Tunataka kura ya amani Zanzibar


editor's picture

Na editor - Imechapwa 28 July 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

JUMAMOSI ijayo yaani tarehe 31 Julai, ni siku ya wananchi wa Zanzibar watapiga kura kufanya maamuzi kuhusu mfumo wa utawala Zanzibar iwepo au isiundwe Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kila Mzanzibari aliyeandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar, anapaswa kushiriki kutumia haki yake ya kikatiba ili kuamua mustakbali wa visiwa hivyo.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupendekeza kubadilisha mfumo wa sasa wa utawala ili iundwe Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kwa kuwa hilo ni jambo zito linalogusa utashi wa kila mwananchi, umependekezwa utaratibu wa Kura ya Maoni kutoa nafasi kwa mwananchi kutoa msimamo wake.

Kura ya Maoni ni muhimu kwa kila Mzanzibari kwani ndiyo itachangia kumaliza mvutano wa kisiasa uliodumu kwa miaka mingi kutokana na tofauti za kiitikadi.

Ikiwa wananchi wengi watasema NDIYO ina maana wanaridhia chama kinachoshinda nafasi ya urais kishirikiane na vyama vingine kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, badaa ya utaratibu wa sasa.

Tangu uchaguzi mkuu wa vyama vingi mwaka 1995, imebainika hakuna chama kinachoweza kushinda kwa asilimia kubwa; na malalamiko yamekuwa yakianzia hapo na kufikia kuwagawa Wazanzibari makundi mawili.

Lakini baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Amani Abeid Karume na Katibu mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharrif Hamad kufanya vikao mara kadhaa na kuviarifu vyama vyao, wakakubaliana mfumo huo ubadilishwe.

Hatimaye Kura ya Maoni iliidhinishwa na Baraza la Wawakilishi, chombo cha kutunga sheria ambacho kulingana na Katiba ya Zanzibar, ndicho kinachotumika kuwakilisha mawazo ya wananchi.

Tunapongeza kwa hatua iliyofikiwa na tunawatakia Wanzanzibari kila la kheri katika upigaji wa kura hiyo. Hata hivyo tunatoa darasa elekezi kwa wasimazi.

Kura ipigwe kwa haki na kufuata misingi yote ya demokrasia. Kila anayestahili yaani aliyeandikishwa kwenye daftari la wapiga kura aachiwe huru kufika kituoni na kupiga kura yake kwa amani.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano zitoe ulinzi wa kutosha ili uwepo ulinzi na usalama ili hali iliyodumu wakati wote wa maandalizi ya kura ya maoni, iendelee hadi siku ya upigaji kura.

Tunaamini kwamba, kwa kuwa elimu kuhusu kura ya maoni imetolewa kwa wananchi kupitia njia mbalimbali, matokeo yake yataheshimiwa.

Amani, upendo na mshikamano kwa Wazanzibari utarejea na kuimarishwa kwa kura ya maoni ya kila mwananchi Jumamosi hivyo tunahimiza kila raia atomize wajibu huu wa kuijenga upya Zanzibar kijamii na kiuchumi.

0
No votes yet