Tusirudie makosa ya nyuma


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 09 June 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

MWAKA jana, mjadala mzito uliibuka nchini kutokana na hatua ya baadhi ya viongozi wa juu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kutangaza kuwa suala la mafuta si la Muungano.

Katika mjadala huo kulikuwapo na hoja mbili kubwa. Mosi, watu wa Zanzibar ni wachoyo na ndiyo maana hawataki utajiri wao kufaidi na watu wa Bara.

Hoja ya pili, na hii ilizungumzwa na Rais wa Jamhuri, Jakaya Kikwete kwamba “kwa nini tugombane wakati mafuta yenyewe bado hayagunduliwa.”

Hoja zote hizo mbili zina ukweli kiasi fulani ndani yake. Lakini nafikiri, kama taifa, tungeenda mbele zaidi ya hapo; kwenye kufikiri ni kwa vipi Tanzania itafaidika na ugunduzi wa mafuta.

Ni jambo lililo wazi kuwa nchi yetu imefanya makosa mengi katika sekta ya madini. Wakati sekta hiyo imekuwa ikiongoza kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni, mchango wake katika pato la taifa umekuwa mdogo mno.

Viongozi wa serikali zetu mbili – Muungano na Zanzibar - wangekuwa wanafanya la maana zaidi kama akili na nguvu zao wangezitoa kwenye ubishi kuhusu iwapo mafuta au gesi ni suala la Muungano, na kuzipeleka kwenye kuwaandaa wananchi kufaidika na utajiri huo.

Na kuwaandaa huko kungejibu ile hoja ya kusubiri kwanza mafuta yapatikane ndipo watu wazungumze haya mambo. Bila shaka mafuta yakipatikana, majadiliano yatakuwa magumu.

Watanzania wanatakiwa kuyazungumza haya mapema hata kabla mafuta hayajapatikana. Kama tutasubiri mafuta yapatikane kwanza ndipo tuzungumze, yale yaliyotokea kwenye dhahabu, almasi na tanzanite yatajirudia.

Kwa mfano, miongoni mwa mambo yaliyosababisha Watanzania wengi zaidi wasifaidike na utajiri wa dhahabu nchini ni ukweli kwamba makampuni ya madini yameshindwa kujiunganisha katika uchumi wa taifa.

Nitatoa mifano kidogo. Kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya Jaji Bomani, serikali imepoteza kiasi cha zaidi ya Sh. 400 bilioni kutokana na makampuni hayo ya madini kutotumia umeme wa Tanesco.
Makampuni hayo hutumia umeme wa mafuta ambayo huyaingiza nchini kwa msamaha maalumu wa kodi.

Kutokana na hilo, serikali imepoteza mapato ya kodi kwa uingizwaji wa mafuta hayo na pia ambayo yangetokana na matumizi ya umeme wa Tanesco.

Kama Tanesco ingepata fedha hizo, ingeweza kutoa umeme kwa Watanzania wengi zaidi. Umeme huo ungeongeza ajira zaidi na uchumi wa nchi yetu ungefaidi.

Na kwa mapato hayo ya Tanesco na ukuaji wa uchumi, serikali ingetumia fedha inazozitumia sasa kama ruzuku kwa Tanesco kuimarisha huduma za afya na elimu kwa Watanzania.

Jambo la pili ambalo lilisababishwa na serikali kutofanya maandalizi ya mapema kabla makampuni makubwa ya uchimbaji hayajaja nchini ni kutofanya tathmini ya mahitaji ya makampuni hayo.

Kwa mfano, serikali ingebaini mapema ni bidhaa gani ambazo wafanyakazi wa makampuni hayo, wazawa na wageni, wangependa kuzitumia na zinapatikana nchini.

Hii ingeondoa malalamiko ya sasa miongoni kwamba makampuni ya madini yanaagiza matunda na hata karatasi za usafi chooni (toilet paper) kutoka nje ya nchi wakati vitu hivyo vinapatikana nchini.

Huduma za vinywaji, vyakula, mavazi na vifaa vya maofisini kama karatasi na wino ni mambo ambayo wananchi wangeweza kuyafanya hata kwa utaratibu wa kuwa na SACCOS tu. Hauhitaji kuwa milionea kuyafanya haya.

Kama tutasubiri kwanza mafuta na gesi vipatikane kila mahali ili nasi ndipo tuanze kuyazungumza mambo haya, basi tutaanza kuwalalamikia wageni kwa kula juisi ya mananasi kutoka Afrika Kusini, huku matunda hayohayo yakiozea juani kule Lushoto, Tanga.

Kwa hiyo ni lazima tufanye tathmini ya nini hasa wananchi wetu wataweza kupata moja kwa moja kutoka kwa wawekezaji hawa hata kama hawana uwezo wa kuwekeza katika utafutaji wa mafuta.

Kwa mujibu wa Anthony Paul, kutoka taasisi ya kimataifa ya Revenue Watch Institute (RWI), nchi kama Trinidad and Tobago, zimefaidika na utajiri wa mafuta kwa utaratibu huo.

“Wananchi wanaweza kujiunga katika vikundi ambavyo vitakuwa na kazi maalumu ya kutoa bidhaa na huduma kwa makampuni ya mafuta,” alisema mwezeshaji huyo jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Mahali pengine ambapo serikali inaweza kutoa mchango mkubwa ni katika kuingia katika mikataba na makampuni ya uchimbaji wakati wa utafutaji.

Kuna tatizo lingine la kiufundi lililopo ndani ya serikali yetu katika kipindi hiki. Kuna mkanganyiko wa majukumu baina ya Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli (TPDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (EWURA).

Wakati TPDC inahusika katika utafutaji, uchimbaji na usambazaji wa mafuta, EWURA inaingia katika “udhibiti” wa nishati hiyo. Udhibiti una tafsiri pana ambayo inaingia hadi katika majukumu ya TPDC.

Akizungumza katika warsha ya siku tatu kuhusu masuala ya mafuta na gesi iliyofanyika jijini Dar es Salaam kati ya Juni 1hadi 3 mwaka huu, Mratibu wa RWI nchini, Silas Olang, alisema ili Tanzania ifaidike katika sekta ya mafuta, ni lazima majukumu ya EWURA na TPDC yawe bayana.

Jambo lingine la muhimu katika kuhakikisha Tanzania inanufaika na uchimbaji wa mafuta na gesi nchini ni kuwa na utaratibu wa kufahamu kuna wazawa kiasi gani wanaoweza kufanya kazi katika makampuni ya sekta hiyo.

Kama nchi itakuwa na kada yake ya wataalamu wanaofahamika, itakuwa rahisi kufahamu, pale uchimbaji utakapoanza, nchi ina upungufu au wingi kiasi gani kulingana na mahitaji.

Tanzania haitaweza kufaidika vya kutosha na uchimbaji wa mafuta na gesi iwapo wengi wa watakaokuwa wafanyakazi wa makampuni hayo watatoka katika nchi za jirani.

Uganda kwa mfano, Rais Yoweri Museveni wa nchi hiyo, alipeleka vijana kwenda kusoma kuhusu mambo ya uchimbaji na utafutaji wa mafuta mwanzoni mwa miaka ya 1990, na sasa vijana hao wanashirikiana na wageni katika utafutaji wa mafuta.

Wakati mafuta yatakapopatikana, Uganda itakuwa na watu wake wa kutosha kwenye uchimbaji na katika maeneo mengine ya ajira ndani ya sekta hiyo; na hili ndilo tunalolitarajia.

Binafsi, mjadala kuhusu mafuta ni suala la muungano au la naona hauna mashiko kwa sasa. Yawe ya muungano au vinginevyo, bado wananchi watahitaji kunufaika na utajiri huo na hilo ndilo la kwanza. Kufaidika.

Muungano hauleti chakula mezani. Muungano hauongezi dawa hospitali. Muungano haupunguzi foleni katika barabara zetu. Ila mapato makubwa, yatafanikisha yote hayo.

0
No votes yet