Tuombe viongozi wapate hekima


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 25 July 2012

Printer-friendly version

TUFUMBE macho tuombe! Ewe Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema sema nasi saa hizi na utuambie nini hiki kilichoifunika nchi yetu!

Maafa ya kutisha yanayoleta simanzi juu ya uso wa nchi; manung’uniko ya kuumiza mioyo; unyama unatendwa na wakubwa wetu wenyewe dhidi yetu, na waliopaswa kututetea wanatughilibu.

Eeh, Bwana, tulipofikishwa na awamu ya nne pagumu. Watawala wetu wanakaidi kuwasikiliza hata watumishi wa Mungu! Basi Bwana na useme nasi ili nchi ipate kujua siku ya kujiliwa kwake.

Watawala wanasema hawawezi kusema na madaktari kupitia watu wengine. Lakini wenyewe wamesema na madaktari  kupitia mahakama. Hivi Baba mahakama siyo watu wengine? Au tuseme mahakama iko mfukoni mwao?

Eeh Bwana, watawala wanachochea uasi kwa upuuzi na kutokujitambua  uwezo wao.

Tunajua nchi inapojaliwa neema na ustawi wa watu, sifa humwendea mkuu wa nchi. Pia majanga yanapolikabili taifa, lawama na chuki vyote huelekezwa kwa mkuu wa nchi.

Ndiyo maana, hata watu wasiojulikana, walioutenda unyama wa kutisha dhidi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka, lawama zote zinaelekezwa kwa rais mpaka hapo watakapokamatwa wahalifu hao.

Baba, mpe nguvu na moyo wa ujasiri mkuu wa nchi akubali rai ya wananchi kwamba aunde tume huru ili ajiweke kando na shutuma hizi.

Wanaomshauri kukataa kuunda tume huru wanataka wananchi waendelee kuelekeza shutuma kwa mkuu wa nchi ukatili huu uonekane ni maagizo yake.

Wanataka siku ya siku aje asutwe, ahukumiwe. Wanajua yeye ndiye aliyekabidhiwa nchi na wananchi kupitia sanduku la kura. Hao wengine wote wanaomzunguka ni wateule wake tu.

Ni sheria ya maumbile duniani kote kuwa viongozi wakijaa udhalimu hutapatapa. Watawashika hata vichaa, badala ya kuwapeleka hospitalini Mirembe wakatibiwe, wao wanawapeleka mahakamani. Uongozi ukishafikia hapo, Baba, huo unakuwa utimilifu wa nyakati.

Duniani kote udhalimu hulipwa kwa udhalimu! Tawala zote zilizoendesha nchi kwa udhalimu zilianguka kwa maana andiko linasema, “Atawalaye kwa upanga, atakufa kwa upanga.”

Baba, umetujalia kuingia katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, tunaomba viongozi wetu wa dini zote, wasinawe mikono yao wakafanana na Pilato aliyenawa mikono akaacha Yesu Kristo ateswe bila hatia, bali warudi tena Ikulu waombe kumwona mkuu wa nchi ili kupunguza idadi ya vifo ambavyo sasa imeongezeka hospitalini. Mgomo baridi unachukua maisha ya watu wengi.

Pale Ikulu wapo waumini wanaokujua wewe Baba na kukusujudia, ingawa, kama ilivyo kila mahali watumishi wa shetani hawakosekani.

Eee Baba, mpe rais wetu moyo wa huruma akubali kukutana na watumishi wa Mungu, ili kwa pamoja, wajadili namna njema ya kumaliza janga hili linaloutesa na kuchukua roho za wasio na hatia.

Kitendo cha rais wetu kuendelea kuwa na moyo mgumu katika hili ni kujitafutia machukizo mbele za uso wako, Baba.

Waliomteka na kumtesa Dk. Ulimboka wametenda dhambi kubwa, stahili yao wewe Baba unaijua. Shingo zao haziwezi kuukwepa upanga wako!

Kwa hili, wenyewe wanajitambua kuwa hawana amani kabisa katika mioyo yao. Nafsi zao zimejaa hofu. Kiburi chao kinawafanya wajione wababe kumbe wanajielekeza kwenye maangamizi. Nani ataishi milele? Ubabe wao ni ujinga wa kitambo tu!

Wananchi wamebaki kupotoshwa tu. Kila wanalogusa wanaambiwa kikasuku tu kuwa suala liko mahakamani. Viongozi wetu watueleze maana ya uhuru wa mahakama ni kitu gani? Wanaposema suala hili liko mahakamani hatupaswi kuliongelea wana maana gani? Kinachokatazwa hasa zaidi ni nini na kwa faida ya nani?

Hivi unyama aliofanyiwa Dk Ulimboka nao uko mahakamani? Sawa, tunakubali lakini majibu ya suala liko mahakamani kisiwe kisingizio tena.

Baba, viongozi wetu wanakera. Mahakama ilipozuia mjadala wa Dowans, wao hawakuheshimu wakaiuza kwa Symbion Power; wabunge walipoomba mgomo wa madaktari ujadiliwe, wakasema suala liko mahakamani lakini bila kujali kesi, serikali ikawafukuza.

Hivi sasa wanazuia suala la Dk. Ulimboka lisijadiliwe eti mtu anayesadikiwa kichaa amekamatwa na kufikishwa kortini kwa madai alihusika kumteka na kumtesa.

Baba, viongozi wetu wamezuia hata wabunge wetu kujadili janga la meli ya Skageti iliyozama karibu na kisiwa cha Chumbe, Zanzibar! Wanaficha nini kwa kusingizia mahakama?

Sasa ulimwengu umejua kuwa kumbe hata Tanzania kunaweza kufanyika unyama kama huu – majanga yanatokea watu wanazuiwa kujadili, watu wanauawa wabunge wanazuiwa kwa kisingizio cha kesi iko kortini.

Kudadisi kilichomsibu Dk. Ulimboka kunamdhuru vipi hakimu aliye mwema? Tuseme wazi kuwa wamefanya ukatili kushinda wanyama ingawa kwa lengo walilokuwa nalo kazi ile hawakuikamilisha. Sasa wanahaha kuzuia udadisi!

Baba jibu la “Suala hili liko mahakamani” ni sentensi inayotumiwa na viongozi wote wasiokuwa na uwezo wa kufikiri. Kwa ufinyu wao wa mawazo na kwa kujua kuwa hawana uwezo wa kutetea hoja, wanadhani sentensi ya kipuuzi kama hiyo inawapa kinga.

Wanaokufa hospitalini siyo madaktari na wanaoteseka kwa kukosa matibabu ni wananchi maskini! Mgomo wa madaktari utamalizwa kwa hekima kama aliyokuwa nayo mfalme Suleiman.

Baba, wape viongozi wetu akili ya kutambua kuwa ujemadari, ujivuni na ubabe vyote hupita kama upepo. Walikuwapo wafalme waliokuwa na mamlaka na majeshi yenye nguvu kupindukia; walikuwepo watawala walioitawala dunia kwa upanga wa moto, lakini leo wako wapi? Hawako tena, wamekwishapita tena wengine kwa aibu. Na watesi wa Dk. Ulimboka nao watapita.

Walikuwako masultani waliofanya kila aina ya ufirauni, wao wakiuita starehe! Je, leo wako wapi? Hawako tena! Wamekwisha pita! Na watesi wa Dk. Ulimboka nao watapita!

Sote tuimbe wimbo huu:

Ee Bwana wangu, nichunguze mimi
Maana wajua na kuketi kwangu.

Umenichunguza kutokea mbali,
Umepepeta kutembea kwangu.

Nipate kujua siku ya kujiliwa kwangu,
Pale utakaposhuka mlima wa Mizeituni ili kuwakusanya mataifa yote
Pale kwenye bonde la Hamagedon kwa ajili ya vita…

0713 334239
0
No votes yet