Tunataka utulivu Busanda


editor's picture

Na editor - Imechapwa 19 May 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

JUMAPILI hii wananchi katika jimbo la Busanda, Geita, mkoani Mwanza, wanafanya uamuzi. Wanachagua mbunge wao.

Mazingira haya yanahitaji utulivu wa akili ili waweze kuchambua kauli za wengi na kuona nani anafaa kuwaongoza. Lakini utulivu uko wapi?

Kwa wiki ya pili sasa serikali imekuwa ikitangaza kuwa inaongeza idadi ya polisi katika jimbo hilo. Hivi polisi wanakwenda kufanya nini Busanda? Hivi wao wako chama gani?

Uwanja wa Busanda ni uwanja wa siasa. Hauhitaji fimbo, bunduki wala matumizi ya mabavu. Lakini ni viongozi wa Chama Cha Mapinduzi ambao, baada ya kuona huenda “mambo hayatakwenda sawa,” walililia serikali kumwaga askari zaidi.

Tunarudia kusema, zoezi la kusikiliza sera na kufanya uchaguzi ni la kiraia lisilohitaji maelfu ya polisi. Mikutano ya wanasiasa haihitaji polisi wengi kama inavyoonekana Busanda. Lakini hii ndiyo tabia ya utawala usiotaka kuona watu wake wanatumia haki yao kwa uhuru na kwa utulivu.

Kumwaga askari wengi kwenye uwanja wa siasa ni kuchokoza wananchi. Na askari wakikosa kazi waweza kuwachokoza raia au kuchukua hatua hata kwa mambo ambayo yasingeripotiwa kwa mjumbe wa nyumba kumi.

Lakini ndivyo Watanzania walivyozoeshwa kwa muda sasa, tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi. Tumekuwa tukishuhudia askari wengi wakati wa kampeni za uchaguzi na wakati wa upigaji kura; utadhani nchi imeingia katika vita.

Mazoea ya kuonewa na kudhulumiwa yanazaa mazoea ya kujiandaa kupinga kuonewa na dhuluma. Na katika Busanda wananchi wana uzoefu wa kuvumilia kwa muda mrefu.

Hivi majuzi walitukanwa na Waziri wa habari, George Mkuchika kuwa hawana hata senti ya kununua gazeti wala televisheni. Waziri alikosea. Wananchi wenyewe wanajua hali yao hiyo kuliko yeye. Hoja inakuja hivi: Nani amewafikisha hapo?

Ni juzi pia walitukanwa na Waziri wa Nishati na madini, William Ngeleja. Aliwaambia kuwa wachague CCM kwa vile serikali itawaletea umeme. Serikali inataka kuleta umeme baada ya kifo cha mbunge.

Hii yaweza kuwa na maana kwamba wawe wanafiwa mbunge ndipo wapate umeme, leseni za kuchimba madini na maji ya bomba. Haya nayo ni matusi.

Ni matusi ya aina hii ambayo huleta ghadhabu na hasira kiasi cha wananchi kutoogopa hata polisi. Lakini CCM inaita askari wengi kwa kuwa inajua inakwenda kutukana wananchi; inataka wawape ulinzi.

Tunasema polisi washike silaha zao na wakae mbali na siasa na vishawishi vingine. Wawaache wananchi watimize jukumu lao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: