Tunapuuza msingi, tutapataje nyumba imara?


Sophia Yamola's picture

Na Sophia Yamola - Imechapwa 02 February 2011

Printer-friendly version

MWENENDO wa elimu nchini unasikitisha. Mfumo wa kuihudumia umeshindwa. Umejaa kasoro. Sera zake kama siyo mbaya basi hazitekelezwi kitaalamu. Siasa imeshika kasi katika utekelezaji ushauri wa wataalamu.

Matokeo mabaya ya mitihani ya wahitimu wa elimu ya msingi na sekondari ndio ushahidi usiobishika.

Ukiangalia kwa mbali, unaona dhahiri tabia ya serikali inahimiza zaidi maendeleo ya elimu ya juu; kwenye vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu. Haijali sana kujenga msingi wa elimu ya ngazi za chini.

Masikini roho za viongozi wanaoidhinisha sera na mifumo ya kusimamia maendeleo ya elimu. Hakuna uwajibikaji na badala yake kila kitu kinaendeshwa shaghalabaghala.

Kwa sababu utekelezaji wa sera za kuimarisha elimu ya chini haufanywi kitaalamu bali kisiasa zaidi, mazao yanayopatikana hayana rutuba.

Unaanzia shule ya msingi ndipo ufike sekondari. Aliyeko chuoni ametokea chini. Iwapo hakujengwa vizuri, hatakuwa mzuri chuoni leo wala kesho. Tuna mfumo wa kuzalisha wahitimu wasioiva. Mabomu.

Utafiti uliofanywa na shirika lisilo la kiserikali la Mpango wa Elimu Tanzania Education Network (TENMET) mwaka 2010, unaonesha kuwa Kiswahili, ingawa ndio lugha ya Taifa nchini, kinatatiza watoto wengi walioko shule.

Takwimu zilizotokana na utafiti huo, zinaonesha kuwa wanafunzi wengi hawawezi kusoma vitabu vya hadithi vya Kiswahili na pia hawawezi kuzungumza vizuri kwa lugha hiyo.

Kati ya watoto 1,000 wanaomaliza darasa la saba, utafiti unaonyesha, watoto 200 hawajui kusoma kwa lugha ya taifa. Maana yake ni kwamba idadi kubwa ya watoto wanamaliza elimu ya msingi bila ya kujua kusoma.

Lugha ya Kiingereza ndio imekuwa tatizo kubwa zaidi. Takwimu za TENMET zinabainisha kuwa kati ya watoto kumi waliopo darasa la tatu shuleni, mtoto mmoja tu ndio anaweza kusoma kitabu cha Kiingereza tena ni cha darasa la pili.

Ukitaka kujenga nyumba imara lazima kwanza ujenge msingi imara wa nyumba hiyo. Hata wasomi wazuri wa vyuo na taasisi za elimu ya juu, lazima wawe wameandaliwa vema katika madaraja ya msingi na sekondari.

Lugha inayotumika kufundishia wanafunzi shule ya msingi ni Kiswahili, lakini wanafunzi wanapojiunga na elimu ya sekondari lugha ya kufundishia hubadilika na kutumika Kiingereza.

Kwa lugha hiyo ya kigeni, idadi kubwa ya wanafunzi wanapata matatizo ya kusoma kwa utulivu na ufanisi. Hawakupata msingi mzuri wa kuzoea lugha hiyo walipokuwa shule ya msingi, ni vigumu kufuata walipoingia sekondari.

Serikali ilipoanzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya msingi (MMEM) mwaka 2002 ililenga kutoa elimu bure kwa wanafunzi wote wa shule za serikali. Ikatoa ruzuku kwa kila mwanafunzi kiasi cha Sh. 10,000 kwa mwaka ili kuziba pengo la ada na michango iliyoondolewa.

Sera hiyo ilikusudiwa kuendana na mahitaji ya taifa katika kutekeleza moja ya malengo ya milenia: kuhakikisha kila mtoto anayestahili kusoma anapelekwa shule.

Malalamiko yakaibuka katika shule mbalimbali kwamba fedha hizo zinachelewa kufika kwa utawala wa shule za msingi. Matokeo yake viongozi wa shule wanalazimika kuomba wazazi na walezi wa watoto wachangie huduma mbalimbali.

Michango inayodaiwa na shule ni dawati kwa kila mwanafunzi, karatasi, pesa za kulipa walinzi, tofali moja na pesa za mitihani kila wiki. Bila ya shaka katika mazingira kama hayo na hasa kwa kuzingati wazazi wenyewe wanakumbwa na maisha magumu, shule zinakosa huduma muhimu.

Vipato vya wazazi wengi ni vidogo ndio maana wenyewe wanahaha kutafuta chakula na mahitaji mengine ya kila siku katika familia. Kutenga kiasi kwa ajili ya michango ya shule inakuwa jambo gumu.

Uvumilivu wa wakuu wa shule unatoweka. Wanaamua kurudisha nyumbani watoto ambao wazazi wao hawajatoa michango hiyo. Mtoto kuwa nje ya darasa wakati wengine wanaendelea kusoma, inajenga hisia mbaya kwake. Baadhi ya watoto wanaacha shule kwa adha ya kila siku.

Yote hayo yasingetoka iwapo serikali imewajibika kimajukumu na kuidhinisha malipo ya ruzuku kwa shule za msingi kwa wakati unaotakiwa.

Wanafunzi wenye ulemavu wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mengi shuleni na utafiti uliofanywa mwaka 2008 na shirika la HakiElimu umebaini kuwa shule nyingi zina miundombinu mibovu, walimu hawana mafunzo ya elimu ya watoto wenye mahitaji maalumu na kuna ukosefu mkubwa wa vifaa vya kufundishia wanafunzi hao.

Maeneo mengi yaliyotembelewa na watafiti wa shirika hilo yamekutwa na majengo ya shule yenye ngazi ndefu ambazo watoto wenye ulemavu wa viungo hawawezi kupanda kwa kuwa wanatumia baiskeli maalum.

Wanafunzi hao pamoja na wale wasioona hupata shida kutembea kutoka eneo moja kwenda eneo jingine wanapokuwa katika mazingira ya shule.

Watafiti walielezwa na wakuu wa shule kuwa matatizo yangepungua kama ungeanzishwa mfuko maalum wa kusaidia wanafunzi walemavu wanaohitaji mahitaji maalum. Hayo yanabainika hata kwenye shule za sekondari za bweni.

Serikali kama ina nia ya dhati ya kuimarisha elimu ya juu basi inapaswa kutambua haja ya kuimarisha elimu ya misingi na sekondari ambako ndiko hupikwa wale wanaoiangia vyuoni.

Ichukue hatua kutatua tatizo la upungufu wa walimu wenye ujuzi wa kufundisha ngazi ya elimu ya msingi na sekondari. Imalize tatizo la ukosefu au uhaba wa vifaa vya kujifunzia, vitabu vya kiada na ziada.

Baadhi ya wahitimu wa sekondari wanasema wazi kuwa hawajapata kuona vifaa vya maabara na kuwa walifanya mtihani ya masomo ya sayansi kwa kubahatisha.

Shule za serikali zilizopewa jina la St. Kayumba zimekuwa zikiwastiri wengi ambao kwao ni ndoto kuweza kulipa fedha nyingi zinazotakiwa kwa ajili ya ada katika shule binafsi ambazo ni za gharama kubwa.

Kwa kutazama matatizo yanayozikabili shule za msingi na sekondari, na uzito wa serikali kutatua matatizo hayo, ni rahisi kusema taifa linaingiza vijana wasioiva kwa ajili ya kujifunza taaluma mbalimbali vyuoni.

0715 221208
0
No votes yet