Tuone kweli kampeni za kistarabu Zanzibar


editor's picture

Na editor - Imechapwa 14 July 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MARA baada ya Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu ujao, alitoa hotuba fupi ya kutia moyo.

Dk. Shein, ambaye hapendi makundi, alisema wakati wa kampeni za uchaguzi huo wa Oktoba mwaka huu, atafanya kampeni za kistaarabu; hatamgusa mtu, hatamsengenya wala kumsema yeyote.

Mgombea huyo wa urais alisema Zanzibar inahitaji amani na utulivu wa hali ya juu kwani ni vitu muhimu kwa ustawi wa watu na maendeleo ya kisiasa, kjamii na kiuchumi.

Haya si maneno yaliyozoeleka kwa wanasiasa kutoka chama tawala—CCM (hata upinzani), hasa wanaopitishwa na chama hicho kugombea urais na nafasi za uwakilishi Zanzibar.

Kwa muda mrefu, siasa za Zanzibar zimekuwa za chuki, fitina na uhasama, hali iliyosababisha kuwepo tofauti za mtazamo kati ya wakazi wa visiwa vya Pemba na Unguja.

Wakazi wa Pemba wamekuwa wakijihisi kuwa wametengwa, hawathaminiwi kama wenzao wa Unguja. Kutokana na hisia hizo na hasa kejeli katika kampeni na dharau ukawepo mpasuko wa kisiasa kati ya Unguja na Pemba.

Ndiyo maana Pemba ikabaki kuwa ngome kuu ya upinzani huku Unguja ikifikiriwa kufaidi raslimali za taifa.

Kwa kuwa mgogoro mkubwa huanzia wakati wa kampeni na kuishia wakati wa kuhesabu kura, tunampongeza Dk. Shein kwa kutangaza kujitenga na kampeni zinazochochea uhasama katika jamii na kurejesha mshikamano wa wakazi wa visiwa hivyo.

Tunaamini kwamba Dk. Shein amejifunza mengi kutoka kwa watangulizi wake na anataka kujenga utamaduni mpya wa kushajiisha siasa za maelewano, kuthaminiana na maridhiano ambazo Wazanzibari wamechagua kuzidumisha.

Kauli hiyo inatupa imani kuwa tutashuhudia wagombea wakinadi sera za vyama vyao katika kujaribu kuwashawishi wananchi badala ya kuhubiri chuki, ambazo zimekuwa kiini cha mpasuko wa kisiasa Zanzibar.

Hatua ya maridhiano, ambao ni ushindi kwa Wazanzibari, imefikiwa baada ya pande mbili hizo, kuchoshwa na siasa zisizo na tija na baada ya wananchi wa Unguja na Pemba kujitambua kuwa ni wa moja.

Iwe CCM ilianzisha hoja ya maridhiano hayo au Chama cha Wananchi (CUF) chenye ngome Pemba kufuta masharti, mustakabali wa wananchi wa visiwa hivyo umo kwenye mikono ya wananchi wenyewe, hivyo njia aliyochagua Dk. Shein ni sahihi na inapaswa kuungwa mkono na wapenda amani, maendeleo na uelewano.

Tuone kweli kampeni za kistarabu Zanzibar ili kuziba makovu ya uhasama uliochangia miaka ya nyuma mauaji ya raia na baadhi kwenda uhamishoni. Zanzibar ni kwa Wazanzibari wote na itajengwa na Wazanzibari wenyewe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: