Tunataka watu huru


editor's picture

Na editor - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version

VIONGOZI wa Serikali wakitaka wanaweza kujidanganya. Ila hawana haki ya kudanganya umma.

Kila tukifuatilia mtiririko wa matukio tangu madaktari walipotangaza mgomo, zaidi ya wiki mbili sasa, tunazidi kujiridhisha kuwa hakuna uchunguzi imara unaofanywa na serikali kuhusiana na kutekwa na kuteswa kwa Dk. Steven Ulimboka.

Ufuatiliaji wetu umezidi kugundua kuwa watu waliopanga na kutekeleza utekaji na utesaji wa Dk. Ulimboka, ni watumishi wa serikali.

Daktari huyu anataja mtu aliyemuita eneo alipotekwa, kuwa ni mtumishi wa Ikulu.

Tena, analalamika waliomtesa walimtisha kwa maneno mabaya yakiwemo, “aga kabisa ndugu zako maana hutarudi.”

Kweli ni kudra ya muumba tu kupona. Walipomuachia wakidhani wamemmaliza, alijikuta akivuja damu mwili mzima. Anasema watekaji wake walikusudia kumtoa roho.

Hali hiyo, pamoja na mbinu zilizotumika kukwamisha msafara wa kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu, yanaongeza nguvu ya hoja kuwa watu walioandaa na kutekeleza utesaji huo ni watu wenye utaalamu wa kijeshi.

Basi ipo haki kwa madaktari na watetezi wa haki za binadamu kupinga uchunguzi wa serikali. Kwa vigezo vyote, hauwezi kuaminika.

Tunaungana na wote hao kuitaka serikali iache kudanganya umma. Itekeleze wajibu wake kwa ukweli. Vinginevyo inajisumbua bure.

Hivi tatizo liko wapi serikali kuunda tume ya watu huru ili kuchunguza tukio hilo iwapo viongozi wakuu wana hakika hawakuagiza mpango huo?

Labda wamesahau. Mwaka 2006, muda mfupi baada ya Rais Jakaya Kikwete kushika madaraka, alimteua Jaji Mussa Kipenka kuongoza uchunguzi wa mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini wa Mahenge, mkoani Morogoro na dereva wao mkazi wa Dar es Salaam.

Uamuzi wa Rais ulitokana na kujiridhisha kuwa suala hilo halikushughulikiwa ipasavyo kabla. Sasa ukichwa ngumu wa serikali yake, hausaidii kitu isipokuwa ni kujisumbua na kuzidi kujiumiza.

0
No votes yet