Tumeshindwa kila mahali


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 14 April 2009

Printer-friendly version

MENGI yamesemwa baada ya treni ya abiria kugongana na treni ya mizigo kati ya Stesheni ya Gulwe na Igandu, Dodoma wiki mbili zilizopita.

Kuna wanaolaumu serikali na wengine muwekezaji – Kampuni ya Reli (TRL) kutoka nchini India. Lakini ukiangalia kwa makini kilichotokea, ukichanganya na hali ya shirika lilivyo kwa hivi sasa, utabaini mambo kadhaa.

Tangu serikali ikabidhi kazi za TRC kwa kampuni hiyo, hakuna kilichofanyika. Ukodishwaji umeidhalilisha serikali, taifa na umeleta machungu kwa wananchi, hasa wenye kipato cha chini wanaotegemea usafiri huo.

Si hivyo tu, ukodishwaji umewakatisha tamaa hata wafadhili.

Hii ni kwa sababu kulikuwa na wakodishaji wenye uwezo mkubwa wa kuendesha shirika hili kutoka Canada, Ujerumani na Afrika ya Kusini ambao waliomba zabuni lakini wakanyimwa.

Badala yake serikali imekabidhi shirika kwa muwekezaji ambaye hana sifa, wala uwezo wa kuliendesha. Mara kadhaa serikali imelazimika kuchota fedha za umma kumpa muekezaji huyo ili kuweza kulipa mishahara watumishi wake.

Baadhi ya wanaosafiri na treni ya TRL wanasema uwekezaji haukuiboresha bali umeiharibu kuliko ilivyokuwa kabla yake.

Kwa kuangalia kinachoendelea ndani ya shirika na kilichotokea kabla ya ukodishwaji kufanyika, utabaini mara moja kuwa chanzo cha ajali iliyotokea ni serikali kushindwa kusimamia shirika lake.

Kuna wanaosema iwapo mchakato wa ukodishaji wa TRC utawekwa wazi, basi kuna uwezekano mkubwa wa vigogo kuumbuka kutokana na jinsi zoezi zima lilivyogubikwa na harufu ya ufisadi.

Na hili la serikali kushindwa kuimarisha mfumo wa reli, kushindwa kumsimamia anayejiita mwekezaji, limetokea miaka 48 baada ya uhuru na mwaka mmoja na miezi mine, tangu mwekezaji akabidhiwe shirika.

Lengo la ukodishaji lilikuwa kuboresha huduma za usafiri, kupunguza ajali na kuleta hali bora kwa watumishi.

Kutokana na hali hiyo, serikali imedhihirisha kuwa haijali na haiku tayari kutunza kile ilichokirithi kutoka kwa wakoloni.

Wakoloni waliachia taifa hili mfumo madhubuti wa reli Tabora-Kigoma; Tabora hadi Mwanza;Msagali hadi Kongwa; Tanga hadi Arusha; na Mtwara hadi Nachingwea.  

Kulikuwa na reli imara ya Kaliua hadi Mpanda, Manyoni hadi Singida-Kitangiri na Ruvu hadi Korogwe.

Hata hivyo, mara baada ya uhuru serikali iling’oa Reli ya Kusini na baadaye reli ya Manyoni-Singida na Msagali-Kongwa, ikafuata njia. Reli ya Kaliua-Mpanda ilinusurika kwa sababu ya migodi ya dhahabu iliyokuwapo katika maeneo hayo.

Kilichosikitisha baadhi ya wananchi ni hatua ya serikali kung’oa Reli ya Kusini; uamuzi ambao kila mmoja aliuona kuwa si sahihi.

Bahati njema tayari serikali imekiri hilo; imetangaza kuwa itajenga upya reli hiyo kwa kuanzia Mtwara na kuiendeleza hadi pwani ya mashariki ya Ziwa Nyassa.

Ujenzi huo utafanywa chini ya mradi wa Uendelezaji wa Upito wa Mtwara (Mtwara Development Corridor). Tayari serikali imejenga reli ya Manyoni-Singida ambayo iliing’oa miaka 25 iliyopita.

Hakuna ubishi kwamba ajali hiyo iliyotokana na treni ya mizigo kusimama njiani bila sababu rasmi ni matokeo ya athari hizi. Taarifa zinasema wafanyakazi wa treni ya abiria walikuwa wamesimama njiani ili kuuza mafuta; viongozi wa TRL walikuwa hawana hata taarifa ya kile kinachoendelea.

Lakini pia kuna hili la treni kuendeshwa kwa kuviziana au kubahatisha. Kwamba treni inaweza kuondoka kituoni bila kuhakikishiwa usalama wao na Mkuu wa Kituo.

Ndiyo maana treni ya abiria iliondoka stesheni ya Gulwe wakati treni ya mizigo iliyoitangulia bado haijafika kituo kinachofuata cha Igandu. Je, vipi wakuu wa TRL wanaliafiki hili? Hivyo ndivyo treni zinavyoendeshwa India?

Kuna madai pia kwamba mara baada tu ya ajali kutokea, wakuu wa TRL hawakujali abiria walioathirika. Walifika kuangalia hasara iliyopatikana hasa miundo mbinu na mabehewa!

Treni ya abiria iliyopata ajali ilikuwa ni ile ya Express ambayo husimama vituo vikuu tu – yaani ikiondoka Dar es Salaam, husimama kwa kupakia na kupakua abiria Ruvu, Morogoro, Kilosa na Dodoma. Huduma hii ilianzishwa majuzi, na tija yake haijapatikana. 

Wananchi wengi kutoka vituo vidogo hawapati huduma ya treni, kinyume cha malengo ya kuwapo njia ya reli inayopitia maeneo yao. Matokeo yake, wananchi katika stesheni za reli ambazo treni haisimami huamua kurusha mawe na kuvunja vioo vya madirisha kwa hasira.

Haya siyo maendeleo tuliyotarajia. Ni ishara kwamba serikali ni mbovu kama mfumo huu wa reli.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: