Tunamdanganya nani?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
RAIS Jakaya Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete hakuisoma Sheria ya Gharama za Uchaguzi aliyosaini kwa mbwembe 17 Machi 2010?

Kama aliisoma, hakuilewa. Kama aliilewa, basi alikuwa anafanya mzaha.

Sheria ya Gharama za Uchaguzi inaweka ukomo wa kiasi cha fedha kinachotakiwa kutumiwa na chama cha siasa kinachoshiriki uchaguzi, pamoja na wagombea wake.

Kila chama kimeruhusiwa kutumia si zaidi ya Sh. 15 bilioni kwa ajili ya kujitangaza.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini sheria hiyo mbele ya majaji, wabunge, viongozi wa serikali, vyama vya siasa na mabalozi, Kikwete alisema, “Nitasimamia sheria hii kwa vitendo.”

Lakini miezi saba baada ya kauli hiyo, angalia mabango yake yaliyotapakaa kila kona ya nchi. Angalia fulana, kanga, vitenge, kapelo na skafu zenye picha yake.

Angalia vipindi maalum vya kampeni vinavyorushwa katika redio, televisheni na magazeti. Je, hicho kinachoitwa, “Sheria ya Gharama za Uchaguzi,” kina maana gani?

Tayari baadhi ya wananchi wanajiuliza, kwa nini rais anatumia mabilioni yote haya kujitangaza?

Nani asiyemjua? Mbona amekuwepo madarakani kwa miaka mitano sasa akiwa rais na zaidi ya miaka 30 kama mbunge na waziri? Woga wote huu unatoka wapi?

Nani anayemtisha rais wetu? Kwa sababu gani? Au ni kweli kwamba matangazo haya yanayofananishwa na yale ya makampuni ya simu, yamesababishwa na yeye kushindwa kutimiza matarajio ya wananchi?

Baadhi ya mabango hasa yale yaliyopo jijini Dar es Salaam, yana ujumbe unaojirudia.

Kwa mfano, bango lililopo barabara ya Morogoro na lile la barabara ya Kawawa yote yana ujumbe unaofanana.

Mengine yana ujumbe unaokejeli hata wale ambao wamelengwa. Mfano hai, ni bango lililopo karibu na kituo cha basi cha Mkwajuni, Kinondoni, Dar es Salaam, linalomuonyesha Kikwete akimsikiliza mmoja wa wazee wa makamo kwa utulivu.

Ni ujumbe unaolenga kumuonyesha Kikwete kuwa ni msikivu na serikali yake inathamini wazee.

Lakini nani asiyejua kuwa ni serikali hii iliyoshindwa kulipa madai ya wazee wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki?

Badala ya kulipa mafao ya wastaafu, serikali ilitumia polisi kuwapiga, kuwafukuza na ilitumia mbwa na maji ya washawasha.

Baadhi ya waliofukuzwa, ni mabalozi wa mashina wa CCM. Wengine ni viongozi wa matawi na kata za chama hicho.

Wakati wazee hawa wananyanyaswa Kikwete na serikali yake imeshindwa kueleza ilikopeleka mabilioni ya shilingi yaliyotolewa na serikali ya Uingereza kulipia mafao ya waastafu hao.

Waastafu wanajua kuwa wamefika hapo walipo ni kwa sababu, serikali yao si sikivu. Haijali wananchi na haisikilizi kilio chao.

Ukiacha mabango kuna kingine pia. Mradi unaoitwa, “Jiunge na Mtandao wa CCM,” nao umetafuna mabilioni ya shilingi.

Ndani ya mradi wa mtandao wa simu, kuna mabilioni ya zawadi ambayo CCM imeahidi kulipa.

Miongoni mwao ni fedha taslimu Sh. 50 milioni, baiskeli 200 na pikipiki 64. Kuna zawadi nyingine nyingi zikiwamo kubwa na ndogo.

Wakati Kikwete na chama chake wakitafuna mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kujitangaza, baadhi ya wananchi hasa wa vijijini, wanalalamikia ukosefu wa huduma za msingi za afya.

Zahanati hazina dawa, hospitali hazina wataalam, vituo vya afya havina wauguzi, vingine havina hata vyoo na viko katika mazingira yanayokatisha tamaa ya maisha ya mgonjwa.

Hayo ni machache. Kuna mengine pia. Kwa mfano, wakati Kikwete anatumia mabilioni ya shilingi kutaka kurejea madarakani kwa kishindo, maelfu ya watoto wanakufa kila uchao kutokana na ukosefu wa lishe bora.

Wananchi wanajiuliza, hizi fedha zinazotapanywa kama vile nchi imepata “laana,” kwa nini zisitumike kutatua matatizo yao? Kwa nini zisiwekezwe katika ujenzi wa shule, uboreshaji wa huduma za afya, ujenzi wa miundombinu, maji na mawasiliano?

Ukiangalia yote haya, haraka unabaini kuwa Kikwete hakusaini sheria ya gharama za uchaguzi kwa nia ya kudhibiti fedha chafu kutumika kuingiza kiongozi madarakani. Bali alichokinya ni aina nyingine ya usanii. Alilenga kufurahisha wahisani. Basi!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: