'Tunataka madini yanufaishe Afrika'


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 27 January 2010

Printer-friendly version
Ana kwa Ana

TAASISI ya Revenue Watch (RWI) imefungua ofisi yake nchini Tanzania kwa ajili ya kusaidia kuleta uwazi katika biashara ya madini. Mwandishi Wetu, EZEKIEL KAMWAGA amekutana na Mshauri wa Sheria wa RWI, PATRICK HELLER aliyekuwa nchini kikazi. Fuatilia mahojiano hayo.

Swali: Revenue Watch Institute ni nini hasa na imeanzishwa kwa malengo gani?

Jibu: Hii ni taasisi yenye makao yake makuu jijini New York, Marekani. Lengo lake kubwa ni kuhakikisha kunakuwa na uwazi na uwajibikaji katika biashara ya madini kwa nchi zilizojaliwa kuwa na raslimali hiyo.

Ilianza mwaka 2002 ikiwa mojawapo ya miradi iliyo chini ya taasisi ya Open Society Institute iliyopo Marekani na ilikuwa ikifahamika kama Revenue Watch. Lakini Juni mwaka 2006, ndipo RWI hii tunayoiona sasa ilianza. Kwa sasa RWI ina ofisi Uingereza, Ghana na Indonesia.

Swali: Nani anafadhili shughuli za RWI?

Jibu: Kwanza ni lazima ufahamu kuwa hii ni taasisi isiyo ya kibiashara. Kazi zetu nyingi zinahusu kusaidia asasi za kijamii na vyombo vya habari katika nchi zinazohitaji msaada wetu kufanya kazi zake.

Wafadhili wetu wakubwa ni taasisi za Bill and Melinda Gates Foundation, William and Flora Hewlett Foundation na Open Society Institute.

Swali: Kwa uzoefu wenu wa kufanya kazi katika nchi za Afrika ikiwamo Tanzania, mnadhani ni kwa nini utajiri wa maliasili haujazinufaisha nchi masikini?

Jibu: Swali zuri. Kuna sababu nyingi na wakati mwingine zinatofautiana kutoka nchi hadi nyingine. Lakini kubwa kuna masuala ya ukosefu wa ujuzi, ugeni katika uchimbaji na rushwa.

Swali: Unaweza kufafanua kidogo katika eneo la ukosefu wa ujuzi na ugeni katika uchimbaji?

Jibu: Bila shaka. Ugeni katika uchimbaji umesababisha nchi nyingi masikini kuwa na sheria za uchimbaji madini ambazo hazina tija kwa nchi hizo. Nikupe mfano, wakati Tanzania ilipotunga sheria yake ya kwanza ya madini mwaka 1998, haikupata upinzani wowote kwa sababu hakukuwa na uelewa na mwamko kuhusu sekta hii kwa uchumi wa nchi.

Lakini sasa, baada ya muongo mmoja kwenye uchimbaji mkubwa, watu wamekuwa wakizungumzia kasoro zilizopo kwa uwazi na kwa mapana yake. Kwa hiyo hapo unaweza kuona pengine makosa yaliyofanyika mwaka 1998 yalitokana zaidi na uchanga wa nchi katika masuala haya kuliko mambo mengine.

Swali: Pamoja na ugeni na rushwa, je si kweli kwamba nchi tajiri siku zote hufikiria tu kuzinyonya nchi masikini? Kwa nini zinashindwa kuzisaidia nchi zenye utajiri wa raslimali kuwa na sheria nzuri zitakazozisaidia kufaidika na utajiri huo?

Jibu: Niseme awali kwamba mimi si miongoni mwa wale wanaoamini kuwa mataifa tajiri huja Afrika kwa ajili tu ya kuziibia nchi hizo. Naona hili halina ukweli sana.

Ila nilicho na uhakika nacho ni kwamba makampuni yanayokuja kuwekeza katika nchi masikini huongozwa na watu wenye mtazamo wa kupata faida zaidi.

Kule Ulaya na Marekani, kiongozi mzuri wa kampuni hupimwa kwa kuangalia ni faida kiasi gani ameiletea kampuni yake. Kama kampuni haina faida, yeye anaonekana hafai. Kwa hiyo watu wanatafuta faida.

Haya ni makampuni ambayo yamesajiliwa katika masoko ya hisa na wanahisa wake wanataka kupewa gawio lao kila mwaka. Ndiyo maana makampuni haya huwa yanaangalia zaidi faida.

Kwa hiyo hapa cha msingi ni kwa nchi husika kuridhia mikataba ambayo itanufaisha nchi zao. Wakikubali kulainishwa kwa rushwa na kuyafaidisha makampuni ya kigeni, hili linakuwa tatizo la nchi na si makampuni.

Swali: Hamjisikii vibaya mkiwa kwenu kwamba mnakuja kutoa elimu na mipango ya kukomesha wizi wa raslimali barani Afrika wakati nchi zenu ndizo zinazochochea wizi huo?

Jibu: Hapana, hatujisikii vibaya. Sisi tunafanya lile ambalo tunadhani ni sahihi na wengine wanafanya lile wanaloona ni sahihi kwao.

Mwisho wa siku, ni jukumu la serikali za Afrika, asasi zake za kiraia pamoja na vyombo vya habari kushinikiza kuwapo kwa mazingira yatakayozinufaisha nchi zao na utajiri wa rasilimali zao. Na sisi tunawawezesha kufanya hivyo.

Swali: Mnawawezesha vipi?

Jibu: Tunatoa misaada ya kitaalamu na kifedha kwa asasi hizo na vyombo vya habari katika kuhakikisha vinasaidia kuchochea uwazi na matumizi mazuri ya mapato kutokana na raslimali walizonazo.

Tunatoa machapisho mbalimbali yenye kuelimisha, tunaandaa mikutano na makongamano yanayohimiza uwajibikaji na uwazi katika mapato yanayotokana na raslimali za nchi husika.

Usisahau pia kwamba sisi huwa tuna mpango maalumu wa kubadilishana wafanyakazi kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa lengo la kubadilishana uzoefu na maarifa.

Swali: Wewe ni mwanasheria. Una maoni gani kuhusu Sheria ya Madini ya Tanzania ya mwaka 1998 na mapendekezo ya sheria mpya iliyoko hatua ya muswada?

Jibu: Nikiri kwamba sheria ilikuwa na mapungufu katika baadhi ya vipengele na nafurahi kwamba serikali imekubali kuifanyia marekebisho na naona, kama mapendekezo ya wadau katika sheria mpya yatazingatiwa, Tanzania itaanza kufaidi utajiri wake.

Swali: Ni kwa njia zipi, ukitoa mifano michache, ambazo unafikiri taasisi kama RWI zinaweza kusaidia Tanzania kufaidika na utajiri wake?

Jibu: Sisi tunashiriki kwa karibu sana katika mpango wa Publish What You Pay (PWYP) – Tangaza Unachopokea na Unacholipa – na Extractive Industry Transparency Initiative (EITI) – juhudi za kuweka wazi mapato yatokanayo na madini na vito vya thamani.

Swali: Mnashiriki vipi katika asasi hizo?

Jibu: Kupitia PWYP, serikali pamoja na makampuni yanayochimba madini yanatakiwa kutoa taarifa zilizochapishwa kuhusu nini hasa kililipwa na nini hasa kilipokewa.

Kwamba kama kampuni A inasema ililipa Sh. 20 bilioni katika kodi, basi ionyeshe stakabadhi; na serikali pia ithibitishe hilo kwa maandishi. Huku ndio kuweka wazi mapato.

Sasa kupitia EITI, tunakwenda mbele zaidi. Kama tutaona, kwa mfano, kampuni imeonyesha kuwa imelipa Sh. 10 bilioni, halafu serikali inasema imepokea Sh. 7 bilioni tu, hapo tunaanza kuchunguza nini kimetokea.

Tukigundua vitendo vya udanganyifu, kazi yetu ni kubainisha hadharani na kuziachia taasisi husika kuendelea na hatua nyingine. Kazi ya EITI si kukamata watu au kufanya uchunguzi wa kipolisi. Sisi tunalinganisha tu taarifa na kutafuta chanzo cha hiyo tofauti ya malipo. Kuna utaratibu maalumu uliowekwa katika kuhakikisha kuwa ukaguzi kama huo unafanyika kwa uwazi na watu wanaoheshimika katika jamii.

Swali: Hapa Tanzania RWI ina ofisi yoyote?

Jibu: Ndiyo. Tuna ofisi na kwa sasa mratibu wetu ni Bw. Silas Olang’.

Ofisi za RWI zipo Kiwanja Na. 436, Mikocheni II, Old Bagamoyo Road. Wanapatikana kwa S.L.P. 3955 Dar es Salaam. Simu: 022 277 16 50 na 0222 200 252. E-mail: solang@revenuewatch.org
0
No votes yet