Tunapigania haki ya wote


editor's picture

Na editor - Imechapwa 22 December 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

SASA serikali imepitiliza katika kunyanyasa gazeti hili. Ijumaa iliyopita, mwandishi wetu, Saed Kubenea, alizuiwa kuingia mkutanoni Ikulu.

Ulikuwa mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Tumezoea kushutumiwa, kubezwa na kusimangwa na serikali. Tumezoea vitisho vya waziri wa habari. Tumezoea vitisho kwa njia ya simu, kwa kuambiwa iwapo hatujui kufa tutazame kaburi.

Hatujasahau na hatutasahau waliotuma vijana wenye njaa kuvamia ofisi zetu; kutumwagia tindikali na kutujeruhi kwa kutukata mapanga.

Tunakumbuka sana jinsi serikali ilivyoshindwa kufanya upelelezi wa kesi hiyo ya jinai hadi hakimu akaifuta.

Hatutasahau wapelelezi walioshindwa kufuatilia taarifa za waliolipa wavamizi; wakiwanuiza ama kuua au kuumiza vibaya, waandishi wa gazeti walilodai linawaumbua.

Siyo rahisi kusahau uzembe wa serikali, kwa kutotumia utaalam wake wote, kudaka watunga njama za uvamizi wanaodaiwa walikuwa wakikutana katika baa moja karibu na soko la Mwanyamala jijini Dar es Salaam, kilometa moja na nusu kutoka ofisi yetu.

Matokeo ya uvamizi ule wa kiharamia katika ofisi zetu, ni hali tete ya afya ya macho ya Kubenea, mwandishi wa habari anayepaa; na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd (HHPL).

Tunajua kuwa mafisadi waliotuma wahuni kutuangamiza, bado wanakula na kusaza huku wakichekelea. Wanaumia kwa kuwa hatukuangamia; lakini wanajifariji kuwa walidiriki kutukumbusha kuwa kifo kipo.

Tunakaa siku zote tukikumbuka Idara ya Habari (MAELEZO) na kutarajia kuitwa, kuhojiwa na hata kuulizwa maana ya neno tulilotumia katika makala.

Inaonekana waandishi waandamizi wa MAELEZO wameelekezwa kusoma kila neno linalochapishwa katika gazeti letu, ili hatimaye, wapate cha kuihoji MwanaHALISI.

Tunaweza kusahau vipi ile hatua ya kulifungia gazeti letu kwa siku 90 mwaka 2008; kwa shabaha tu ya kuliua.

Sasa hili la wiki iliyopita, la kumkatalia mwandishi wetu kuingia mkutanoni, linadhihirisha chuki, uadui na woga usiokuwa na msingi kwa chombo chetu; kwa chombo cha umma.

Tunaandikia umma. Ni umma unaotuita. Unaotutuma. Nasi tunaitika na kuutumikia. Nguvu yetu ni wasomaji wetu, hata wale wanaotufukuza ikulu.

Na hata tusipoingia ikulu, tutawashangaza wengi kesho yake tutakapotoka na kauli za wote walioshiriki hoja, au hata hila. Kwani hii kazi ya uandishi tunaielewa vema. 

Bali tunalilia haki yetu ya kupata habari kwa manufaa ya wananchi. Tunalaani kitendo cha kufukuza mwandishi wetu. Na hapa, tunakata rufaa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: