Tunahitaji kinga ya kuvuana uanachama


John Kibasso's picture

Na John Kibasso - Imechapwa 15 September 2009

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

KATIBA ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) fungu la (1) Ibara ya 8(2) inatoa masharti ya mwanachama kwamba awe ni mtu anayefanya "juhudi ya kuelewa, kuieleza na kuitekeleza itikadi na siasa ya CCM."

Vilevile kifungu kidogo cha (5) kinasema, "mwanachama awe ni mtu ambaye siku zote yupo mstari wa mbele katika utekelezaji wa mambo yote ya umma kulingana na miongozo ya CCM."

Hapana shaka kwa masharti hayo, hususan kifungu cha (5), kinaonyesha kwamba mwanachama yeyote wa CCM, bila kujali wadhifa wake kichama au kitaifa, ni lazima awe mstari wa mbele katika utekelezaji wa "mambo ya umma kulingana na muongozo wa chama. "

Nashawishika kuamini kwamba haikuwa dhamira ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kumsulubu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samwel Sita, kwa kukaidi mwongozo wa chama, bali ni mwenendo na utaratibu wa kawaida wa kuendesha vikao vya chama kwa mujibu wa katiba na taratibu zilizowekwa.

Nashindwa kuelewa tafsiri ya kusulubiwa na kufungwa mdomo kwa Sita inatoka wapi. Kiongozi yeyote aliyeteuliwa na chama, hatimaye kupata wadhifa wa kitaifa, bado analazimika kuheshimu, kusimamia, kulinda na kutetea katiba ya chama chake.

Sita ni mwanachama wa CCM. Ni kiongozi. Kwa mujibu wa katiba ya CCM ibara (76), Spika wa Bunge la Jamhuri ni yule wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, anayetokana na CCM, ni mjumbe wa NEC na Kamati Kuu (CC).

CCM ina haki ya kumwita mwanachama wake mwenye wadhifa wowote ule, kuhudhuria kwenye kikao kinachomhusu kikatiba.

Kilichotokea NEC-CCM ni kwamba, Sitta alihudhuria kwenye kikao kinachomhusu, siyo kwa nia ya kufungwa mdomo au kusulubiwa, hapana. Ni kujadili mustakabali wa CCM.

Kikao cha NEC kina uwezo na madaraka ya kumwita na kutoa maelekezo kwa mwanachama wake bila kuingiliwa na mtu, ili mradi asiingilie uhuru wa kutoa mawazo.

Kwa muono wangu, udhaifu na upungufu uliojitokeza kwenye kikao hicho, ni ukosefu wa maadili ambapo baadhi ya wajumbe walivujisha siri ya kikao.

Kwa kadri ya uelewa wangu, vikao vya chama vyote ni vya siri. Wajumbe wa CCM walikuwa wanajadili hali ya hewa kisiasa ndani ya chama chao, na si kumjadili Sitta kama spika wa Bunge.

Maamuzi ya chama yalilenga kukosoa mwenendo wa baadhi ya wanachama usioridhisha na siyo Sitta.

Si sahihi na wala si busara kumchonganisha Sitta (Spika) na viongozi wenzake wa CCM na Bunge, kwa maana ya utaratibu na mwongozo wa kanuni za Bunge.

Uwezo wa Sitta kisheria unafahamika. Ameonyesha ujasiri na uthubutu wa kuendesha shughuli za Bunge kwa uwazi kuliko ilivyowahi kutokea. Ni lazima tumpe pongezi kwa kazi yake hii.

Bali, si kweli kwamba alifungwa mdomo au amefungwa mdomo Dodoma kama ambavyo vyombo vya habari vinaripoti. CCM kinaendelea kumheshimu na kitaendelea kumheshimu na sidhani wanaweza kufikia hatua Sitta wakamvua uanachama.

Nashawishika kuamini kwamba Watanzania wengi hivi sasa wana uelewa mkubwa wa kisiasa ndani ya nchi yao.

Haipendezi baadhi ya watu kuanza kupandikiza au kupotosha ukweli wa yaliyojiri NEC kwa kutaka kumgonganisha Sitta na viongozi wenzake wa CCM.

Ningetegemea weledi wa siasa, wanasheria, viongozi wa vyama vingine, wasomi na wananchi kwa ujumla, watoe mawazo mbadala wa nini kifanyike ili chama kinachoshika dola kisiingilie mihimili mingine katika nchi.

Kwa muono wangu, nadhani wazo mbadala ni kwa Tume ya Uchaguzi kupewa uwezo wa kisheria kwamba "mwanachama yeyote wa chama akishapata nafasi ya uongozi wa kuanzia serikali za mitaa hadi urais, basi asiondolewe katika wadhifa huo kwa kisingizio cha kumfukuza uanachama.

Kwa kufuata utaratibu huu, mbunge au diwani akihama chama chake kabla ya muda kuisha, basi aendelee kubaki kuwa mbunge.

Hii itapunguza uwezekano wa vyama vya kidikteta kufanya maamuzi ya hovyo, ya kutishia mbunge, au waziri kuvuliwa uanachama.

Kwa hali ilivyo sasa, rais, spika, waziri, mbunge au diwani, anakuwa mwoga kuendelea kusimamia kile anachokiamini iwapo chama chake hakikubaliani na msimamo wake.

Ushauri mwingine ni kutenganisha nafasi za chama na dola. Kwa mfano, mwenyekiti wa chama abaki kuwa mwenyekiti na rais abaki kuwa rais.

Mara nyingi unajitokeza utata kwenye maamuzi ya rais, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama. Mtafaruku unatokana na utekelezaji wa maagizo ya rais kwa kigezo cha itikadi ya vyama kwa kuhisi kuwa maagizo yaliyotolewa yanalenga kuhujumu vyama vingine.

Sina sababu ya kutofautiana na waliokerwa na maamuzi ya NEC, lakini tukubali kwamba mfumo huu wa uendeshaji vyama ndicho chanzo cha mtafaruku uliojitokeza.

Mapokeo ya wanachama walio wengi yanabainisha kwamba CCM iliamua, kwa makusudi, kukwepa kuwajibisha mafisadi ndani ya chama na badala yake wakaamua "kumtupia changa Sitta."

Hakika hili ni changamoto kwa jamii kutumia busara na hekima kupata suluhisho bila kuathiri miongozo ya katiba za vyama husika.

Bila kutafuta muafaka au utaratibu mbadala bado dudu hili litaendelea kutusumbua na kuchafua hali ya hewa kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Huwezi kuwa na chama cha siasa ambacho hakina masharti wala mwongozo wa maadili. Bila utaratibu, kanuni au sheria hapatakuwepo na amani.

Katiba za vyama zipo ili kusimamia miiko na maadili ya wanachama bila kingilia uhuru wa mwanachama mwingine.

Hakika, kama tutapata dawa ya kutenganisha majukumu ya viongozi wa vyama na yale ya kitaifa, hususan kufuta kipengele cha vyama kuweza kumvua uanachama au uongozi na kupoteza nafasi yake kitaifa, tutakuwa tumepiga hatua kubwa kisiasa barani Afrika.

Mwingiliano huu unaweza kupatiwa ufumbuzi pale wanasiasa watakapokubali kuweka itikadi ya vyama vyao pembeni na kusimamia mambo ya kitaifa, bila kujali vyama vyao.

Makala hii imeandikwa na msomaji wa MwanaHALISI na amewahi kuwa mbunge wa Temeke, Dar es Salaam, kupitia CCM. Anapatikana kwa Simu: 0713 399004
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: