Tusiukubali kamwe uhuni huu wa CCM


editor's picture

Na editor - Imechapwa 25 August 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KATIKA mchakato wa kupata wagombea ubunge na udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa uchaguzi mkuu ujao, kumefanyika uhuni.

Bila sababu za msingi, baadhi ya watu waliotangaza nia na hatimaye kuomba ridhaa ya wanachama wateuliwe kuwania nafasi za ubunge na udiwani, waliondolewa kwa kigezo cha utata wa uraia.

Halafu, baada ya kila chama kumaliza utaratibu wa kupata wagombea wao, tumeshuhudia wagombea wa vyama vya upinzani wakienguliwa kwa madai ya utata wa uraia wao.

CCM ikajipa mamlaka ya Idara ya Uhamiaji, ikawekea pingamizi wagombea wa upinzani wakidaiwa si raia. Wasimamizi wa uchaguzi wa wilaya wakakubali pingamizi hizo na hatimaye wakawaengua wagombea husika.

Matokeo yake, ni kuwezesha wagombea wa CCM kubaki peke yao hivyo kupita bila ya kupingwa.

Tunajua ni jambo la wazi kwamba nchini petu wapo watu wasiokuwa raia lakini wanapata haki kama ni raia. Lakini suala hili linahitaji uchunguzi makini kulithibitisha. Hilo ni jukumu la serikali katika utendaji wake wa kila siku.

Baadhi yao walitoka Burundi, Rwanda, Waganda na Jamhuri ya Kideomkrasi ya Congo walioingia nchini tangu wakati nchi zao zikiwa kwenye harakati za ukombozi na baadaye zilipokabiliwa na machafuko. Wengi wao walirudi kwao baada ya vita kumalizika na wengine wamebaki hadi leo. Baadhi waliomba na kupewa uraia.

Lakini hata baada ya kuwa umewekwa utaratibu mzuri wa kuwabaini wageni na kuwaripoti kwenye vyombo vya serikali, kuanzia serikali za vijiji hadi serikali kuu, CCM wameamua kuwapakazia raia wema kuwa si raia kwa sababu tu hawawataki.

Mbaya zaidi ni kwamba CCM wanakataa nyaraka halali zilizotolewa na serikali inayoongozwa na chama hichohicho na kuwatuhumu watu wazima kuwa si raia.

Halafu, mgombea ubunge, kwa vile yeye ni waziri, bila ya kutoa uthibitisho, anamtaja mpinzani wake kuwa si raia. Na Wasimamizi wa Uchaguzi wanakubali.

Iko wapi haki? Hivi ndivyo CCM inavyoendesha nchi. Kiongozi akijisikia kumvua mtu uraia, anafanya hivyo na kuachia mtuhumiwa atoe vielelezo. Huu ni nini kama si uhuni?

Hatuna sababu yoyote ya kutetea wanaotuhumiwa si raia. Hatukingii kifua si wao tu bali mtu yeyote mwenye uovu. Hiyo si dhamira yetu. Tunajua Watanzania Tanzania ndio wanaostahili kufaidi raslimali tulizojaaliwa kuwa nazo.

Ardhi, nafasi za ajira na uongozi ndani ya vyama vya siasa na serikali ni kwa ajili ya wananchi wa nchi hii siyo wageni. Wengine watapata kwa kufuata sheria.

Tunaunga mkono juhudi zote za serikali kubaini wageni haramu, ila tunapinga utaratibu wa kifisadiunaotumiwa na wanasiasa wa CCM kwani unakandamiza demokrasia.

Ni matukio kama haya yanayosababisha kukosekana amani katika baadhi ya nchi. Tujiulize, waliovuliwa uraia ni raia wawapi? Serikali itawarejesha lini kwao?

Kama si raia, kwa nini walisubiriwa wakati wa kugombea nafasi za uongozi? Je, watapiga kura? Uchaguzi utahesabika kuwa halali kama wageni hao wameshiriki? Ndiyo maana tunasisitiza tusiukubali kamwe uhuni huu wa CCM.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: