Tunamsubiri Pinda siyo vikao butu


editor's picture

Na editor - Imechapwa 17 June 2008

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KUTOKA kaulimbiu ya ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya, hadi vikao visivyo na ajenda mahsusi. Hii ndiyo picha inayojengeka haraka tunapotafakari mwenendo wa utendaji kazi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Taarifa kwamba kikao cha wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho kilichofanyika Jumapili mjini Dodoma, hakikuwa na ajenda, ni za kusikitisha.

Zinasikitisha zaidi kwa sababu kilikuja kuonekana kama kilichoandaliwa maalum kwa lengo la kusafisha majina ya baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa ufisadi.

Ni kweli watuhumiwa wana haki ya kujitetea ndani ya chama chao; vilevile katika kushawishi watu wa kuwasemea; kama ilivyokuwa kwenye kikao hicho.

Lakini kwamba hakukuwa na ajenda kikaoni; kwamba kila mwenye lake aseme, ilikuwa shabaha ya kutoa nafasi kwa watuhumiwa kupumua na kujiona wamerudi kundini hata kabla serikali kuwachukulia hatua.

Hii ndiyo maana kikao kiliishia kwenye mgawanyiko. Watuhumiwa na wanaowaunga mkono, na wabunge na viongozi wa NEC wenye msimamo wa kuona watuhumiwa wanachukuliwa hatua.

Kwa njia nyingine, kikao cha aina hii kinaweza kuonekana kuwa kilikuwa cha kumtishia Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye anapaswa kutoa maamuzi ya msingi juu ya watuhumiwa, tena mwezi huu.

Tunaona dhahiri kulikuwa na mkakati uliojengwa mapema ili kurudisha watuhumiwa katika nafasi ya kujisikia kama wasiokuwa na doa lolote mbele ya umma wa Watanzania, ingawa wengine tayari wamejiuzulu nyadhifa zao.

Nani anaweza kukana kwamba huo haukuwa mkakati wa mwendelezo wa utamaduni wa serikali ya CCM wa kufinyangafinyanga mambo, ili itakapofika siku ya mwisho, kusipatikane wa kujibu tuhuma za ufisadi zilizoko mezani.

Hapa ndipo tunaungana na wajumbe wa kikao hicho ambao wanalalamikia uitishaji kikao hicho. Na kwanini iwe sasa, katika kipindi ambacho Rais na Mwenyekiti wa CCM anajua fika umma unasubiri, kwa shauku, kusikia serikali inasema nini kwa Bunge kuhusu masuala mawili muhimu.

Haya ni pamoja na utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti ya Kamati ya Dk. Mwakyembe kuhusiana na ugunduzi wa yaliyozingira mkataba wa uzalishaji umeme wa dharura uliosainiwa na serikali na kampuni ya Richmond Development Corporation.

Jingine ni ripoti ya Timu ya Rais ya kufuatilia wahusika wa wizi wa zaidi ya Sh. 133 bilioni katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), iliyoko ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Hili la utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti ya uchunguzi wa mkataba wa Richmond, halina muda tena maana lazima serikali itoe maelezo katika mkutano unaoendelea wa Bunge.

Lile la ufisadi wa EPA linasubiriwa baada ya muda wa miezi sita wa Timu aliyoiunda rais kufuatilia yaliyobainishwa na ripoti ya ukaguzi wa hesabu za EPA kumalizika wiki iliyopita.

Tunaitaka serikali isisikilize mbwembwe na madoido ya vikao visivyokuwa na ajenda. Itende. Ichukue hatua dhidi ya mafisadi kama Waziri Mkuu alivyoahidi taifa na ulimwengu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: