Turudi kwenye muungano


editor's picture

Na editor - Imechapwa 16 November 2011

Printer-friendly version

NI dhahiri sasa Tanzania inahitaji kura ya maoni ili kuamua mustakabali wa Muungano.

Tunathubutu kutamka haya kwa sababu ya hali inayotokea nchini wakati wa kuanzisha mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya itakayoridhiwa na Watanzania.

Wakati wa mjadala uliolazimika kuendeshwa baada ya bunge kukataa muswada wa awali wa sheria ya marekebisho ya katiba ya nchi Machi mwaka huu, suala la Muungano liliibuka.

Hoja ikaibuka mjadala ulipoendeshwa jijini Dar es Salaam, ukumbi wa Karimjee, na iliibuka, na hapa kwa nguvu kubwa, mjadala uliofanyika ukumbi wa Sekondari ya Haile Selasie, mjini Zanzibar.

Watoa maoni Zanzibar walitaka kwanza kutafutwe ufumbuzi wa mvutano wa muda mrefu kuhusu Muungano na kufikia kuishinikiza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iachane na muswada huo, badala yake iitishe kura ya maoni kuwauliza wananchi kama wanataka kuendelea na Muungano.

Hata mwishoni mwa wiki, pale ujumbe wa Serikali ya Muungano ulioongozwa na Samwel Sitta, ambaye ni Waziri wa Afrika Mashariki, hilo liliibuka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipotaka suala la Muungano litafutiwe ufumbuzi kwanza.

Na katika msimamo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinachoongoza kambi ya upinzani bungeni, kimesema wazi kuwa mfumo wa muungano uangaliwe upya.

CHADEMA imethubutu kwa mara ya kwanza kutaka Tanganyika irejeshwe ili washirika wawili wa muungano wawepo bila kificho kwa kuwa wanaona Zanzibar imeanza kutwaa hata isichostahiki.

Katika hali kama hiyo, na kwa sababu kilio cha wananchi kutaka serikali itatue tatizo la muda mrefu la mfumo wa muungano, hakuna tena namna ya kupuuza kilio hicho.

Katika muswada huo uliowasilishwa bungeni Jumatatu, Serikali imependekeza kuwa sasa ni ruhusa wananchi kujadili muungano, kinyume na pale awali, ila iwe ni katika kuuimarisha na siyo kutaka kubadilisha mfumo wake.

Hapa serikali inashikilia mfumo wa muungano wa serikali mbili, msimamo ambao ungekuwa sahihi iwapo haujapata kulalamikiwa. Umelalamikiwa sana.

Kwanza, kilio hicho hakikuja tu kwa bahati mbaya; kimetokana na wananchi wa upande wa Zanzibar kutoridhika na namna mamlaka ya nchi yao yalivyodhoofishwa kinyume na matarajio yao.

Wanalalamika kuwa baadhi ya mambo yanayotambuliwa kama mambo ya Muungano, yaliingizwa kinyemela kutoka yale mambo 11 yaliyotajwa na kujumuishwa katika Hati ya Makubaliano ya Muungano (Articles of Union) ambayo ndiyo msingi wa muungano.

Kwa miaka yote ya uhai wa muungano, miaka 47, serikali zote mbili zimeendelea kupuuza malalamiko ya wananchi. Hatua za sasa kupitia muswada wa katiba, zinaashiria kutaka kuzima kabisa malalamiko hayo.

Hatudhani kwamba hiyo ni sahihi. Haiwezekani kukandamiza madai ya haki ya wananchi. Ni muhimu hoja zao zisikilizwe na kuzingatiwa kwa sababu hakuna ubaya wowote kutazama upya mfumo wa muungano kama ni kweli uliasisiwa kwa ajili ya maslahi ya wananchi wa nchi zilizoungana.

Tunasema huu ndio wakati hasa serikali zetu kufanya uamuzi mgumu ili kumaliza mvutano na tunaamini ikifanya hivyo, itakuwa inaepusha balaa huko mbele twendako.

0
No votes yet