Tunatamani makubwa, lakini hatuyawezi


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 05 May 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

TUNAWEZA kusema kuwa tumepata bahati ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa kujadili hali Uchumi Duniani (World Economic Forum) unaofanyika kwa siku tatu nchini. Mkutano unaanza leo Jumatano hadi Ijumaa.

Hii ni mara ya kwanza kwa wajumbe wa mkutano huo kukutana katika ukanda wa Afrika Mashariki tangu ulipoanza miaka 20 iliyopita. Mara ya mwisho mkutano ulifanyika mjini Cape Town nchini Afrika Kusini.

Mkutano huu ni fursa nzuri ya kupandisha nchi kwenye uwekezaji; unaweza kutumika kutangaza maeneo ya uwekezaji ili kuinua uchumi wa nchi. Uwekezaji waweza kuwa kwenye kilimo, viwanda, madini, utalii na kila eneo ambalo linaweza kusisimua uchumi ambao kasi ya ukuaji wake haitii moyo sana katika siku za hivi karibuni.

Wananchi watashuhudia misururu mingi ya magari ya viongozi wa nchi zitakazoshiriki akiwemo Jacob Zuma (Afrika Kusini), Paul Kagame (Rwanda ), Armando Guebuza (Msumbiji), Boni Yayi ( Gabon ) na wengineo. Watakuwamo hata mawaziri wakuu, kama Morgan Tsvangirai ( Zimbabwe ) na Raila Amolo Odinga ( Kenya ).

Kimsingi mikutano kama hii ni fursa nzuri ya kutangaza nchi, lakini pia ni nafasi ya kujiweka kwenye harakati za kuonyesha kwamba kama taifa tupo na tuna nguvu hizi na zile katika kushiriki kwenye uchumi wa kikanda na dunia kwa ujumla wake.

Kwa maana hiyo, Tanzania taifa lenye historia ya kushiriki harakati nyingi duniani hasa ukombozi wa Afrika, mkutano huu ni kielelezo kingine kwamba baada ya kukamilisha ile kazi ya ukombozi sasa tunajielekeza kwenye harakati za kiuchumi. Hii ni nia njema.

Kilichobakia ni kujiuliza ni kwa kiwango gani basi kama taifa tumejipanga ili kupata faida za mkutano huu; ni kwa jinsi gani wananchi watanufaika na mkutano huu na hivyo kusahau adha ya kufungwa kwa barabara mbalimbali jijini Dar es Salaam kwa saa kadhaa katika muda huo wa siku tatu.

Pamoja na kuunga mkono mkutano huu na kwa kweli kuichagiza serikali kuchangamkia mikutano mingine kama hii, ni muhimu kuangalia maandalizi katika kufanikisha mikutano kama hii.

Nitatoa mifano michache: Nimepokea ujumbe kwa njia ya barua pepe kutoka kwa mtu mmoja akihoji kitu alichoona kinafanyika katikati ya barabara ya Sam Nujoma. Mwandishi wa ujumbe huo alihoji inakuwaje mitende (palm) mikubwa ambayo imefikia ukomo wa kukua inan’golewa huko ilikokuwa na kuja kupandikizwa kwenye barabara hiyo wakati wa saa za majeruhi?

Kwani mkutano huu ni suala la dharura? Je, haukujulikana kwa muda mrefu ungefanyika nchini? Sasa kwa nini serikali inafanya haya saa za majeruhi?

Ingawa unaweza kuyachukuliwa kwa wepesi maswali ya ujumbe huu wa barua pepe, ukweli ni kwamba harakati hizi za barabarani ambazo binafsi nimezishuhudia kwa mapana zaidi ya barabara ya Sam Nujoma ambayo crini (crane) zimekuwa zikitumika kupanda miti mikubwa na iliyozeeka tayari, zinatoa ujumbe mkubwa.

Ukitembelea barabara ya Ocean kuanzia makutano ya Ali Hassan Mwinyi hadi unapofika makutano na Lithuli, kupitia Lithuli hadi ilipo Mahakama Kuu kitengo cha Biashara, utagundua pia kuwepo kwa harakati nyingi barabarani. Hizi ni pamoja na kuziba mashimo, kufagia na kukwangua mchanga ulioachwa miaka na miaka kumeza sehemu barabara hiyo kana kwamba taifa hili lilikuwa vitani.

Lakini kilichonishutua zaidi ni kuona kwamba eneo linalojaa maji mwaka hadi mwaka kila mvua inaponyesha na kuwa kero kubwa kwa watumiaji wa barabara, hatua chache tu kutoka makutano ya barabara Ocean na Ali Hassan Mwinyi, ni kushughulikiwa kisayansi.

Mtaro mkubwa wa maji taka umejengwa na juzi jioni wakati napita barabara hiyo, kulikwa na greda lilikuwa kazini kuziba na kusawazisha eneo la barabara hiyo katika eneo hilo ambalo halijawahi kurabatiwa tangu zama za Nabii Mussa.

Katika barabara ya Sam Nujoma nako eneo la Mwenge ambako suala la kusafisha barabara hiyo mpya iliyojengwa hivi karibuni tu lilikuwa limesahaulika, kundi kubwa la akina mama wenye mafagio na mabeleshi walikuwa kazini wakiitakatisha.

Ni kweli wahenga walisema mgeni njoo mwenyeji apone, lakini kila nikitazama harakati hizi barabarani ambazo zinafanywa kwa mwendo wa askari wa kuzima moto, najiuliza tena na tena haya yote hatukuyajua hadi tukimbizane saa za majeruhi?

Kama haya mepesi, yaani kufagia, kuzima mashimo, kupanda maua, kuwagilia maji, kufunga taa za barabarani tunafanya kwa mwendo huu wa zima moto, hivi yale magumu ya kimkakati kama vile kuitangaza nchi, kutayarisha miradi ambayo tutawashawishi wawekezaji, tumejipanga vizuri kiasi gani?

Nina wasiwasi kwamba mkutano huu utafanyika kama ambavyo umekwisha kuanza, watu wetu watapata tabu ya msongamano wa magari kwa sababu ya kufungwa kwa baadhi ya barabara, lakini hawatanufaika kwa lolote na uwekezaji unaotarajiwa kwa kwa sababu hatutajipanga.

Kwa jinsi nilivyoona hizi harakati za kusafisha barabara na kupanda miti mizima mizima tena iliyozeeka, ni sawa kabisa na zile harakati za watoto wadogo wa shule ya msingi ambao wanajishughulisha na mchezo, hawasomi na wala hawana habari na kitabu, lakini wakisikia mwalimu anakuja, kila mmoja huchukua kitabu na kujifanya alikuwa makini kujisomea.

Sasa nashindwa kuelewa kuwa taifa hili limeamua kujigeuka mtoto mdogo wa shule asiyeelewa maana na umuhimu wa kujipanga, kiasi cha kuanza kukimbizana na harakati za aibu kabisa saa za majeruhi.

Kwa maandalizi haya na kwa tabia zetu nachelea kusema kwamba World Economic Forum itafanyika, viongozi wa mataifa haya na washiriki wengine watarejea kwao, lakini sisi tutabaki tu na historia kwamba tuliandaa mkutano bila kunufaika lolote katika uwekezaji.

Tatizo letu ni lile lile la miaka yote, watu wasiojali kujiandaa, wasiotaka kuwa makini na kila wakati tukichukulia mambo kwa wepesi tu. Matokeo yake taifa linazidi kupitwa na majirani zake katika mizani ya maendeleo. Tunahitaji viongozi waliopo madarakani wabadilike sasa. Vinginevyo, taifa hili litaendelea kuwa msindikizaji.

0
No votes yet