Tusikubali kamwe Kagoda itushinde


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 28 January 2009

Printer-friendly version

ZIPO simulizi nyingi zinazoelezea hatari mbalimbali. Wapo wanaotumia joka hatari kama nondo mla watu; wengine hutumia mijitu ya miraba minne inayoishi mapangoni; na wengine hutumia majina ya wanyama wakali.

Haya yote yanatumika kuasa au kufunza watoto kuchukua hadhari maishani mwao. Ni simulizi za kuwatisha ili wapende uadilifu.

Inashangaza kuwa hata leo, yapo majina au vitu ambavyo vikitajwa tu huonekana ni vya kutisha kama mijitu; nondo na wanyama wakali.

Kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, moja ya makampuni 22 yaliyochota kwa njia haramu Sh. 133 bilioni kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ilioko Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ni mfano wa ninachokieleza. Inaweza kutajwa kama moja ya vitu vya kuogofya.

Katika kashfa ya aina yake kwa serikali, imethibitishwa na maodita wa Ernst & Young kuwa Kagoda ilichota Sh. 40 bilioni (Dola 30.8 milioni); kiasi ambacho ni asilimia 30 ya fedha zote zilizoibwa EPA.

Wengi wanaona Kagoda ndiyo kampuni asisi ya ufisadi huu na wala muono huo si kwa bahati mbaya, bali ni kwa vile ilivyojipanga ikafanikisha uchotaji huo huku ikimwingiza mtegoni Gavana wa BoT wakati huo, Daudi Ballali.

Si hivyo tu. Ilimvuta ndani aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, mwanamke wa kwanza kushika wizara hiyo tangu uhuru. Na kikubwa kuliko yote, ni namna viongozi serikalini walivyoshindwa kuwa na ujasiri wa kuieleza vizuri Kagoda.

Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, mfanyabiashara aliyethubutu kusimamia kwa dhati mapambano ya ufisadi ili kumsaidia Rais Jakaya Kikwete katika azma ya kukomesha ufisadi, ameuliza: Huyu mdudu Kagoda hasa ni nani?”

Mengi angali anashangaa imekuaje hasa serikali haijathubutu kueleza kwa ufasaha taarifa muhimu zinazoihusu kampuni hii iliyoiba fedha nyingi za umma?

Kwa hakika, viongozi wote serikalini wanakosa amani wakiulizwa chochote kuhusu Kagoda inayojitokeza mfano wa jini linalotafuta damu. Inapotajwa tu, kila mmoja hunywea na kujiona kama damu yake inasisimka kwa sababu mumiani yu karibu naye.

Nini kinasukuma Kagoda kuogopwa hivi? Sababu ni nyingi ila mbili ni dhahiri; ya kwanza: Kagoda ni dhambi mbaya iliyotendwa na baadhi ya watendaji serikalini kwa kushirikiana na wafanyabiashara na kwa maana hiyo wapo wengine wasiotaka kabisa kukaribia dhambi hiyo. Lakini ya pili inayoogofya zaidi ni kwamba imethibitishwa dhambi hiyo ni mbaya maana imeathiri baadhi ya watu waliokuwa na madaraka.

Kagoda inahusika sana katika sababu zilizomtoa roho Ballali; pia ina mkono katika sababu za Meghji kutoteuliwa tena Waziri wa Fedha na pengine popote baada ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa Februari mwaka jana serikali ilipoanguka kwa kujiuzulu Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

Lakini Kagoda ndiyo chimbuko la sakata lote la EPA maana baada ya maodita wa Deloitte & Touche kung’amua ufisadi wao na baadaye Ballali akaamua kudanganya na tena kuvunja mkataba nao, ndiyo mambo yote maovu yakaibuka kuhusu wizi ndani ya BoT.

Ni Kagoda hiyohiyo ilimsukuma Waziri Meghji kuandika barua ya uongo – na akaifuta huku akijitetea kuwa alidanganywa na Ballali baada ya kubaini ameingia mtegoni – kwa Deloitte. Kwanini Kagoda isitishie wakubwa na kukwepwa na watumaini madaraka milele!

Sasa kama huu ndio ukweli wa Kagoda na kwa kuwa viongozi hawataki kufungamanishwa nayo, ni kwa nini basi wasithubutu na kuhimiza suala lake kumalizwa haraka ili wapate kupumua?

Wiki iliyopita magazeti yaliripoti kuwa jalada la Kagoda alipelekewa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Elieza Feleshi. Baada ya kulipitia, akamrejeshea Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba.

Ripoti zikaeleza DCI anatakiwa na anafanya uchunguzi wa kuthibitisha taarifa ambazo hazijijajulikana akishirikiana na makachero wa nje.

Majibu na mbinu zote zinazotumiwa na vyombo vya usalama kuchunguza Kagoda ni vichekesho. Kwanza wanaoogopa kuzungumzia Kagoda wanaendeleza unafiki mchana kweupe; kwa sababu wanajua wazi kilichotokea na kilitokeaje.

Maelezo na mbinu za kukwepa ukweli wa Kagoda ni mbinu tu za kupoteza muda ili Watanzania wasahau. Tatizo kwa wakubwa, ni “mbona Watanzania hawasahau?”

Lakini tukija kwa uchunguzi huu mpya, ipo shida nyingine. Hivi si kweli kwamba Sh. 40 bilioni zilichotwa BoT, na si kweli kwamba ziliingizwa benki za humuhumu nchini? Na je, si ni kweli wapo watu waliokwenda kwa miguu BoT kuchukua fedha iwe kwa hundi au zililipwa kwa mtandao na wahusika wanajulikana?

Na je, si ni kweli kwamba benki hizo zipo nchini na kwa mujibu wa sheria za nchi zinapaswa kushirikiana na vyombo vya dola kuzuia uhalifu?

Watu wanajiuliza hivi sababu ya kuikuza Kagoda ili ionekane kama kampuni yenye hadhi maalum, inayoshughulikiwa kwa hadhari kubwa kiasi cha kufanya mambo mengine ambayo wananchi wanaanza kuhoji utashi wa kuwafikisha mahakamani wezi wa Kagoda nini hasa? Analindwa nani na kwa maslahi gani; ya nani? Ya taifa au ya kikundi kidogo cha wahalifu?

Kwa nini Kagoda imeruhusiwa kutikisa serikali na nchi kiasi hiki? Mwalimu Nyerere katika hotuba zake alipata kusema “ni lazima serikali iwatishe wala rushwa.” Alisema hivi kwa sababu yupo mwehu mmoja akibwabwaja mitaani eti “ameiweka serikali mfukoni.”

Mwalimu pia alihoji huyu binadamu anayeiweka serikali mfukoni, ana mfuko mrefu kiasi gani hata kushinda nguvu za serikali? Hili ndilo swali la kujiuliza kuhusu Kagoda; inaengwaengwa, inaogopwaogopwa na kuangaliwa kama jini vile au jitu linalotisha, linaloweza kumeza watu, kila kiongozi akitajiwa Kagoda anataharuki, kwanini lakini?

Lazima serikali ikae macho na ikatae mbinu chafu zinazojengwa ili kuionyesha Kagoda jini nyonya damu. Serikali ijiepushe na mbinu zozote zinazolenga kukwamisha au kuzuia Kagoda kubanwa na wahusika wake kushitakiwa.

Na Serikali ina sifa moja; ina mkono mrefu wa kufika popote. Mbona haiutumii mkono wake kufika benki na kuchukua taarifa muhimu za vile Kagoda ilivyochota mabilioni, ilivyoyaingiza kwenye akaunti na kuzisambaza kwa wanufaikaji wengine?

Umma unataka kusikia DPP, DCI na wote wanaohusika na uchunguzi kukamilisha kazi yao ya kuchunguza na kushitaki Kagoda na washirika wake. Sasa ielezwe basi wapi uchunguzi umefikia maana hakuna uchunguzi usiokamilika.

Haipo sababu ya kutengeneza mazingira ya kuionyesha Kagoda jitu lililoshindikana, badala yake taasisi za kiuchunguzi na mashitaka ziwajibike na kuthibitisha kazi ya maodita walioitaja Kagoda ni moja ya makampuni 22 yaliyochota EPA.

Si vizuri serikali kuachia ukungu kuzidi hata umma kuamini kuwa wapo wahalifu serikali inawaogopa. Yetu ni serikali ya Watanzania wenye akili na ujuzi wa kupambanua mambo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: