Tunataka mdahalo wa wagombea urais


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 04 August 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki
Mgombea Urais kupitia CCM, Jakaya Kikwete

KATIKA nchi zilizoendelea, jambo moja dogo linaweza kuharibu kabisa nafasi ya mgombea wa nafasi ya juu ya uongozi.

Hebu chukulia mfano wa aliyekuwa mgombea wa chama cha Labour nchini Uingereza katika uchaguzi wa mwaka huu, Gordon Brown.

Kabla hajazungumza maneno yake machafu dhidi ya mwanamama mmoja wa nchi hiyo, kura za maoni zilikuwa zimeonyesha kwamba ameanza kumkaribia mpinzani wake David Cameron wa Conservative.

Lakini baada ya tukio hilo kuripotiwa katika vyombo vya habari, ghafla akaanza kuporomoka kisiasa na haikuwa ajabu kwamba alishindwa kujinasua kutoka katika kashfa hiyo na huo ndiyo ukawa mwisho wake.

Na ninakumbuka pia tukio lililotokea miaka miwili iliyopita wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Marekani kwenye mdahalo kati ya Barack Obama na John McCain.

Kabla ya mdahalo huo, Obama alikuwa amemuacha McCain kwa mbali kwenye kura za maoni. Hata hivyo, katika mdahalo huo, McCain alizungumzia juu ya mtu aliyeitwa Joe ‘The Plumber’ na ghafla chati yake ikaanza kupanda.

Joe The Plumber (Fundi bomba) alikuwa ni kiwakilisho cha wazungu wasio wasomi ambao walikuwa wameanza kuumizwa na anguko la uchumi wa nchi hiyo.

Kwa kutaja shida alizokuwa anazipata Joe, McCain akajitokeza kama mtetezi wa watu wa aina hiyo ambao ni wengi nchini Marekani. Chati yake ikapanda ghafla na ndiyo alikuja kumpa shida sana Obama mwishoni mwa kampeni.

Hata hivyo, tofauti na nchi zilizoendelea, nchi zinazoendelea kama Tanzania, matukio ya ghafla yamekuwa hayana nafasi kwenye kuamua mshindi.

Kwamba, mara nyingi, serikali iliyoko madarakani huhakikisha inashinda katika uchaguzi hata kabla siku ya upigaji kura haijafika.

Wasomi mbalimbali wa bara la Afrika, wamekuwa wakidai ya kuwa katika chaguzi za bara hili, katika mchakato mzima wa uchaguzi, jambo pekee ambalo hufanyika kwa haki ni upigaji kura.

Yaliyobaki yote huwa si huru. Serikali huwa tayari imeshinda uchaguzi “wakati wapiga kura wakienda kupiga kura.” Hii maana yake ni kwamba uchaguzi unafanyika mapema kabla ya upigaji kura.

Na ndiyo maana wengi wa viongozi wa nchi zinaoendelea huwa hawana haja ya midahalo ya kabla ya uchaguzi. Midahalo hiyo haiwezi kuongeza wala kupunguza kura kwao.

Watawala wa Uingereza walikuwa pia hawataki midahalo ingawa mwaka huu ilibidi tu Brown akubali kwa sababu ya shinikizo kubwa kutoka kwenye vyombo vya habari, asasi zisizo za kiserikali na wananchi kwa ujumla.

Hata hivyo, Uingereza walikuwa na sababu moja kubwa ya kukataa midahalo. Sababu yenyewe ni kwamba siku zote, wakati wa mdahalo, anayenufaika ni yule wa kutoka upinzani.

Yeye ndiye atakayekuwa na fursa ya kuponda sera mbaya za serikali iliyo madarakani, ambaye hatakuwa na woga wa kutoa siri yoyote ya serikali na hana la kupoteza.

Kama atashindwa uchaguzi, ataendelea kuwa mtu yuleyule lakini kwa aliye madarakani, atapoteza kila kitu kama atshindwa kwenye uchaguzi. Hii ndiyo ilikuwa hoja yao kubwa.

Na hili linaeleweka. Nchini Uingereza uchaguzi huwa huru na wa haki kuanzia siku ya kwanza. Kama mtu atachemsha kwenye midahalo, anajua watu watamuadhibu kwenye upigaji kura.

Barani Afrika, hili halifanyiki mara nyingi. Na hii ndiyo sababu nadhani tunadhani kuona mdahalo baina ya wagombea mbalimbali wa nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania baadaye mwaka huu.

Nina uhakika kwamba chochote kitakachotokea katika uchaguzi huo, hakitabadilisha chochote kwenye matokeo ya uchaguzi.

Tuhuma za wagombea ‘kuchezeana rafu’ zilianza miaka miwili iliyopita na sasa zimepamba moto katika kipindi hiki cha uchaguzi wenyewe.

Kuna taarifa kuwa viko vyama ambavyo vimeanza kununua haki za watu za kupiga kura, kuna walioandikishwa zaidi ya mara moja kupiga kura na waliowekewa pingamizi wasiandikishwe wakati wana sifa zote.

Na kuna ukweli mwingine unaouma zaidi kuhusu chaguzi za Tanzania. Kuna uwezekano mkubwa kwamba mamilioni ya watu hawatakwenda kupiga kura.

Mwaka 2005, zaidi ya watanzania milioni tano waliojiandikisha hawakupiga kura. Kumbuka kuwa wakati huo watu wengi sana walitaka kumpigia kura aliyekuwa mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete.

Baada ya uchaguzi huo, hali ikawa mbaya kwenye chaguzi ndogo. Katika uchaguzi mdogo wa Mbeya Vijijini, pungufu ya asilimia 40 ya waliojiandikisha ndiyo waliopiga kura.

Kwamba katika kila watu 10 waliojiandikisha kupiga kura, pungufu ya watu wanne ndiyo waliokwenda kupiga kura. Na hakuna yeyote ndani ya serikali aliyeonekana kuguswa na hilo.

Kama huu ndio ukweli na si matukio ya makusudi yaliyopangwa ili kusaidia kuvuruga uchaguzi, sina imani ya kwamba Watanzania watajitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba mwaka huu.

Ndiyo maana mimi ni miongoni mwa wale wanaoomba fursa ya kuona mdahalo baina ya wagombea wa vyama vikubwa Tanzania – CCM, CUF na CHADEMA.

Mdahalo huo utatupa nafasi ya kuwaona na kuwapima wale wanaotaka kupewa fursa ya kuiongoza nchi yetu miaka mitano ijayo.

Ninataka kuona uwezo wa wagombea katika kujenga hoja na si kupiga prorojo. Ninataka kuona watoto na vijana wa leo wanajifunza kutokana na mdahalo au hata midahalo ya wagombea.

Kama hili litafanyika, Kikwete, Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), wataichangamkia fursa ya kutoa elimu ya uraia ya aina yake kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Watakuwa wamejenga utaratibu mzuri kwa wagombea wajao kwamba wajue ufundi wa kushindana kwa hoja na si kupigana. Wapate fursa ya kushindana kwenye jukwaa moja angalau mara moja.

Kuna ushahidi kwamba umoja wa wagombea kwenye mdahalo ni miongoni mwa mambo yanayochangia umoja wa kitaifa. Kama leo mtoto akiona Kikwete, Slaa na Lipumba wanakumbatiana baada ya mdahalo atajifunza kuwa siasa si ugomvi. Hili ni funzo kubwa.

Sasa itokee taasisi na kutangaza fursa ya kuwepo mdahalo kwa wagombea urais mwaka huu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: