"Tumekubamba Mbeya Vijijini"


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 28 January 2009

Printer-friendly version
Uchambuzi

ACHA! Unavaa? Kaa ulivyo wakuone. Hivyo ndivyo ulivyo. Ndiyo sura yako halisi. Ndivyo matendo yako yalivyo. Kaa ulivyo wakuone.

Uko Mbeya baba. Uko Mbeya mama. Mbeya hakuna umbeya, utaumbuka. Hayo sasa yamekukuta. Huvui, huvai, unatetema kama kikongwe. Umekutwa pabaya. Hukani, hukiri shitaka!

Kwenye orodha ya wapiga kura kuna mamia walokufa. Mbeya Vijijini. Hawa watapigaje kura? Tunajua wangepiga kura. Walikuwa wanataka kupiga kura; ndiyo maana walijiandikisha. Lakini sasa hawapo.

Umewatoa wapi walioko akhera? Kwa nini wawasumbua wale walopumzika? Kwa nini wavuka mipaka, wa huko hawatakiki hapa na kwao kura muhali? Uswahiba gani huo hadi kuita maiti mamia?

Kaa ulivyo wakuone; umeyataka mwenyewe. Na hawa je? Majina yao yapo hapa yapo pale. Wamejiandikisha mara mbili. Huenda wengine mara tatu. Na mwenyekiti wa chama kizee yumo; jinale limetinga mara kadhaa.

Jinai! Jinai! Hata kiongozi mwandani wa watawala kasaini mara hizo! Hajui sheria? Hajui taratibu? Si naye mwalimu taratibu kuelekeza? Vipi jinale mara hizo? Sainiye mara hizo. Kura ataka kupiga zaidi ya mara moja? Hahaaa! Anaibipu sheria? Hatua gani kachukuliwa?

Kaa ulivyo wakuone wewe! Wafu huwaoni? Walojiandikisha mara mbili, nao huwaoni? Uko wapi walakini: Machoni au akilini? Au makusudi wafanya mwenziyo kupendelea? Ni wewe wajua.

Huna aibu. Ushindi watangaza. Macho makavumakavu utadhani ni salama. Utadhani ni sahihi. Jinai wafunika, upendeleo washushia na kibindo chatuna. Huyooo! Watangaza ushindi wa kishindo pasipo hata mulisi. Kaa ulivyo kukuona wakuone.

Masanduku ya kura kila mmoja wampa. Nyara nyeti za serikali wagawa kama karanga. Nyumba za nduguzo wafanya kama tunzio, kwa mrahaba au burebure? Nani huko haki ya mtu kulinda?

Masanduku hushikwa wale tu waloapa. Hata kama kwa ujanja lakini sheria wamekidhi. Hata kama majizi kanuni wametimu. Kwa mkuu wa nyumba saba za chama kizee masanduku kulikoni? Usijitingishe. Kaa ulivyo wakuone.

Masanduku yalivyo yastahili ulinzi. Siyo mtu kujibebea na “mchanga” kutumbukiza. Polisi na wengine walinzi jukumu hilo ni lao. Vipi Nyani na Ngedere wakutwe na mali – haki ya mpigakura, bila ulinzi; bila kiapo, bila halali?

Tumekubamba kikweli, huna pa kukimbilia. Pembejeo waona wapewa wa chama kizee, tena kwa kadi kijani. Wewe kimya! Kauli halifu zatanda na wewe kimya chanoga. Huna macho, huna mdomo, mbona wapigwa utata? Kaa ulivyo; hivyohivyo wakuone na kukifu.

Nyetizo tumeziona, bora ukae ulivyo. Watangaza mambo safi kila kitu kwenda salama. Subiri. Jana ndiyo leo na vituo havina majina ya wapiga kura. Saa moja, mbili, tatu, na hiyo ni hapa makao makuu ya kata tu; mita chache kutoka ofisiyo.

Na huko vijijini kukoje? Uliko limekorogeka. Kila kilometa kutoka uliko kila mmoja ufalme kujitangazia. Taratibu zinatupwa. Kanuni zinapuuzwa na kubezwa. Sheria ama hazifahamiki au zinakimbiwa. Usimamizi wako – bila taratibu, kanuni wala sheria unazaa wizi wa kishindo.

Si ndivyo ulivyo na wako walivyo? Hustuki, huogopi wala aibu huoni. Macho makavumakavu vifungu vya sheria wataja. Nyuma ya pazia watanda ulaghai na wizi, haki ya raia yaporwa.

Limechanika! Lakini lilikuwa bandia lile pazia. Kumbe lilikuwa la ukungu si nguo wala turubali wala ukuta. Limeyeyuka haraka utupu kukuacha. Kaa ulivyo wote wakuone.

Acha wakuone basi. Waone kazi yako. Wakupe maksi au wakunyime. Hivyo hivyo ulivyo ndivyo watakuona, watakuelewa. Huhitaji kujiremba kwa suti, vitenge na manukato. Ulivyo kama ulivyo, ndivyo watakuelewa. Kaa hivyo.

Mbeya siyo mwanzo siyo mwisho. Tumeyaona likichomoza hadi linapozama. Tumeyashuhudia kichanga kikinyonya hadi kimezeeka. Tumeyasikia na yametusibu; tumekerwa na kukereka; vilio vimetutoka lakini ni mawe tuyaambiayo.

Kaa hivyo ulivyo wajue uwezo huna. Wajue vifaa huna. Waelewe watendaji huna. Wajue kwa fadhila wewe waenda na mwoga wa kusema ulivyo hadi wakukute; wakubambe uki…

Acha wakuone. Uumbuke. Ujiumbue. Kwani wewe huna mdomo. Mbona husemi? Kwani wewe huna macho. Mbona huoni? Kwani wewe huna akili. Mbona hufikiri? Unasema utabaki ulivyo, kama walivyokufinyanga. Utanyonya hadi lini?

Kaa hivyo ulivyo, wajue huna uwezo. Kwamba una kazi lakini nyenzo huna. Huna hata raslimaliwatu. Uliipataje kazi hii? Ulipewaje? Au walokupa kazi walitaka usitende. Uwe nayo lakini usiifanye. Au uifanye lakini kwa mapungufu mengi. Au usiifanye vizuri ili walokupa wafurahi na kila mashindano waibuke mbele ya wengine.

Wala usijisikie vibaya. Kaa ulivyo wakuone. Ulitendalo walione. Wajiulize kama nifanyavyo mimi. Wajipekue akili na kudadisi: Vipi upewe kazi ili usiifanye? Si mwendo wa kurudi nyuma huo?

Nyuma utakwenda. Utakwenda. Lakini mpaka lini na mpaka wapi. Labda mpaka kurudi nyuma kutakapokuwa kwenda mbele. Basi hakutakuwa tena na kwenda mbele au nyuma. Itakuwa mvurugano na mikanganyiko.

Wewe kaa ulivyo; usijitingishe, usifanye juhudi za kujificha kwani umeonekana. Hiyo nayo bahati yako kuonekana ulivyo. Sasa hakuna atakayekulaumu. Kila aliyekuelewa atakuchukulia ulivyo: mwaminifu, mchumia tumbo, mwoga, kibaraka, mtumwa. Vyovyote watakavyokuona.

Kitu kimoja ni kwamba hawawezi kukupima peke yako. Watampima mwajiri wako pia. Nia na shabaha yake. Uwezo wake. Sababu za kukuweka kama ulivyo.

Nawe ni mtu. Ni hapa ulikozaliwa kuwa? Ili uweze kubambwa ukiwa hivi ulivyo? Na kila ukibambwa ugegeme tu; upigapige kope na kuzamisha kichwa shingoni ukisema “mambo ya watu haya?”

Shukuru Mungu umebambwa. Siri yako haipo tena. Mshindi ni wewe au washindani? Amua. Uvae au ubaki ulivyo. Ili iweje?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: