'Tumepoteza misingi, tutaangamia'


David Majebelle's picture

Na David Majebelle - Imechapwa 17 June 2008

Printer-friendly version

TANZANIA ni nchi iliyojengwa vizuri na waasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abed Amani Karume kwa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Uongozi wa Rais Alli Hassan Mwinyi uliamua kuacha siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Binafsi sina shida ya kuacha ujamaa; lakini kujitegemea ni lazima.

Hata zile nchi kubwa kama Marekani, Urusi, China na nchi za Ulaya, pamoja na kuwa na mfumo wa kibepari, zimeng'ang'ania kujitegemea.

Nchi hizo pia zinaendeshwa kwa maadili kama kutochanganya utumishi wa umma na siasa, na mtu akipatikana na hatia ya ufisadi au rushwa anashughulikiwa mara moja na vyombo vya dola vinavyohusika.

Hata nchi tunazoshangilia za Mashariki ya Mbali kama Singapore, Malaysia, Taiwan na Korea ya Kusini zilikuwa na maendeleo sawa Tanzania miaka 41 iliyopita; lakini zilipanga mambo yao vizuri na kutekeleza siasa ya kujitegemea.

Chukua mfano wa Korea. Taifa lilihakikisha kwamba kile kilichoitwa "The Family Silver Ware," yaani mali muhimu za taifa za nchi kama nishati, maji, madini, miundombinu na mabenki havibinafsishwi ovyoovyo kwa mikataba mibovu ambayo haisaidii nchi.

Hata kama vilibinafsishwa, basi serikali ilikuwemo kwa kiasi kikubwa kuhakikisha sera na dira ya nchi zao inaendelea kama ilivyopangwa.

Nchi hizi zilijipangia dira na malengo ya muda mfupi, wa kati na mrefu, kuhakikisha zinapeleka vijana wake kupata elimu popote pale duniani.

Vijana hao waliporejea wakawa wahandisi, madaktari, wakunga, walimu wa kila aina na serikali zikajitosheleza kwa mahitaji ya wataalamu.

Sisi hapa "Bongo" ni tofauti kabisa. Kwanza serikali ilikuwa ikizuia watu kutoka na kutafuta maisha nje ya nchi. Ilikuwa baada ya vita dhidi ya Iddi Amin, baadhi ya wataalamu kama madaktari, waalimuna wahandisi walianza kuhama nchi.

Angalia Watanzania waliohamia Kenya, Uganda, Botswana, Zimbabwe, Msumbiji, Lesotho, Swaziland, Zambia, Namibia, Afrika Kusini na hata Ulaya na Marekani ili kutafuta maslahi bora.

Hebu tuangalie ujio wa Balozi Andrew Young na wajumbe wa Mkutano wa Nane wa Leon Sullivan. Andrew Young ameshauriwa Tanzania ifungue milango kwa wawekezaji zaidi kuliko ilivyofunguliwa sasa.

Katika hili, mimi sikubaliani naye kabisa. Hatuwezi kufungua milango holela. Tangu serikali imefanya hivyo nchi yetu imetapeliwa na wanaojiita wawekezaji kwa sababu serikali haikuwachunguza.

Mfano mzuri ni pale jengo la Millennium Hotel la Akiba ya Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa lililoko Kijitonyama, Dar es Salaam.

Aliyekuwa anamiliki hoteli hiyo ameondoka na mabilioni ya shilingi. Alidai kuwa mwekezaji mwenye hoteli hata Afrika Kusini. Akakopeshwa mabilioni ya shilingi hapa nchini.

Alipanga, akaendesha hoteli, akakusanya fedha; hakulipa kodi kwa vile alikuwa amesamehewa; akateleza na mabilioni yote ya Watanzania. Huwezi kumpata sasa.

Watu wa aina hii wanastahili kubanwa ili waweke kiasi fulani cha fedha kama dhamana kabla ya kukubaliwa kuanza miradi.

Watanzania wangefurahi kama Andrew Young angejadili jinsi ya kusaidia Tanzania kupata angalau asilimia 30 ya mrabaha wa dhahabu yake kutoka migodi ya kampuni ya Barrick ambako inasadikika ana maslahi, badala ya asilimia tatu inazopata sasa.

Au angetoa ushauri juu ya umiliki. Kwa mfano serikali ya Botswana ina hisa asilimia 50 katika migodi yote. Wawekezaji nao wana asilimia 50.

Serikali ya Botswana na kampuni yake ya Desbswana inachukua mrahaba wa asilimia 30 huku almasi zote zinakatwa na kuchongwa, kupimwa uzito na thamani yake kabla ya kupelekwa Johannesburg, London, Antwerp, Moscow, New York, Bangkok, Tokyo na miji mingine.

Leo mtu yoyote mstarabu angefikiria Bwana mkubwa huyu angejitahidi kuwasaidia Watanzania wapate 30% ya mrahaba (Royalties) wa dhahabu yao kutoka migodi hiyo badala ya 3% Tanzania inayopata sasa ukizingatia kwamba bei ya dhahabu sasa ni kubwa.

Ilitarajiwa Mkutano wa Sullivan ungeifumbua macho Tanzania. Tanzania ingekuwa wapi kama tungefanya kama Botswana kwa kuwa na mikataba bora ya almasi, dhahabu, makaa ya mawe, tanzanite, ulanga na madini mengine yaliyogunduliwa huko kanda ya ziwa, Mbeya, Ruvuma na Morogoro?

Kama kusingekuwa na ufisadi na rushwa ya kutisha kama ilivyo sasa, si tungekuwa mbali sana kimaendeleo?

Tanzania inaweza kufanya vema kama kutakuwa na utashi wa kisiasa, mipango mizuri ya sasa ya muda mfupi, wa kati na muda mefu na kuondoa maisha ya anasa ya kulifilisi taifa kwa ulafi.

Kubinafsisha peke yake siyo muarobaini wa uchumi bora. Angalia Ufaransa inavyokatalia hata nchi jirani kuwekeza katika maeneo kama vile reli, utengenezaji wa nishati za nuklia na utengenezaji wa ndege za vita na abiria. Hawataki.

Wajerumani vivyo hivyo. Reli, ndege na miundombinu mingine, wanasisistiza wafanye wenyewe. Urusi ndio kabisa! Angalia wanavyopeleka puta wazungu wanaotaka kuwekeza katika nishati ya gesi na mafuta.

Kwingine kote watu wako makini. Sisi "Bongo" mtu akitudengulia vijisenti hewani tu, waheshimiwa wanakurupuka kwenda kusaini mikataba isiyo na kichwa wala miguu, bila kwanza kukaa chini na kufikiri Tanzania itafaidikaje; vizazi vijavyo vitafaidikaje, wajukuu zetu watafaidikaje.

Tanzania imejaa mikataba ya "nailoni" inayosainiwa usiku na mingine isiyo na mafao kwa wananchi kama ile ya Reli, Maji, Bandari, ATC, IPTL, Richmond, Dowans Agreco na mingine mingi ambayo haijawasaidia wananchi.

Ni mikataba hii ambayo inazidi kufanya maisha ya wananchi kuwa magumu zaidi kila siku. Andrew Young na wenzake wa Sullivan wangefanya vizuri kushauri Rais Kikwete kuondoa kasoro hizi.

0
No votes yet