Tunataka mabadiliko Zanzibar


editor's picture

Na editor - Imechapwa 11 November 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

CHAMA cha Wananchi (CUF) kinaendesha kampeni ya kujenga imani kwa wananchi kwamba hakijapotea njia. Viongozi wake wa juu wanatembelea matawi wakieneza neno "Tuitambue Serikali ya Rais Karume."

Ni kampeni mahsusi iliyoanzishwa baada ya wananchi kutoelewa neno hilo lilipotolewa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Shariff Hamad, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Kibandamaiti mjini Unguja, Jumamosi iliyopita.

Kufuatia idhini ya Baraza Kuu la Uongozi, lililokutana saa chache kabla ya mkutano huo, CUF imetamka sasa inatambua urais wa Amani Abeid Karume na serikali yake na kwamba imechukua uamuzi huo kwa nia njema ya kuleta maelewano nchini.

Hiki ni chama ambacho kimelalamikia matokeo ya uchaguzi tangu mwaka 1995 na kudai kinaporwa ushindi.

Lakini wakati CUF wakiendelea kulalamikia kuporwa ushindi, bado kinalazimika kufuta misimamo kwa nia ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro uliopo na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mara tatu vyama hivi vimekutana kwa majadiliano lakini hakuna muafaka uliotekelezwa sawasawa. Msimamo wetu ni kwamba CCM, inayoongoza serikali, ndio wenye tatizo la kukataa demokrasia.

Ni wao wameupiga kumbo muafaka uliokuwa nchani kusainiwa baada ya vyama hivyo kujadiliana kwa miezi kadhaa mjini Bagamoyo na Dar es Salaam.

CCM ilizua jambo jipya la kutaka makubaliano waliyofikia yapelekwe kwa wananchi kupitia kura ya maoni ya kuwauliza kama wanataka mabadiliko yaliyoazimiwa kwenye rasimu ya muafaka.

CUF ikakataa kurudi mezani na kushutumu CCM kwamba wamekataa muafaka kwasababu wamezoea siasa za kisanii. Ikamshambulia hata Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kwamba anaendekeza usanii katika siasa.

Baada ya kimya cha muda mrefu tangu muafaka ukwame, ghafla tumeshuhudia mkutano wa faragha uliokutanisha Maalim Seif na Rais Karume kwenye Ikulu ya Zanzibar.

Kilichofuatia, ni Maalim Seif kupanda jukwaa na kutamka kumtambua Rais Karume na serikali yake.

Hatua hii inaweza kuwa ya maana kwa mustakabali wa Zanzibar; kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Inaweza kuwa mwanzo wa kufutwa kwa siasa chafu visiwani Zanzibar.

Ila tunasema iwapo haitaendana na mabadiliko ya haraka katika masuala ya msingi – hasa maandalizi ya uchaguzi wa 2010 – ikianzia na kuruhusu kila mwenye haki ya kupiga kura aandikishwe bila ya kikwazo cha kipuuzi, kama cha kuhusisha kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi katika uchaguzi, hatua hiyo haitakuwa na maana yoyote isipokuwa kulaghai wananchi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: