Tunahitaji upendo kuliko vingine vyote


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 23 February 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

WAKATI wananchi wa Gongolamboto, Majohe, Pugu, Kisarawe na Tabata wakiteswa, kuuawa na kuchanganywa na mabomu; baadhi ya Watanzania walikuwa wanajitahidi ‘kufaidika’ na hali hiyo.

Zipo taarifa zisizo rasmi kuwa wapo wasichana na akina mama waliobakwa baada ya kukimbia makazi yao na kuangukia katika mikono ya waovu.

Nilisoma gazeti la Mwananchi siku mbili baada ya tukio hilo na niliona habari moja ya kusikitisha. Kwamba mwanamume mmoja ambaye umri wake unakadiriwa kuwa kati ya miaka 35 hadi 40, alikuwa akimtongoza binti wa miaka 17 aliyekuwa amekimbia milipuko ili akalale naye.

Binti huyo alikuwa amembeba mdogo wake na wakati huo, majira ya saa saba usiku, alikuwa hana nauli na amekwama katika eneo ambalo mwanamume huyo alikuwa akimwomba waende kwenye nyumba ya kulala wageni.

Kuna matukio pia ya watu ambao baada ya kuacha nyumba zao wazi wakikimbia milipuko, watu wengine walivamia nyumba hizo na kupora kila walichoweza.

Nakumbuka tukio moja lililotokea mwaka jana mkoani Tanga ambapo kundi la watalii kutoka Uholanzi lilinusurika katika ajali ya ndege lakini kwa mshangao wao, badala ya wananchi kusaidia kuwaokoa, waliishia kwenda kuiba mali za wageni hao.

Miaka 30 au pengine hata 20 iliyopita, matukio kama haya yalikuwa hayatokei hapa nchini. Watanzania walikuwa watu wema, wema sana. Ni wazi kuwa kuna mambo yanabadilika na mbaya zaidi ni kuwa yanabadilika kwenda kubaya.

Wiki iliyopita, wananchi wa mji wa Peshawar nchini Pakistan waliwaua wezi waliowakamata na kuwachoma moto. Baada ya kusikia hivyo, makundi mbalimbali ya jamii yameanza kuitisha mjadala wa kitaifa kuhusu hatua hiyo.

Wao wanaamini kuwa inapofikia hatua ya wananchi kujichukulia sheria mkononi, hiyo ni hali ya hatari. Nilipomaliza kusoma habari hiyo nilifumba macho na kuwaza – nadhani inawezekana imefika miaka kumi tangu Watanzania waanze kuchoma moto wezi.

Hakuna anayeshtuka. Wala hakuna anayeonyesha kushangazwa na mwelekeo huu wa Tanzania mpya. Tuko karibu miaka mitano au sita mbele ya Pakistan nab ado hatujachukua hatua yoyote.

Wakati nilipokuwa nikifikiri kuhusu hili, nilijitahidi kusoma mambo mawili matatu kuhusu wanadamu. Jambo moja la msingi nililojifunza wiki hii ni kuwa kuna tofauti moja kubwa kati ya binadamu wa awali na binadamu wa sasa kisaikolojia.

Binadamu wa zama za kale alikuwa na adui mmoja mkubwa – mazingira yake. Hakujua jinsi ya kupambana na joto wala baridi. Hakujua jinsi ya kupambana na jua wala mvua. Mafuriko na vimbunga. Binadamu mwenzake hakuwahi kuwa adui.

Baada ya maendeleo ya kiteknolojia na kiuchumi, adui namba moja wa binadamu katika kizazi tunachoishi sasa amekuwa ni binadamu mwenzake. Na hapa ndipo ilipo changamoto kubwa.

Mwanadamu sasa ameweza kudhibiti na kuyatumia mazingira yanayomzunguka. Tatizo ni kuwa, kila mwanadamu anataka kutumia vizuri mazingira na fursa zilizopo kuliko mwingine. Na hapa ndipo matatizo yanapoanza.

Wale wenye uwezo wa kutumia mazingira na kujinufaisha wanataka zaidi na kuacha watu wengi zaidi nje ya mfumo wa kunufaika. Wale wanaoachwa nje wanafanya kila jitihada ili nao wanufaike. Na hapa ndipo inawezekana tulipo.

Ukiangalia orodha ya nchi zenye vitendo vingi zaidi vya uhalifu duniani, utaona majina ya nchi kama vile Marekani, Uingereza, Ujerumani, Afrika Kusini, Russia na Japan. Hii ni kwa sababu nchi hizi zina matajiri wa kutupwa na masikini wa kutupwa.

Nchi kama Cuba ambako hali ya kiuchumi ya watu walau inalingana, unakuta vitendo vya kihalifu ni vichache sana. Kama kilichotokea Gongolamboto juzi kingetokea Havana, Moncada au Matanzas nchini Cuba, huenda watoto na akinamama hao wasingekutwa na masaibu yaliyowakuta.

Nikitaka urahisi, naweza kusema kuwa taifa letu sasa limefika hatua ya kuhitaji kufanya mjadala kufahamu chanzo cha kufikia hatua hii. Hili ni rahisi kulisema kuliko kulitenda kwa sababu najua watu watasema kuna shida nyingi sana za kuzifanyia mijadala kuliko hili.

Kwa mfano, wapo watakaosema kwamba mjadala unaotakiwa sasa ni ule wa kuwa na Katiba mpya. Na ninafahamu kuwa wananchi wanahitaji Katiba mpya. Hata hivyo, sioni kama Katiba mpya inaweza kuondoa hali hii inayozidi kujenga mizizi sasa.

Kama nilivyoeleza awali, nchi zote zinazoongoza kwa maendeleo duniani zina vitendo vya ukatili vya hali ya juu. Nchi zote hizo zina Katiba ambazo wakati sisi tunapotaka kutengeneza yetu mpya, tunafikiria kuiga machache kutoka kwao.

Naunga mkono ujio wa Katiba mpya lakini nafikiri inabidi itafutwe namna ya kurejesha ule upendo na uungwana ambao katika miaka ya nyuma ulitupa sifa kubwa sana Watanzania.

Kama Katiba mpya itasaidia kuondoa ukatili na unyanyasaji unaofanyika miongoni mwa Watanzania; katika sehemu za kazi, majumbani, mitaani na kwingineko, hilo litakuwa jambo la heri.

Kama ningeulizwa leo nataka nini kati ya Katiba mpya na UPENDO miongoni mwa Watanzania, ningechagua la pili. Mimi ni mkristo na nakumbuka niliwahi kuambiwa na mwalimu wangu wa dini siku zote kuwa amri kuu kuliko zote ni UPENDO.

Bila ya UPENDO miongoni mwa Watanzania, taifa hili halitakwenda popote. Tutabaki tu kuwa nchi ya manyang’au.

Natoa pole kwa waathirika wa mabomu ya Gongolamboto.

0718 81 48 75
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: