'Tunaogopa Dowans kama baba mkwe'


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version

NI hatari sana kuwa na viongozi woga. Ni hatari zaidi kuwa na viongozi wasio na maono. Ni hatari iliyopita kiasi kuwa na viongozi wasio wakweli kwa wanaowaongoza.

Lakini, ni hatari isiyokadirika kuwa na viongozi wenye hayo yote matatu kwa wakati mmoja.

Suala la Dowans na jinsi ambavyo wale wanaojiona ni viongozi wanavyolishughulikia, inanifanya niamini pasipo shaka, nchi yetu inalea viongozi wenye hayo matatu: woga, wasio na maono na wasio wakweli.

Kwa muda mrefu tumekuwa tukizungumzia suala la Dowans na tunafahamu kwa juujuu jinsi gani kampuni hii “ilirithi” mkataba wa Richmond.

Kitu kimoja ambacho serikali na viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hawataki kuambia wananchi, ni ukweli kuhusu kampuni hii; wanahofia ukweli huo ukifahmika wananchi wataelewa sababu za serikali kupwaya mbele ya “wawekezaji” wa Dowans.

Kwa ufupi Dowans ni kampuni iliyoundwa kurithi shughuli za kampuni hewa ya Richmond hasa baada ya Richmond kufahamika kuwa ni ya mfukoni na hivyo kuwekewa kigingi.

Mmiliki mkubwa wa Dowans ni Brigedia Jenerali Suleiman Al-Adawi ambaye ni afisa katika jeshi la Umoja wa Falme za Nchi za Kiarabu (UAE) na mtu wa karibu na nyumba ya Zayed (watawala wa UAE). Huyu na wenzake wamelenga kuchota utajiri wetu mithili ya wanaochota maji kisimani.

Kundi lao na washirika wao, Watanzania (wakiwemo waliowahi kuwa Ikulu na waliopo Ikulu na taasisi nyingine), wamekuwa na mipango mingi ya namna ya kuvuna utajiri nchini kwa jina la “wawekezaji.”

Kwa wale wasiojua, kundi hili ndio wahusika wakuu wa suala la Loliondo, bonde la Yaeda Chini nyumbani kwa Wahadzabe na sasa wako kwenye suala la Dowans na sitoshangaa wakiwa tena kwingineko.

Kampuni ya Dowans ilirithishwa kinyemela “mkataba” wa Richmond huku wahusika wake wakuu wakitarajia kuwa zitapatikana fedha za haraka. Lengo lilikuwa ni kujipatia si chini ya Sh. 70 bilioni katika kutatua tatizo la umeme nchini.

Lakini lengo la pili, kwa mujibu wa mkataba huo, ni uamuzi wa serikali kununua majenereta yaliyoletwa nao baada ya mkataba kumalizika. Matokeo yake ni washirika hawa kujitengenezea kiasi kingine cha mabilioni ya shilingi. Hilo ndilo dili lililotakiwa kuchezwa.

Sasa kuna watu wanachanganya mambo. Tanzania ina upungufu katika kutengeneza nishati; siyo upungufu wa vyanzo vya nishati. Vyanzo vya nishati vipo.

Bali utaona watawala wetu wanataka tujadili majenereta badala ya kujadili mmiliki wake. Wao hawajali majenereta yameletwa na nani na katika mazingira yapi. Wanataka wananchi wafumbie macho yote hayo; badala yake, wakubali fedha zao zitumike kuyanunua ili waamini tatizo la nishati limetatuka.

Kina William Ngeleja (waziri wa nishati na madini) na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Idris Rashid hawataki kabisa tuzungumzie mmiliki wa mitambo au iliingizwa vipi.

Wanataka tuzungumzie matatizo yetu na kuwa Dowans ipo tayari kutuokoa. Hawataki tufuatilie uhalali wa Dowans kuwepo nchini; hawataki tuhoji kampuni hii imewahi kufanya wapi biashara ya nishati; hawataki tuulize maswali kama hayo.

Wanachotaka wao ni kuwa wananchi waone uchungu kwa kukosa umeme (na baadhi ya magazeti na wengine wameanza kusalimu amri), ili tuweze kununua mitambo hii. Wanajua tatizo lilipo.

Kwanza, Dowans hawana uhalali wa kuwepo nchini kwani wametoa taarifa za kilaghai. Pili, Dowans kama ilivyooneshwa huko nyuma, hawakurithi mkataba halali kisheria maana kampuni ambayo inadaiwa kuingia nayo mkataba haikuwepo kisheria.

Tatu, wamiliki wake na wale waliowaleta wanatakiwa kufikishwa mahakamani kwa udanganyifu. Mambo haya matatu yanatosha kuipa serikali yoyote duniani meno ya kutaifisha kampuni hiyo na mali zake na kuwatia hasara watakayoikumbuka maishani.

Kitu kimoja kinachonikera sana ni hii imani kuwa wawekezaji hawatakuja nchini tukiwa na misimamo inayoeleweka na kuchukua maamuzi magumu yanayostahili. Kwamba tukiifurumua kampuni yoyote ya kitapeli nchini basi tunafukuza wawekezaji.

Mawazo haya ni ya kitumwa na yanaendeleza fikra za unyonge. Ninachukia kusikia kuwa hatuwezi kusimama kama watu wazima na wenye akili timamu vichwani na kuwakatalia wawekezaji uchwara.

Tunawaogopa kwa sababu eti tukiwapigia kelele watatutishia kuwa watafunga biashara zao na kurudi kwao. Hivyo kuanzia ikulu hadi tarishi, wote wamebakia wakiwapigia wawekezaji magoti kana kwamba ni wakwe zao.

Unyonge wetu ndio uliotufanya tudharauliwe; ni ukimya wetu umetufanya tunyonywe, na ni woga wa watawala wetu umefungua milango ya ufisadi nchini. Tunaibiwa wala hatutaki kupiga kelele; kwa sababu eti wawekezaji watakimbia.

Ndio kusema watawala wanaendesha serikali kwa ajili ya kufurahisha wawekezaji siyo kuridhisha wananchi waliopiga kura.

Hakuna mwekezaji yeyote nchini ambaye ameingia kwa haki, anafanya biashara kwa haki na anayetutakia sisi na watu wetu mema, ataamua kukimbia tukitaifisha Dowans. Hakuna.

Hakuna mwekezaji yeyote ambaye atasema tunarudisha ujamaa ati tukiamua kukataa fikra za kinyonge zinazoendekezwa na watu wachache nchini. Hayupo.

Tunaona Ngeleja na serikali nzima ya Rais Kikwete inaamini, kwa moyo wote na kwa miungu yao, kuwa Dowans ndio mkombozi wa tatizo la nishati nchini.

Hawa pia tayari wanajua kuna fedha za kuwapa Dowans hata kama hatujui walivyoingia nchini na wamejikanyaga vipi kwenye fomu zao za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).

Kama hivyo ndivyo, basi mimi nasema Kikwete, Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, baraza lote la mawaziri na watendaji wao wote wakuu, wawe wa kwanza kwenda kwenye ofisi za Dowans kuwapigia magoti na kuwabembeleza wasiondoe mitambo yao.

Natumaini katika taifa langu bado wapo masalia walio tayari kutupwa kwenye tanuru la moto kuliko kuuza utu wao kwa wageni na kupigia wezi magoti.

Ndani ya serikali nataka kuamini wangalipo watu – hata kama ni wachache – wenye ujasiri wa kupinga nidhamu ya woga na fikra za uduni; natumaini wapo katika Tanzania viongozi wa kisiasa walio tayari kuamsha wananchi wakatae utumwa huu wa kifikra na ubeberu wa kimawazo.

Kama hawapo, basi tukubali tu tuwalipe Dowans, tununue majenereta yao, na miezi michache ijayo mgao mwingine uanze.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: