jumuiya ya Ulaya, wana mipango isiyo tija kwa nchi masikini. Bado ndio wansikilizwa na Tanzania.

Wanaheshimu sera za kuwapa motisha wakulima ili wapate bei nzuri ya mazao, lakini uzalishaji wa mazao ya chakula unashuka. Kilimo kinawakifu vijana na kukimbia vijiji vyao kuhamia kwenye miji ili kutafuta maisha bora.

Ni wazi bei ya chakula inapopanda kwa walaji wa mijini hupandisha pia bei ya bidhaa za viwanda ambavyo vingi ni vya nchi tajiri. Kile anachopata mkulima katika nchi masikini, hakimtoshi kununua mahitaji yake ya kila siku hasa katika wakati ambao bei ya mafuta nayo hupanda kwa kasi ya roketi.

Njaa haiwezi kwisha kwa kushajiisha maendeleo ya teknolojia maana matumizi ya teknolojia huwa na tabia ya kuathiri mfumo wa maisha y jamii: tunaona namna teknolojia inavyohimizwa zaidi kwenye uzalishaji wa mazao biashara kuliko ya chakula.

Teknolojia ya kilimo ina maana kununua zana zinazozalishwa na viwanda vya nchi tajiri. Nchi masiniki zinapeleka fedha za kigeni huko kupata zana hizi huku zikilazimika kulipa zaidi ili kununua pembejeo za kilimo ambazo hazijawahi kutosheleza mahitaji ya wakulima.

Tunaposhinikiza wakulima wadogo watumie zana za kisasa (trekta, mashine za kupandia, kupalilia na kuvunia) tunajidanganya kwa sababu hatua hiyo inaweza kuua ubunifu wa kiteknolojia na uwezo wa kujitegemea.

Mwalimu Nyerere hakukosea aliposema: 'Kilimo cha jembe kitaondolewa na plau; plau itaondolewa na trekta; na trekta litaondolewa na mashine kubwa kubwa za kulima na kuvuna.'

Mkulima wa Tanzania bado anatumia jembe la mkono. Atafikia lini kutumia mashine kubwa? Uko wapi utaratibu wa kumuendeleza ili kufikia huko? Haupo wala serikali haijafikiria hili na hiyo maana yake bado anaendelea kupuuzwa asizalishe chakula kingi.

Ndio sababu ya kulaumu sekta ya kilimo kupewa fungu dogo la bajeti. Asilimia sita haitoshi kumwezesha kubadilika ili afikie kutumia mashine kubwa katika uzalishaji mahindi na mpunga.

Bajeti inayotakiwa ni ile ambayo itajenga msingi wa kuimarika sekta ya kilimo kwa maana ya kumwezesha mkulima wa Tanzania kubadilika na kutumia sayansi katika shughuli zake. Hii inatakiwa kufike angalau asilimia 30. Kilimo ndicho kinachoajiri zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania, iweje kipewe fungu dogo?

0
No votes yet