Tundu la Mkapa jembamba


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 28 January 2009

Printer-friendly version
Tafakuri

UTATA juu ya mmiliki wa mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya ambao umekuwa ukihusishwa na rais mstaafu Benjamin Mkapa,  unakaribia kutatuliwa.

Nyaraka ambazo Mtendaji Mkuu wa Kiwira Coal and Power Limited (KCP), Francis Tabaro, amekabidhi bunge zinaonyesha Kiwira inamilikiwa na watu wa karibu na Mkapa.

Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, ilikuwa Kiwira tarehe 16 Januari 2009 katika hatua ya kutaka kujua usahihi wa mmiliki wa mgodi huo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mtoto wa kuzaa wa Benjamin Mkapa, Nick (Nicholas) Mkapa na mkewe Foster Mkapa, ndio wametajwa kuwa wamiliki wa kampuni ya Fosnik Enterprises, moja ya makampuni yanayomiliki mgodi.

Mkurugenzi mwingine ambaye pia ni mmiliki ametajwa kuwa ni D. Mahembe.

Kampuni ya Mkapa ni miongoni mwa makampuni manne yaliyoungana na “kumilikishwa” mgodi wa Kiwira ambao ulikuwa mali ya serikali kwa asilimia 100. KCP ilianzishwa Julai 2005.

Taarifa hizi zimekuja wakati Mkapa akiwa tayari amewaambia wananchi kijijini kwao kuwa wapuuze tuhuma dhidi yake.

Mkapa alikana kumiliki Kiwira wakati alipoongea na wakazi wa Lupaso, wilayani Masasi, mkoa wa Mtwara, mwishoni mwa mwaka jana.

“Wapuuzeni waandishi wa habari na magazeti yakija huku yachaneni. Ni uwongo, uwongo mtupu. Sina mali. Sina pesa. Naishi kwa pensheni,” alisema Mkapa kwa sauti ya ukali.

Kampuni nyingine ni Choice Industries, ambayo wakurugenzi wake, ni Joe Mbuna na Goodyear Francis.

Hata hivyo, taarifa za usahihi zinasema mtoto wa rais mstaafu Mkapa ambaye ni Nicholas Mkapa, ameoa mtoto wa Mbuna. Hapa kuna muungano wa makampuni na familia.

Kampuni nyingine iliyoko kwenye miliki ya Kiwira ni Devconsult Limited. Wakurugenzi wa kampuni hiyo wametajwa kuwa ni D. Yona na Danny Yona Jr. Daniel Yona alikuwa Waziri wa Nishati na Madini katika utawala wa Mkapa.

Ipo pia kampuni ya Universal Technologies, ambayo wakurugenzi wake walioandikishwa Wakala wa Usajili na Makampuni (BRELA), ni Wilfred Malekia na Evance Mapundi.

Uhusiano kati ya wamiliki wa Universal Technologies na familia ya Mkapa haujafahamika.

Mbali na Mkapa, mwingine aliyejitwisha mzigo wa kukana, ni Daniel Yona. Akizungumza mwaka jana na waandishi wa habari Dar es Salaam, Yona alisema, “Sihusiki na Kiwira.”

Mbali na Mkapa na Yona, utawala wa Kiwira umetoa taarifa kwa vyombo vya habari ukitaja ulichoita, “wakurugenzi wa Kiwira” lakini haukutaja wamiliki.  

Hadi hapo hakuna kinachoweza kuwaondoa Mkapa na Yona kwenye kufikiriwa au kudhaniwa au kushukiwa kuwa, ama wakurugenzi au wamiliki wa Kiwira.

Kinachosubiriwa ni ukweli utakaodhihirisha maandiko matakatifu yasemayo, kila lililofanyika mvunguni, litawekwa wazi kwenye paa la nyumba.

Mgodi wa Kiwira ni moja ya rasilimali kubwa za taifa. Imekuwa ikidaiwa kuwa Mkapa na Yona “walijimilikisha” mgodi huo kwa bei ya Sh. 700 milioni. Bei hii imetajwa kuwa ya “kutupa” kutokana na thamani halisi ya mgodi kuwa Sh. 4 bilioni.

Hata hivyo, taarifa za serikali zilizopo zinasema hata kiasi kilichoahidiwa kulipwa hakijalipwa hadi sasa. Zililipwa Sh. 70 milioni tu ambayo ni asilimia 10 ya bei ya “chee.”

Mgodi wa Kiwira una uwezo wa kuzalisha tani 3,000,000 za mkaa wa mawe kwa mwaka. Mradi ulianza mwaka 1983 na uzalishaji kuanza 11 Novemba 1998.  

Hivi sasa serikali ina asilimia 20 tu na “wawekezaji” wana asilimia 80 ya mgodi wenye uwezo wa kuzalisha umeme kwa nchi zote za Afrika Mashariki na zile za Ushirikiano wa Kiuchumi Kusini mwa Afrika (SADC).

Wakati wa utawala wa Mkapa, mradi mwingine wa mkaa wa mawe kwenye vilima vya Kabulo, Kiwira, ambao ulipewa dola 50 milioni kufanyia utafiti, nao ulibinafsishwa katika mazingira kama ya Kiwira.

Kwa taarifa zilizopo, mkopo huo wa Benki ya Dunia umesukumwa kwa serikali kuulipa wakati mgodi umeuzwa hata kabla serikali kupata mafao ya mkopo.

Kufumuka kwa taarifa hizi kunatokana na kukimbizana na taarifa mbalimbali juu ya usiri uliokuwepo wakati wa kubinafsisha mashirika na makampuni ya serikali, uliofanywa kwa kasi na mashirika mengi kuuzwa kwa bei ya kutupa.

Jina la Mkapa haliwezi kukosekana kwenye ubinafsishaji wa Kiwira kwa kuwa ndiye alikuwa rais. Vivyo hivyo jina la Yona aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini.

Lakini kinacholeta majina yao wazi katika “dili” hili ni ule usiri ulioambatana na ubinafsishaji, hadi upekuaji ulipoanza na hata kuhusisha Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.

Si hayo tu. Wakati ubinafsishaji umefanywa na kutawaliwa na ukimya, yanakutwa majina ya watoto au ndugu wa rais na waziri. Hili nalo linaongeza mashaka na kutoa mwanya kwa wananchi kujenga mashaka.

Laiti majina Mkapa na Yona yangekuwa ya watu wengine wasiohusika na rais wala waziri, kwani kuwepo kwa majina siyo lazima yawe ya familia au ukoo mmoja. Lakini Nicholas ni mtoto wa Benjamin Mkapa na Foster ni mkwewe. Nani ataita hiyo kuwa ni “bahati mbaya?”

Je, wakati Benjamin Mkapa akiwa bado madarakani, anaweza kweli kushindwa au kukataa kusaidia mtoto wake au mkwewe au kampuni yao kumilikishwa mali ya serikali?

Hapo ndipo yanazaliwa mashaka juu ya nafasi ya rais katika biashara hii na uwezekano wa yeye kushiriki kutoa mawazo, kuyarutubisha, kutumia nafasi yake kurahisisha utekelezaji na hata kuathiri bei ya raslimali.

Hayohayo ndiyo yanamkumba Yona ambaye pia, kwa nafasi yake, inawezekana alishawishi, kushauri, kuwezesha na hata kurahisisha upatikanaji wa mgodi kwa wale aliowafahamu.

Hoja hizi zinawekwa hapa kueleza kwa nini wananchi wanachekecha, wanauliza, wanasita na wakati mwingine wanalipuka na madai ya Mkapa na Yona kushiriki katika “kugawa” mgodi wa thamani kubwa tena kwa “hela ndogo.”

Wanashindwa kuelewa mantiki ya tani milioni tatu (3) za mkaa wa mawe kila mwaka (zenye thamani ya mabilioni na mabilioni ya shilingi) kuuzwa kwa Sh. 70 milioni!

Wananchi wanauliza ujasiri huu wa kugawa mali kubwa na yenye thamani kuu ulitoka wapi. Wanajaribu kuuhusisha na waliokuwa madarakani na ambao hata kwa majina wanaonyesha uhusiano na wamiliki wapya.

Hata hapa, wananchi hawajatoa hukumu. Wanalilia mali na utajiri wa nchi yao na wanasikitika kwa nini, katika hili, imelazimu hata Kamati ya Bunge kuingilia.

Haya ni mambo yanayoweza kudadisiwa na serikali iliyoko madarakani. Wala hayahitaji uamuzi wa mahakama wala kuuliza bunge.

Eliezer Feleshi, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, kwa kuongozwa na misingi ya utawala bora, aweza kugundua kuwa kuna kilichofanywa nje ya kazi rasmi za rais na waziri.

Na hapo hoja ya kumshitaki rais na waziri isingeleta utata. Hakuna kinga inayohitajika kuondolewa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: