Tuombee ubindamu 2012


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 04 January 2012

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

BINADAMU hata awe na sura au umbile zuri kiasi gani yuko kundi moja na simba, chui, ng’ombe, fisi, punda na wengineo.

Hata hivyo, wanasayansi na wanafalsafa wanasema wanyama wengine wote ni hayawani ila binadamu ni mnyama aliyeendelea. Kinachomtofautisha na wanyama wengine ni akili.

Kwa kutumia akili binadamu ametengeneza mazingira mazuri ya kuishi; ameweka sheria, kanuni, mikataba, mipaka na ametengeneza jamii. Lakini anapotumia vibaya akili yake naye hurudi katika hulka ya mnyama hayawani.

Ndiyo maana katika jamii utasikia, “Kiongozi/ mzee yule hana ubinadamu” au “Huu ni unyama” au “Usiku yule ni mnyama” au “Ameuawa kinyama.” Hii ina maana matendo yao yanawaondolea ubinadamu.

Baadhi ya viongozi walifanya matendo yaliyowaondolea ubinadamu mwaka 2011 wakaonekana katika hulka ya unyama wao.

Tarehe 5 Januari 2011 viongozi wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) walifungua mwaka kwa kutoa amri za kihayawani. Waliamrisha polisi kuzuia kwa risasi za moto maandamano ya amani ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mjini Arusha. Matokeo yake wakaua watatu na wakajeruhi makumi.

Mara serikali ikatangaza na kusimamia bomoa bomoa ya nyumba zilizojengwa karibu na barabara bila fidia. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akaingiwa na ubinadamu akasema wasiostahili fidia ni wale waliojenga nyumba kuifuata barabara.

Wakati Bunge la Bajeti likiendelea, polisi waliwakamata Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Magdalena Sakaya na wenzake kumi kwa madai walizusha vurugu katika kata ya Usinge wakati wa ukamatwaji wa mifugo ya wafugaji wa Urambo wanaodaiwa kufanya shughuli zao katika eneo la hifadhi ya taifa.

Serikali ikafungua kesi dhidi ya Sakaya na wenzake katika Mahakama ya Wilaya ya Urambo wakidaiwa kusababisha mkusanyiko, kupiga polisi mawe, kutaka kunyang’anya silaha, kujeruhi polisi na kukataa kutoa taarifa polisi.

Wakiwa mahabusu bila chakula waliomba ruhusa polisi awaruhusu waende kula nje ya mahabusu hayo lakini askari huyo akahoji kwa dharau; “Hivi hamjafa tu?”

Walipofikishwa mahakamani, hati zao za dhamana zikakaguliwa zikaonekana hazina matatizo, lakini katika hali ya kushangaza Hakimu aliwanyima dhamana. Sakaya na wenzake wakakaa rumande wiki mbili tena siku ya kwanza wakiwa ‘selo’ moja na wanaume.

Mei mwaka 2011, polisi waliua watu watano katika mgodi wa dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na African Barrick Gold.

Polisi wakapiga wanafunzi wa vyuo vikuu, wakabomoa nyumba za wakazi Dodoma kumpisha mwekezaji, wakatwanga wakazi wa Mbeya. Serikali ikapongeza polisi kwa kutembeza mkong’oto huo.

Mwanafalsafa Mgiriki Aristotle anasema hata kutunga sheria mbaya ni unyama. Kwa hiyo, sheria mbaya ya marekebisho ya katiba ni unyama kwani itasababisha watu kuparurana. Vilevile sheria ya kuzuia mikutano ya wapinzani tu ni unyama.

Halafu viongozi wetu wakathibitisha unyama zaidi katika mgawo wa keki ya taifa. Wakajitengenezea kanuni kuruhusu wakisafiri nje wajichotee ‘miposho mikubwa’ kuliko hata maofisa wa Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia na hata baadhi ya nchi zilizoendelea.

Ndiyo maana wanasafiri kila kukicha. Ili wasionewe gele, wakaidhinisha posho ‘nene’ kwa wabunge maana nao nchi ni yao ili wakishavimbiwa wabaki wakitazama polisi wanavyolilia posho na Sh. 100000 na walimu wakililia walipwe malimbikizo ya mishahara iliyofikia Sh. 53 bilioni.

Fedha kwa malipo ya wanasiasa zipo lakini wafanyakazi; walimu, madaktari na watumishi wengine hazipo. Huu ni uchoyo ambao ni silka ya wanyama. Tuombee ubindamu 2012.

0658 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet