Tumekwama, turejee kwa Nyerere


Renatus Mkinga's picture

Na Renatus Mkinga - Imechapwa 07 April 2010

Printer-friendly version

HUU ni mwaka wa uchaguzi. Ni uchaguzi mkuu wa nne kufanyika nchini tangu kuzikwa kwa udikteta wa mfumo wa chama kimoja miaka 18 iliyopita.

Mtu yeyote makini lazima atatafakari ni wapi taifa hili linaelekea, hasa baada ya chaguzi tatu kumalizika. Kwa maoni yangu, taifa hili linakoelekea si kuzuri.

Kwanza, uchaguzi mkuu wa Oktoba unafanyika wakati taifa likiwa katika ombwe kubwa la uongozi.

Ni jambo ambalo halijapata kutokea kwa viongozi wastaafu kuibuka hadharani na kumtaka rais kuchukua maamuzi magumu ya kufikisha watuhumiwa wakuu wa ufisadi mahakamani, vinginenvyo azuiwe kugombea ngwe ya pili ya urais.

Hili limefanyika wakati huu wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete.

Pili, haikutarajiwa kwa kiongozi mkuu wa serikali kutoa kauli kuwa hafahamu kwanini Tanzania bado ni maskini, hata baada ya miaka 45 ya uhuru pamoja na utitiri wa rasilimali zake.

Lakini Rais Kikwete mwenyewe ametamka hili alipohojiwa na gazeti la Finantial Times la Uingereza. Hii inathibitisha kuwa taifa linakabiliwa na tatizo sugu la kukosekana kwa viongozi wenye muono.

Tatu, serikali au chama makini, kisingemruhusu Yusuph Makamba, katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kushambulia wakosoaji wa serikali hadi kufikia hatua ya kuwaita “wehu na wenye chuki binafsi,” tena kurejea kauli hiyo mara kadhaa.

Walengwa wa mashambulizi ya Makamba, hawakuwa waandishi wa habari. Ni viongozi waandamizi katika chama, wastaafu katika serikali na wengine wakubwa zake kiumri.

Alikuwa anawazungumzia mawaziri wakuu wastaafu, Dk. Salim Ahmed Salim na Fredrick Sumaye, kwamba hawana sifa ya kuzungumzia mapungufu katika utawala wa Kikwete.

Alidai kuwa hao walikuwa washindani wa Kikwete katika mbio za urais ndani ya chama chake, na kwamba walipokuwa serikalini walishindwa kuleta wanachokidai.

Nne, Mnajimu Yahya Hussen naye amejitokeza na kuonya juu ya yeyote atakayempinga Kikwete toka ndani ya CCM, haswa yule mwenye sifa za kumzidi, si kama John Shibuda, “atakutwa na kifo cha ghafla.”

Kinachotia utamu katika hili, ni kauli ya ikulu kwamba hayo ni maoni yake binafsi na ni vyema yakaheshimiwa.

Lakini tumefikaje hapa tulipo? Jibu liko wazi. Chanzo cha yote haya ni Benjamin Mkapa. Ni Mkapa aliyevuruga, kwa maslahi yake binafsi, ule utaratibu ulioweka na uongozi thabiti wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa mtu mmoja kura tatu.

Uamuzi huo wa Mkapa wa kuondoa kura tatu mtu mmoja, ndio ulisababisha yote haya. Ni hatua hiyo iliyomuibua Joseph Butiku, mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere hadi kuandikia barua kwa Mkapa akimtuhumu kujenga misingi mibaya kwa chama chake.

Malalamiko ya kukiuka utaratibu wa siku zote tena wakati wa “lala salama,” yanmaendelea kulalamikiwa kuwa yalilenga kubeba mtu badala ya demokrasia.

Wapo wanaosema kwamba Mkapa alikuwa sahihi kutenda alichotenda kutokana na mazingira yalivyokuwepo. Kuna taarifa kwamba Mkapa alichukua uamuzi huo ili kukiokoa chama chake na tishio la kumeguka.

Maneno ya hapa na pale yalifika mbali zaidi hata kudhani kuwa endapo mgombea fulani asingepitishwa, kulikuwa na mpango wa kujiengua na kujiunga na moja ya vyama vya upinzani vilivyokuwepo.

Mbali na hayo, hadi sasa, hapajakuwepo jitihada zozote zilizolenga kurekebisha mapungufu yaliyotokea wakati wa uchaguzi kama vile matumizi yasiyo sahihi ya fedha. Hiki kinachovaliwa njuga sasa na watawala, kimelenga kuengua tu baadhi ya watu.

Pamoja na kwamba Mkapa alikiri kuwapo kwa viongozi wabinafsi (kikao cha halmashauri ya CCM – NEC, 5 Septemba 2004), lakini ni uongozi wake ulioongeza mamlaka ya rais kuteua watu kumi kuwa wabunge katika bunge la Jamhuri na hata kuwapa uwaziri.

Hakusikiliza kilio cha wananchi wala hakujikumbusha hotuba yake ya awali. Matokeo yake, nafasi 10 zilizotengwa na katiba zimeanza kutolewa kama zawadi.

Swali la msingi hata hivyo ni iwapo Mkapa alikuwa akijitazama mwenyewe au alikuwa akiwaangalia walio chini yake?

Mwaka 2005 wakati anamalizia kipindi chake cha uongozi, Mkapa mbali na kugusia baadhi ya mapungufu ya uongozi wake, hakufanya jitihada za kutosha kukijenga chama chake na kuwa taasisi inayoweza kijisimamia.

Mgogoro mkubwa ulionekana mwaka 2005 pale ilipojengeka imani kwamba “ukichaguliwa kuwa rais wa nchi, basi wewe na marafiki zako mtakuwa mmeula.”

Katika imani na mazingira haya, chama na serikali vinaweza kugeuka mara moja na kuwa magenge ya walanguzi.

Hakuna mashaka kuwa mara baada ya kuchaguliwa kuongoza nchi, Novemba mwaka 1995, Mkapa alifanya jitihada kubwa za kuitambulisha serikali yake kama isiyovumilia rushwa.

Yeye mwenyewe alitangaza mali zake hadharani kama mfano wa kiongozi anayechukia rushwa.

Dalili mbaya ya mambo ilianza pale serikali ya Mkapa na hata Mkapa mwenyewe aliposhambulia Tume ya Jaji Robert Kisanga iliyokusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba.

Kama hiyo haitoshi, mwaka 2000 serikali ya CCM ilipeleka muswada wa marekebisho ya katiba kuruhusu mshindi wa urais atangazwe hata kama atapata chini ya asilimia 50 ya kura.

Kipengele hicho kinakwenda kinyume na kanuni ya CCM inayotaka mshindi apatikane kwa zaidi ya asilimia 50.

Kama tunataka kurejesha taifa letu katika mstari ni vema turejee kauli ya Mwalimu Nyerere aliyoitoa mwaka 1995 kwenye sherehe za Mei Mosi mkoani Mbeya.

Mwalimu alisema, “Wanaotaka kutuongoza wanaweza, kwanza kueleza tulikuwa wapi, tuko wapi na tunataka kwenda wapi?”

Tuseme basi, tena bila kutafuna maneno, na tuulize je, hawa wanaotaka uongozi leo wanaweza kutupeleka kule tunakotaka? Wanaweza kutushirikisha ili na sisi tusaidie kufika huko tunakotaka kwenda?

Je, huyu anayetaka uongozi, tayari amepata majibu ya kwanini karibu nusu karne imepita, lakini bado wananchi wake ni masikini. Tutafakari.

Mwandishi anapatikana kwa simu: 0784 219535 au barua pepe: a_bomani@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: