Tusitoneshe majeraha ya udini


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 23 November 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

NIMEJITOSA kujadili makala za Nyaronyo Kicheere, iliyobeba kichwa cha maneno kisemacho, “Rostam anacheza kama Pele.” Imechapishwa kwenye MwanaHALISI, 19 Oktoba 2011.

Baada ya kuisoma makala hiyo kwa makini, nimegundua jambo moja kubwa: Mwandishi anadhamira mbaya ya kuwashawishi wananchi wasahau matatizo yao ya sasa yanayoletwa na serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwamo hatua ya watawala kujitwisha mamlaka ya kujadili katiba mpya kinyume na matakwa ya umma na kushindwa kutekeleza ahadi ya kuleta “Maisha bora.”

Badala yake, anataka wananchi wajikite kwenye mjadala usio tija unaolenga kuchokonoa na kutonesha vidonda vya udini.

Swali kuu ninalojiuliza, “Nani amemtuma Kicheere kufanya kazi hii?” Kwa mfano, kwenye makala hiyo ya "Rostam anacheza kama pele," mwandishi hajaonyesha kwa mapana jinsi Rostam anavyocheza kama pele, badala yake ametumia sehemu kubwa ya andishi lake “kuwasimanga” waislam.

Katika andishi jingine, Kicheere amepotosha umma kwa makusudi kwa kutaka uwongo uonekane ukweli.

Mathalani, katika historia ya Tanzania, amesema hakuna mahali ambako wakristo wamegombea kanisa, ispokuwa mambo hayo hufanywa na waislamu tu.

Kwamba hakuna mahali Padri ama Mchungaji amedai kanisa fulani ni lake. Anasema mambo ya kugombea nyumba za ibada yako kwa waislamu tu – wao ndiyo mabingwa wa kugombea misikiti. Hili si kweli na Nyaronyo kwa upeo wake anafahamu hivyo.

Anajua kuna orodha ndefu ya viongozi wa madhehebu ya kikirsto wanaogombea makinisa, pengine kukilo wale wa kiislamu wanaogombea misikiti.

Mfano hai, anajua kilichotokea kwenye mgogoro wa Dayosisi ya Pare uliosababisha hadi muumini mmoja wa madhehebu ya kikristo kuuawa.

Katika mgogoro ambapo wananchi wa Mwanga walitaka kujitenga na Same kwa kuunda dayosisi yao.

Lakini pia anajua kwa undani mgogoro unaofukuta kwenye Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), linaloongozwa na Askofu Zacharia.

Kwa mfumo wa FGBF, Kakobe ndiyo kanisa. Ni yeye aliyelianzisha na ni yeye mwenye mamlaka ya kila kitu ndani ya kanisa hilo.

Ndivyo Jaji wa Mahakama Kuu Augustine Shangwa, alivyonukuliwa akieleza wachungaji watatu waliomfungulia kesi ya matumizi mabaya ya Sh. 14 bilioni, Askofu Kakobe.

Kimsingi hakuna muislam hata mmoja asiyejua madhila wanayopata kutoka kwa serikali hii; lakini kwa kuwa hawataki kuongeza matatizo katikati ya matatizo, wameamua kukaa kimya na kutafakari yanayolisibu taifa lao.

Waislamu wanajua kinachojiri jijini Arusha. Wanafahamu jinsi wananchi wanavyokandamizwa; wanavyoonewa na wanavyonyanyaswa na watawala wakati wa kudai haki zao.

Wanaviona vyombo vya dola na vile vya mahakama vinavyotumiwa na waliopo madarakani kwa mslahi binafsi ya kisiasa.

Wanamuona na kumsikia, mkuu wa polisi wa wilaya (OCD- Zuberi Mwombeji), akiwaita wananchi wanaodai haki zao, "mapanya."

Wanamuona na kumsikia, mkuu wa mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, jinsi mchana anavyokuwa mkuu wa mkoa, huku usiku akijivisha ukada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Jamii ya waislamu wamesikia na kushuhudia – maana nao walikuwapo – kauli alizozitoa kiongozi huyo wa mkoa kwenye mkutano wa kamati ya siasa ya CCM mkoani Arusha. Katika mkutano huo, Muongo alijigamba kuwa amefika Arusha kwa kazi moja tu: Kudhibiti upinzani.

Waislamu wameona yanayotokea Mkoani Tabora, ambako serikali imepiga mabomu mamia ya raia wake na kunyang'anya mali zao kwa kisingizio cha “uvunjifu wa sheria.”

Waislam wanajua ni jinsi gani serikali ya Tanganyika African Uniun (TANU) na baadaye CCM ilivyohujumu taasisi zao za maendeleo, ikiwemo East African Muslim Welfare Society (EAMWS), pamoja na mali nyingine kama vile, nyumba na taasisi za elimu.

Serikali ya Benjamin Mkapa ilipoamua kurudisha mali na taasisi za elimu za dini, ilirejesha za wakristo tu – zile za waislam hazikurudishwa.

Yote haya wanayajua, lakini wameama kukaa kimya; Kicheere usiwarejeshe huko.

Haya siyatoi kichwani mwangu; yametoka kichwani kwa Mwalimu Nyerere na yamethibitishwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Ni pale alipokuwa akizindua harambee ya Chuo Kikuu cha Waislam Morogoro (MU).

Kama madai haya hayana ukweli, kipi kimemgusa Mkapa hadi kuamua kutoa kilichokuwa chuo cha umma na kuwapa Waislam?  Nani asyejua kwamba kulikuwa na upendeleo maalum kwa vijana wa kikristo katika sekta ya elimu?

 Kitabu cha “Kanisa katoliki na siasa za Tanzania," kilichoandikwa na Padri Sivalon na kuchapishwa na Ndanda Mission Publisher, kinathibitisha madai haya.

Hadi Mwalimu Nyerere anafariki dunia Oktoba 1999, hakuwahi kukanusha kilichoandikwa kwenye kitabu hicho.

Wala mwandishi wake, Padri Sivalon, hakuwahi kujitokeza kukanusha. Kanisa Katoriki nalo halijakana.

Waislamu wanayajua yote haya; wanayaona na kuyashuhudia, lakini hawataki kuwa sehemu ya wale wanaotaka kuingiza nchi kwenye machafuko.

Watusi na Wahutu walifikia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe (genocide) kwa bahati mbaya. Walichochewa na viongozi waliowaita wenzao “mende;” vita vya halaiki si kwa Rwanda tu: Vyaweza kutokea hapa hapa nchini.

Wapo Watutsi na Wahutu wengi waliooana na kuzaa, lakini pale ubaguzi uliposhamiri kwa jamii moja kujiona bora kuliko nyingine – haki  kupindishwa – baadhi yao, tena wengi waliwachinja wake zao na hata mashemeji zao kutokana na tofauti ya ututsi na uhutu.

Chamsingi Kicheere anataka wananchi wasahau madhira ya serikali. Anataka kuaminisha wananchi, Tanzania ni taifa la amani wakati anaona jinsi watawala wanavyoendesha nchi kwa mabavu. Anataka tusijadili mabavu ya serikali katika kupitisha muswaada wa katiba mpya. Tusijadili mikataba ya kinyonyaji na sheria zake.

Anataka tusijadili matatizo ya maisha yanayowakabili wanannchi. Tusiseme kwamba baadhi yao hawamudu hata mlo mmoja kwa siku, huku wengine hasa wale wanaoishi mijini wanashindia mihogo ya kuchoma na pilipili ya unga.

Wengine wanashinda kwa vipande vya mahindi ya kuchoma na ndimu.

Anataka tujadili waislamu na malalamiko yao.

Waislamu wa nchi hii, tuna mambo mengi ambayo kwa umoja wetu yanarudisha nyuma maendeleo yetu.

Leo tunaambiwa serikali inatumia karibu Sh. 70 bilioni kwa mwezi kununulia mafuta mazito kwa ajili ya mitambo ya kufua umeme kutoka kampuni binafsi ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL)! Watala wanafurahia.

Waliongiza nchi katika mkataba huu wa kinyonyaji wanafahamika. Waliogawana mlungula kwa kufanikisha mkataba wanajulika. Wanaoendelea kunufaika na fedha zinazotolewa na serikali kwa kisingizio cha kununulia mafuta, wanaeleweka na watawala. Lakini wote wameachwa kana kwamba taifa hili linakufa kesho.

Hayo ndio mambo ya msingi ambayo wananchi walitarajia Kicheere angeyajadili, kuliko kujitumbukiza katika kutonesha vidonda vya udini.

Je, ametumwa? Kama ndiyo, ametumwa na nani na kwa faida ya nani? Chondechonde, tusimruhusu Kicheere kufanikisha mradi wake huu.

0
No votes yet