Tunataka kura ya amani Igunga


editor's picture

Na editor - Imechapwa 28 September 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

TUNAHIMIZA amani Igunga. Ndio wajibu wetu. Tuwasihi wananchi wa jimbo hili, linalokabiliwa na uchaguzi mdogo wa ubunge, wajizuie na vurugu.

 Matukio yanayoripotiwa kutokea kipindi hiki cha kampeni ya uchaguzi huo wa Jumapili ijayo, 2 Oktoba, yana mchango mkubwa wa mfungamano uliopo kati ya chama tawala na serikali.

Chama hicho – Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeamua kuthibitisha kilivyo chama dola. Kinapanga na kupangua na kutekeleza mbinu zake kwa kutegemea mgongo wa vyombo vya dola.

Kinachoonekana ni mikakati yake kutaka kurudisha kiti kwa gharama yoyote. Kwa bahati mbaya, hilo linafanywa huku viongozi wakisahau kwamba wamebeba dhamana ya ulinzi na usalama wa nchi na raia.

Wanaijua dhamana hii bali kwa makusudi wanaipuuza na badala yake wanaitumia kutisha watu na kuwavuruga wasisikilize kampeni za vyama vingine.

Hizo ni siasa za kijambazi; zile ambazo aliwahi kuzikemea Dk. Omar Ali Juma (Mwenyezi Mungu amrehemu), alipokuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar na baadaye Makamu wa Rais wa Tanzania .

Alipokuwa akikemea siasa chafu, alisema haiwezekani wanasiasa wakaanzisha siasa za kijambazi kwa kuchochea wananchi wapambane na kuasi nchi yao . Alikuwa akilenga wapinzani.

Leo, ni chama kinachoshika dola, CCM, ambacho kinashuhudiwa kikisuka michoro ya kuingiza watu katika migogoro ya kisiasa. Kisa? Kiti cha ubunge lazima kirudi CCM.

CCM ndio chimbuko la uchaguzi mdogo Igunga. Walimfikisha Rostam Aziz kwenye kona hadi akaamua kujiuzulu ubunge. Mwenyewe alisema “siasa uchwara” zilizojaa “chuki na fitina” ndani ya chama chake zimemsukuma kuachia uongozi.

Tusingependa siasa hizo zikahamia kwa jamii kubwa. Zibaki hukohuko CCM. Kama ni gamba wavuane, wasihusishe wengine. Ni muhimu waelewe makosa yao .

Tunataka kila chama na kila kiongozi aliyeko Igunga ajiheshimu. Ni muhimu wagombea wote wa kiti cha ubunge pamoja na wapambe wao wanaofuatana katika mikutano ya kampeni, wajiheshimu.

Yule anayedhani vurugu ndio njia ya kupata kura za wananchi wema, huyo ni kiongozi mchovu. Amechoka. Kwanza , akome. Pili, tunashawishi umma – hasa wale wenye kura mkononi wakisubiri kuziweka visandukuni Jumapili, wawakatae viongozi wa aina hii.

Wananchi wa Igunga hawana historia ya kupiga kura ndani ya vishindo kama inavyotokea sasa. Wanajulikana ni watu watulivu wanaojua nini wanachokitaka. Wapewe nafasi ya kuchagua watakacho.

Tunataka kura kwa amani.

0
No votes yet