Tuna amani Tanzania? Haiwezekani!


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 01 July 2008

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

'Tuna tatizo kubwa la ukosefu wa utawala bora nchini petu Tanzania. Kwa sababu hiyo, tunaona tatizo jingine kubwa zaidi: amani ya nchi na wananchi inatetereka.'

SEMINA elekezi zimeendeshwa si moja wala mbili. Mamilioni ya shilingi yametumika kuzigharamia. Walishiriki mawaziri, makatibu wakuu na wasaidizi wao kama wakurugenzi na makamishna.

Nyingine wakawepo wakuu wa mikoa na ma DC. Maofisa tawala wa ngazi hizi pia walijumuishwa. Mamilioni mengine yakatumika kugharamia. Si mchezo, zilifanyikia Ngurdoto, Arusha. Ni hoteli mpyampya hii.

Wapi? Wachache wanatumia mafunzo yale kubadilisha utamaduni wa namna ya kutumikia umma. Walivyo ni kama vile kisiki cha mpingo, haking?oki wala kugeuka hata uje upepo mkali kiasi gani.

Kama ilivyo kwa kisiki cha mpingo, kubaki madhubuti hivyo mpaka kikasirikiwe na buldoza, dawa pekee ya maofisa wetu hawa ni kutokea kiongozi anayejali utu na haki za watu. Lini atakuja, hakuna ajuaye.

Wafunguaji na wafungaji wa semina elekezi walihimiza utiifu kwa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma ili kuhudumia wananchi kwa ufanisi wa hali ya juu.

Ufanisi unaotajwa na viongozi watukuka ni ule unaoendana na kaulimbiu yao wenyewe ya; ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya (ANKA), kusudi wawezeshe kupatikana haki na kwa jumla, maisha bora kwa kila Mtanzania, maana, wanasema na kuamini, 'Tanzania yenye neema inawezekana!'

Maofisa wetu Tanzania hawajasikia ndio maana tunashuhudia wakibaki kama kisingi cha mpingo kinachosubiri buldoza. Tunaona wanaendeleza utamaduni uleule waliouzoea. Utamaduni wa kulinda maslahi yao binafsi kwanza badala ya wale wanaowatumikia.

Masikini maofisa watumishi wa umma hawa; kama vile hawajui kuwa wanachokifanya kina matokeo mabaya kwa jamii, kwa uchumi na kwa taifa lao. Wamechoka kukaa na kufikiri na wala hakipo cha kuwazindua ili warudi kwenye mstari. Wametopea katika uhafidhina.

Ndivyo mtu anathubutu kusema. Anasema hivi kwa sababu kila akifikiri jinsi hali inavyokwenda, haoni kama maofisa wanaweza kubadilika katika zama za karibuni. Kwamba wafikie mahali wasema imetosha, ni bahati tu itakayotokana na utashi wa aliyewaumba.

Kwa hakika Watanzania wanahitaji maofisa wao waonyeshe kwa vitendo kuwa wamejifunza kwa zile semina elekezi zilizotapanya mamilioni ya fedha za kodi. Mabadiliko yawe ya kujitambua ili watumikie umma badala ya matumbo yao.

Si wanalipwa mishahara mikubwa na marupurupu ya haja pale wanapopangiwa safari za kikazi nje ya vituo vyao vya kazi; liko wapi tatizo jamani? Wao wanasema lipo.

Hebu tuingie hapa, katika ile dhamira ya kusaidia kuibua hoja za kuwagusa maofisa hawa dhaifu, lengo likiwa moja tu: kuwasukuma wabadilike ili umma upate faida inayoendelea (faida endelevu) kutokana na utumishi wao.

Yupo Mzee Rajab Iddi Kambi, mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam. Ni mzee kweli maana ukimuona, amechoka hasa. Anaburura miguu atembeapo, kushoto kulia, kushoto kulia kama vile anajifunza kutembea.

Tatizo lake si umri kumzidia. Inaonyesha pana harufu ya ufisadi na utunishaji misuli kwa sababu ya kiburi cha madaraka na pesa. Maofisa wenye dhamana ya kuendesha shughuli za umma kwa kuzingatia haki na wajibu, wamemgeuka.

Mzee Kambi, hata kabla ya neno 'mjasiriamali' halijatoholewa na aliyekuwa Rais katika awamu ya tatu ya uongozi wa nchi, Benjamin Mkapa, alikopa benki ili kuendeleza shughuli zake za useremala.

Alikopa Sh. 5 milioni kwenye Benki ya CRDB (1996) Ltd mwaka 1999. Baadaye aliridhiana na benki hii kuongezewa kiwango cha mkopo wake iwe ni Sh. 11. 5 milioni. Maana yake aliongezewa Sh. 6.5 milioni.

Lakini, benki ilimtilia katika akaunti yake, Sh. 10 milioni (asilimia 88), hivyo kushikilia Sh. 1,500,000. Kitendo hicho kilizorotesha mradi wa Mzee Kambi kuanza na haukuanza kweli. Sivyo. Umekufa kufikia sasa.

Hoja muhimu hapa ni kuwa ushikiliaji ule wa asilimia mbili za mkopo halisi, ulifanywa na Benki kwa maamuzi ya upande mmoja tu: aliamua mkopeshaji peke yake bila ya ridhaa ya mkopaji.

Kweli, shughuli za mradi zilizorota. Mzee Kambi alitaka kununua zana za useremala ikiwemo mashine za kupasulia na kuwekea sawa mbao. Hakuzipata kwa ukamilifu wake, akakwama.

Alipohitaji fedha zilizoshikiliwa na benki, ikawa shida kuzipata. Suala hili likafika mahakamani. Mzee Kambi alishinda kesi aliyofungua kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni (Kivukoni).

Hukumu ya kesi hii ya madai namba 17/1999 iliyosikilizwa na Hakimu Nkya ilitoka 16 Novemba 2006 na kumpa haki Mzee Kambi dhidi ya Benki ya CRDB.

Hukumu iliamuru: Benki imlipe mdai Sh. 1,500,000 ambazo ilizishikilia bila ya ridhaa ya mkopaji; ilipe Sh. 2,500,000 za fidia ya kuharibika kwa zana za kazi; ilipe Sh. 6 milioni za fidia kwa hasara ambayo mdai alipata kwa kukosa kipato; ilipe Sh. 3 milioni za fidia kwa hasara iliyotokana na mdaiwa kuvunja mkataba wa ukopeshaji; na benki kuzuiwa kutoa mali mpaka masharti yaliyotajwa yatimizwe.

Benki haikuridhika na uamuzi huo. Ilikata rufani kwa ombi namba 68/2007 ikiomba uamuzi huo utenguliwe. Ilishindwa. Katika uamuzi uliotolewa 13 Desemba 2007, Jaji wa Mahakama Kuu, A.R. Mruma, alishikilia uamuzi ulioamuru Mzee Kambi alipwe yaliyoamriwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi, pamoja na gharama za rufani.

Benki haikuridhika na imekata rufani Mahakama ya Rufaa Tanzania. Muda wa kisheria wa kukata rufani ulikwisha, ikaomba nyongeza na ikatoa sababu kuwa ilichelewa kuwasilisha rufani hiyo kwa kuwa ilikuwa ni lazima iambatanishe na kumbukumbu za maamuzi ya kesi ambazo yenyewe ilicheleweshewa na Mahakama.

Wakati hayo yakitokea, kumbukumbu zinaonyesha Benki imewahi kuafikiana na Mzee Kambi katika hatua ya kutaka kumaliza mvutano wao ili alipwe haki yake. Hata hivyo, Benki imehalifu maafikiano hayo.

Moja ya kumbukumbu hizo, inasomeka kwamba inaonekana wakili ameona aendelee na hatua za kutafuta haki mahakamani. Rufani iliyokatwa kwa ajili ya kupinga uamuzi wa 13 Desemba 2007, wa Jaji Mruma, haijaamuliwa.

Mzee Kambi analalamika kuwa zipo mbinu za kukwamisha haki yake maana haoni sababu za msingi za kutopatiwa haki hiyo. Analalamika kuwa kesi hiyo imemmaliza kimaisha baada ya kupatwa ugonjwa katikati.

Ana kisa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB akimlaumu kumgeuka baada ya kukubaliana njia ya kurahisisha utaratibu wa kulipwa haki yake.

Hakuna uamuzi, haki haijalipwa kwa Mzee Kambi, ambaye anapambana kuitafuta haki kwa miaka tisa sasa. Anaumia maana maisha hayaendi kama alivyokusudia alipooomba mkopo. Alitarajia umsaidie, umemuangamiza.

Nani wa kumuokoa Mzee Kambi? Sijui, maana utawala bora ni kama vile hauwezekani Tanzania!

0
No votes yet