Tunaongozwa kama Shamba la Wanyama


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 24 March 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

MWANDISHI mmoja wa vitabu aitwaye George Orwell aliamua kuwachekesha watu alipoandika kitabu alichokiita Shamba la Wanyama (The Animal Farm).

Kila anayesoma kitabu hicho, anabaki akifurahia ufundi wa msanii huyo na anabaki akihusisha vituko au visa na nchi anayoishi. Je, inaweza kuwa Tanzania yetu? Je, serikali yetu ina viongozi aina ya nguruwe?

Inaelezwa baada ya wanyama hao; ng’ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe, mbwa, paka, punda nk, kuchoshwa na utawala wa binadamu waliamua kufanya mapinduzi na kushika uongozi yaani kujitawala wenyewe.

Wakaanza kujenga taasisi mbalimbali kwa ajili ya ustawi wa kila mnyama. Wakaanzisha zahanati kwa ajili ya kuhakikisha afya bora kwa kila mmoja.

Walianzisha shule kwa ajili ya wasiojua kusoma na kuandika. Kazi hiyo ilifanyika kwa ukamilifu hadi wanyama wagumu kuelewa kama kondoo wakawa na uelewa mkubwa.

Vilevile wakaimarisha taasisi za haki na utawala bora chini ya uongozi wa nguruwe aitwaye Napoleon na wakabandika kila mahali kauli mbiu ya Maisha Bora kwa Wote. Ndoto zao zilikuwa kuishi katika dunia ambayo wanyama wote ni sawa na wanapaswa kugawana raslimali kwa usawa.

Lakini taratibu matumaini yao yakaanza kufifia. Ahadi za msingi za wanyama wote ni ndugu zangu, nitatumikia nchi yangu na wanyama wote kwa haki na usawa, rushwa ni adui wa haki, cheo ni dhamana zikabaki kwenye makabati na nyingine zilibadilishwa kinyemela.

Mathalan, ahadi iliyohubiri usawa wa wanyama wote na kubandikwa hadharani “Wanyama Wote ni Sawa” ikaongezewa maneno kinyemela halafu kibao kikapinduliwa kisisomeke vizuri “Wanyama Wote ni Sawa lakini Wengine ni Sawa Zaidi”.

Awali kila mnyama alikuwa na haki ya kupata maziwa lakini baadaye ni nguruwe tu (tabaka tawala) waliokuwa wanapewa. Vitu vizuri na maslahi makubwa yalibaki kwa tabaka hilo. Udikteta ukaota mizizi.

Matumaini ya wanyama chini ya Napoleon hayana tofauti na Tanzania iliyoanza kujenga utawala bora chini ya Azimio la Arusha nwaka 1967 lililoweka miiko ya uongozi. Watu wakawa wanalima kijamaa, viongozi wakazuiwa kuwa na nyumba za kupangisha, kuwa na mishahara miwili na kuwa na hisa katika mashirika binafsi.

Mwalimu Nyerere akatufundisha ili nchi iendelee inahitaji Watu, Ardhi, Siasa safi na uongozi bora na kwamba pesa si msingi wa maendeleo. Tuliimba hivyo hadi mwaka 1991, jamaa walipokutana kwenye mji wa marashi ya karafuu, Zanzibar ambako walitangaza Azimio la Kifisadi lililofuta Azimio la Arusha. Hee, Mzee Ruksa anasema halikufutwa!

Tanzania ikaandaliwa kuwa mkono wa ubepari wa kimataifa na pepo ya mafisadi kwa kufuta miiko ya uongozi na kuzalisha viongozi wasiojali maslahi ya wananchi. Eti wanatufundisha kwa nguvu “ili nchi iendelee inahitaji wawekezaji, pesa, siasa za kifisadi na uongozi wa kibabaishaji” enzi hizi za utandawazi.

Mabepari ambao wanaitwa wawekezaji wanaabudiwa na serikali, wananyenyekewa na kuuziwa kama njugu raslimali za nchi kupitia sheria mbaya ya ubinafsishaji.

Kupitia sheria hizo kiinimacho wakatwaa Kiwira, Meremeta, wakanunua hisa kwenye makampuni ya kibepari na viongozi mafisadi wakajijengea utukufu kwa kujenga mahoteli, mahekalu ya kuishi. Viongozi wakaanza kulamba mishahara miwili na zaidi na kujikusanyia posho. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ikawekwa mfukoni.

Kama Shamba la Wanyama ahadi waliyoingia nayo ya ‘Maisha Bora kwa Wote’ haipo, tunashuhudia kuporomoka kwa maadili ya utawala bora na utu. Nyumba za walalahoi zinabomolewa ili wajiuzie maeneo wajenge ‘Satelite Towns’.

Moja ya hotuba za kwanza za Rais Jakaya Kikwete zilizovutia watu wengi ni ahadi kwamba kiongozi atakayekumbwa na tuhuma tu itakuwa inatosha kujitenga naye, lakini anafanya kinyume chake. Akamkumbatia jamaa mwenye tuhuma za kuweka vijisenti vya rushwa ya rada kwenye moja ya visiwa vya Malikia.

Pia amegoma kuwaachisha nyadhifa watuhumiwa wa kupitisha mkataba wa kifisadi unaoipa Richmond kazi ya kufua umeme wa dharura. Akampa ukuu wa wilaya jamaa aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya kupokea rushwa.

Ikulu siyo tu imewahakikishia Maisha Bora Mafisadi bali pia imewapa jeuri ya kufanya lolote bila kuulizwa wala kufuatwa fuatwa na vyombo vya sheria.

Jeuri yao ni kubwa sasa. Wananchi wamelalamikia mazingira ya kutiwa saini mgodi wa Buzwagi, kwamba haikuwa sahihi waziri kukimbia na mkataba kwenda nao Uswisi badala ya ofisini Dar es Salaam. Ili kuonyesha jambo lile lilikuwa na baraka za Ikulu, Kikwete alifunga safari hivi karibuni kwenda kuusifu mgodi huo na kuwaacha mamia ya watu wakihaha kulipwa fidia yao.

Wakazi wa Nyamongo mkoani Mara wamelalamikia Mgodi wa North Mara kuwasababishia maafa kwa kutiririsha sumu kwenye Mto Tigithe wanaotumia maji ya kunywa, Kikwete akapuuza malalamiko hayo akaenda kuwapongeza wamiliki Kampuni ya Barrick Goldmine kwa kazi nzuri.

Hata uchunguzi wa kitaalamu uliopaswa kufanywa na serikali kuhusu watu walioathiriwa na kemikali za paf na cyanide haukufanyika kwa madai hawana pesa. Hivi inangia akilini kweli?

Hapa ina maana mchezo umekwisha kitu muhimu kwa serikali ni pesa za wawekezaji si uhai wa wakazi wa Nyamongo wala Buzwagi ambao wanahitaji kufarijiwa na viongozi wao wa juu. Je, huu si utimilifu wa kauli ya Nyerere kwamba serikali fisadi inawatumikia mabepari na siyo watu wake? Ndivyo ilivyo katika Shamba la Wanyama tunamoishi.

Tazama serikali inavyombeba mwekezaji aliyewatoa baruti wakazi wa Ngorongoro! Halafu mahakama wilayani Bunda ikawafunga vijana watatu akiwemo mtoto wa shule kumfurahisha mwekezaji. Kuna siku watahitaji kujenga hekalu Ikulu wataruhusiwa tu.

Japokuwa alikuwa anajua kabisa hoteli imejengwa kwenye eneo la hifadhi ya barabara Arusha, Kikwete alikwenda kuifungua, siku ya pili yake Tanroads wakaivunja, lakini kwa vile wamejengewa kiburi siku iliyofuata ikajengwa tena.

Tunaweza kutofautiana kwa fasili maana ndivyo fasihi ilivyo, Tanzania inaongozwa kama Shamba la Wanyama. Serikali imefuta msingi wa maendeleo usemao ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora imegeuza kuwa ni wawekezaji, pesa, siasa za kifisadi na uongozi wa kibabaishaji .

Leo inawezekana kweli kuna watu na ardhi, lakini kuna siasa safi gani hadi sasa? Uongozi ukoje? Kwa kifupi siasa ni za kifisadi na uongozi wa kutetea ulafi wa viongozi na matajiri.

Kwa bahati mbaya wanyama wengi wapigakura wenye mashati ya kijani, sketi au suruali nyeusi na kofia za njano chini ya Kikwete hawajashtuka. Hiki ndiyo kiama cha maisha ndani ya Shamba la Wanyama.

0
Your rating: None Average: 4 (2 votes)