Tushiriki uchaguzi wa mitaa


editor's picture

Na editor - Imechapwa 06 October 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

HIKI ni kipindi cha uandikishaji kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kote nchini. Uchaguzi unatarajiwa kufanyika 25 Oktoba 2009.

Huu ndio uchaguzi unaotoa taswira halisi hasa ya aina ya viongozi ambao taifa linataka. Viongozi wanaojua majukumu yao, wanaojali wanaowaongoza, waadilifu na wanaoheshimu utu.

Katika kipindi hiki cha viongozi wengi waliopo madarakani kujali maslahi binafsi kuliko yale ya wananchi, hakuna shaka kwamba uchaguzi huu ni muhimu katika kuleta mabadiliko.

Tunahitaji kuondokana na viongozi wapenda rushwa, mafisadi na malimbukeni. Hilo linaweza kufanikiwa iwapo tutaweka msingi katika uchaguzi huu.

Kupata viongozi safi katika maeneo tunayoishi, ndio kunakoweza kuzalisha kupatikana kwa madiwani, wabunge na rais bora katika uchaguzi wa mwaka kesho.

Mti imara ni ule wenye mizizi imara na kutarajiwa kutoa matunda bora. Wabunge, madiwani na hata rais bora watapatikana kwa kupitia uongozi huu wa chini.

Ipo mifano ya viongozi waovu wanaoendekezwa kwa miaka mingi na Chana Cha Mapinduzi (CCM) katika mitaa. Hawa tuwakatae.

Ni vema wananchi wasitazame chama, bali nani anawafaa kuwaongoza. Ajenda iwe mtu, siyo chama.

Historia inatuonyesha kuwa vipo vyama vilivyokubuhu katika kulea maovu, lakini ndani ya vyama hivyo wapo watu wasafi wenye uwezo mzuri wa kuongoza. Hao tuwachague.

Lakini tuwakatae, tena kwa nguvu zote wale wachafu hata kama wanatokana na chama kikongwe. Maana kinachoongoza si chama, bali ni mtu. Huyo ndiye anayeamka usiku wa manane kusikiliza shida za wananchi.

Tunahimiza kila mtu kushiriki uchaguzi huu, ingawa mashaka yameanza kuwa kuna dalili za wazi za serikali kupendelea chama kilichopo madarakani.

Kwa mfano, wakati serikali inajua 2009 ni mwaka wa uchaguzi huu, imechelewa bila sababu za msingi kutoa muongozo wa uchaguzi.

Lakini ukweli ni kwamba kimekuwa katika maandalizi zamani kwani wakuu wake ndio haohao waamuzi wa muongo wa uchaguzi.

Katika mtaa mmoja wa Nyoka, eneo la Mbagala, serikali imeugawa mtaa na kuzaliwa mtaa mwingine wa Juhudi. Hapo tayari CCM imeteua wagombea wake wakati ndio kwanza inatoa taarifa kwa umma juu ya mabadiliko hayo.

Ni dalili mbaya. Lakini ni mwiko vyama vingine kususia uchaguzi. Ni kushiriki tu kwa kadri viwezavyo, maana haiwezekani kuchia chama kimoja hatimiliki ya taifa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: