Tunajifunza nini kutoka Angola?


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 20 January 2010

Printer-friendly version
Michezo

MACHO na masikio ya Watanzania, hasa wapenda michezo kwa sasa yameelekezwa katika uhondo wa michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika inayoendelea huko Angola.

Ni dhahiri kwamba Watanzania wangependa Taifa Stars, timu ya taifa ya Tanzania iwe miongoni mwa mataifa 16 yanayopigana kiume huko Kusini mwa Afrika.

Lakini, katika kile tunachokiita bahati mbaya, tumekosa makali ya kwenda huko, hivyo kutimiza miaka 30 tangu tuliposhiriki kwa mara ya kwanza na ya mwisho mwaka 1980 nchini Nigeria.

Na tuache kujikumbusha maumivu haya, bali tukae chini na kujiuliza, tumejikwaa wapi? Mara kadhaa, timu yetu ya taifa inaposhindwa kutimiza lengo, huwa tunakuja na sababu za kila aina, ili mradi tu kuhalalisha kuvurunda.

Lakini ukiangalia sababu nyingi na ukweli halisi wa mambo ulivyo, utagundua huwa tunadanganyana, bali ukweli ni kwamba hatuna MIPANGO ENDELEVU NA MALENGO.

Kwa mfano, mara baada ya kocha Mbrazil Marcio Maximo kutua nchini, alidai Tanzania itawachukua muda kuwika kimataifa kutokana na kutokuwa na nyota wanaocheza soka ya kulipwa Ulaya.

Kuna ukweli katika hili, ingawa kwa upande mwingine si hoja ya msingi sana. Kwa kuangalia michuano inayoendelea Angola, tumeshuhudia nchi zisizo na makali kama Gabon na Malawi zikividuwaza vigogo kama Cameroon na Algeria.

Kama uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, hakika kikosi kama cha Ivory Coast kilichosheheni nyota kisingeweza kusimama na nchi yoyote kwa Afrika au hata katika ngazi ya klabu iwe Barcelona, Real Madrid, Chelsea, Arsenal, Manchester United au hata Liverpool.

Ivory Coast imesheheni kwelikweli, lakini mbona kwa Burkina Faso iligwaya kwa sare? Cha msingi ni mipango ya vyama na mashirikisho ya soka katika kuwa na mikakati endelevu ambayo kimsingi inakwenda sambamba na uwezo kifedha.

Hebu jiulize, kama leo hii wadhamini wakuu wa Taifa Stars kama Benki ya NMB na Serengeti Breweries wakiamua kujiweka kando, TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) itakuwa na jeuri gani?

Haina chanzo cha mapato cha uhakika, itawezaje kuendeleza mpira au kushindana na nchi kama Ivory Coast ambayo thamani ya kucha ya nyota wake mmoja tu, Didier Drogba ni zaidi ya bajeti ya TFF?

Sababu nyingine inayojaribu kuenezwa ni juu ya maumbile, tunaziona timu kama Zambia kule Angola. Wengi ni ‘vibushuti’, lakini soka inaonekana. Ufupi nao unaweza kutajwa kuwa sababu?

Nani anasema Pele wa Brazil, Gianfranco Zola wa Italia, Diego Maradona wa Argentina au Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ walikuwa warefu? Hata golini, Juma Kaseja ana tofauti gani na Omar Mahadhi bin Jabir? Lakini hawa walikuwa mahiri mno, licha ya ufupi wao.

Sasa hivi Tanzania tunatafuta kocha wa kumrithi Maximo, lakini vigezo vinavyotolewa vinawaweka kando kwa kiasi kikubwa makocha wazalendo ambao bila shaka kama wakipewa nafasi, wakaaminiwa katika kufanya maamuzi na kupewa ushirikiano kutoka serikalini, kwa wadhamini na wadau kwa ujaumla, hakuna kitakachoshindikana.

Malawi tunayoizungumza leo hii, ina kocha mzalendo, Kinnah Phiri na hata wasaidizi wake ni wazalendo, akiwamo Jack Chamangwana asiyeonekana makapi katika klabu ya hapa kwetu, Yanga.

Nionavyo mimi, kocha ni sawa na dereva. Dereva akiwa ndani ya Benz, atapendeza na kuonekana wa maana, tofauti na akiwa kwenye gari bovu ambaye naye ukimtoa kwenye gari bovu ukampa Benz, naye anapendeza. Ni sawa na timu, kocha akiwa mzuri ataonekana tu, cha msingi ni mipangilio na ushirikiano.

Kuna suala la ukomavu na uzoefu wa michuano ya kimataifa. Malawi kwa mfano, ina wachezaji wawili wa chini ya umri wa miaka 20, na wanachezeshwa katika kikosi cha Kinnah Phiri.

Hawa ni Nyirenda Harry ambaye Agosti 25 mwaka huu atatimiza miaka 20 na anacheza soka kwao Malawi. Yumo pia Nyondo Atusaye wa Carrrara Kicks ya Afrika Kusini. Huyu atatimiza miaka 20 Novemba 15 mwaka huu.

Kimsingi, kama hawa wanakomazwa mapema, ina maana wana jeuri ya kuifanyia nchi yao mapinduzi makubwa ya soka katika miaka michache ijayo, kwani wanapata uzoefu wa mapema, ndiyo maana katika umri walionao, wana uwezo wa kuwatoa kamasi timu kama Algeria yenye nyota waliotapakaa katika ligi kubwa za Ulaya kuanzia England, Ujerumani, Ureno, Italia, Ufaransa na hata Uskochi.

Kinyume cha uamuzi wa makocha kama Kinnah Phiri, hapa kwetu wachezaji chipukizi ni kwa ajili ya kucheza na watoto wenzao tu, basi.

Hebu angalia michuano ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 kutoka timu za Ligi Kuu ilivyoendeshwa kihuni. TFF, bila kuona mbali, iliendesha michuano huku makocha wa timu za taifa kutoka Brazil wakiwa Kenya kwa michuano ya Chalenji.

Ni ukweli usiofichika kwamba, vipaji vingi, tena mno vilionekana kiasi cha kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki waliojitokeza kuishuhudia pale Uwanja wa Karume, Ilala. Lakini haitashangaza kuona, hiyo ‘imeshatoka, ikirudi pacha’.

Kwa staili hii, ni wapi tutawapata warithi wa akina Shadrack Nsajigwa ambao ni dhahiri umri unawatupa? Ilipaswa hawa wa chini ya miaka 20 au wadogo zao kama wa Kombe la Coca Cola, ambao michuano ikishapita hakuna anayejua tena taarifa zao.

Hawa ndio wanaopaswa kupewa nafasi hasa kwa kipindi hiki ambacho hatuna michuano ya maana, kwani hata wakipangwa na akina Drogba au Davidi Beckham, kamwe hawataogopa kuumia kama mastaa hao watakavyokuwa wanacheza kwa tahadhari, na zaidi watataka kujitangaza kimataifa kama ilivyoonekana kwa vijana wa Taifa Stars mbele ya ivory Coast hivi karibuni.

Ili tuweze kutimiza kweli ndoto za Watanzania, ni budi TFF, makocha na wadau wakaungana na kuwa na malengo ya kweli ya kuivusha Tanzania kisoka, vinginevyo fedha na nguvu kubwa za wafadhili zitaishia kupotea. Na tuzidi kujifunza kutoka katika michuano inayoendelea Angola.

0
No votes yet