Tutafikia siku kuambiwa Mwalimu Nyerere aliishi Kigamboni


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 07 December 2011

Printer-friendly version

KABLA ya kuanza safari yake ya kwenda kupandishwa kwenye kilele cha Uhuru cha Mlima Kilimanjaro, Mwenge wa Uhuru ulipitishwa kwa mbwembwe nyingi mkoani Dar es Salaam kama sehemu ya kuenzi kumbukumbu ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika.

Mwenge ulipitia wilaya zote tatu – Ilala, Kinondoni na Temeke. Ukiwa Kinondoni, ulipitishwa mtaa wa Ifunda, Magomeni, ambako Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliishi wakati wa harakati za kudai uhuru.

Katika nyumba hiyo ambayo sasa ni sehemu ya ofisi ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Mwalimu aliishi kwa miezi mitano tu ndipo akaenda Ikulu. Ila ipo nyumba ambayo ndiyo hasa aliishi na familia yake kwa miaka minne mfululizo akiendesha harakati za uhuru – mwaka 1956 mpaka 1960.

Inakuaje historia halisi inapotoshwa? Wakati hii ni wiki ya kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru, kwa kaulimbiu iliyochaguliwa ya “Tumethubutu, tumeweza na tunasonga mbele” itakuwa jambo zuri kuitunza historia na kuwapa fursa wananchi kutambua ukweli badala ya uongo.

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii kitengo cha kumbukumbu za waasisi wa taifa kuvunja nyumba ambayo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliishi kwa miaka minne.

Nyumba hiyo ipo Magomeni, Kituo cha Mabasi cha Usalama (zamani Maduka Sita) akitokea Pugu Sekondari baada ya kulazimishwa na serikali ya kikoloni kuacha kazi ya ualimu na kuanza harakati za uhuru.

Hivi ni sahihi kumuenzi baba wa taifa kwa taarifa za kubahatisha? Na ni uamuzi muafaka kupoteza moja ya kumbukumbu muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo? Au ndio kaulimbiu ya watawala wakisema “Wamethubutu, wameweza na wanasonga mbele!”

Hapana shaka ilikuwa moja ya kumbukumbu muhimu kwa taifa letu kwani Baba wa Taifa aliishi hapo kama mpangaji kabla ya kuhamia kwenye nyumba aliyoijenga, mtaa wa Ifunda, jirani na hapo Magomeni-Usalama. Serikali sasa inataka jamii ipatambue hapo ndipo panafaa kuwa kumbukumbu sahihi.

Hii si sawa. Hakuishi kwenye nyumba yake kwa zaidi ya miezi sita kwani Tanganyika ilipopewa uhuru na serikali ya kikoloni kukabidhi madaraka kwa wazalendo chini ya TANU, Mwalimu alihamia Ikulu ya Magogoni.

Kumbukumbu zinaonyesha wazi kuwa katika nyumba ambayo Baba wa Taifa aliishi kwa miaka minne, Wizara ya Maliasili na Utalii, kitengo cha kumbukumbu, iliweka bango kubwa la kujulisha umma kwamba Mwalimu Nyerere aliishi hapo wakati wa harakati za kudai uhuru.

Kwenye bango hilo kulikuwa na maneno ya Kiswahili: KUMBUKUMBU… Mwalimu Julius K. Nyerere aliishi katika nyumba hii baada ya kulazimishwa kuacha kazi ya ualimu kwa ajili ya kuongoza vita vya uhuru tangu 1956-1960.

Maneno hayo ya yalifuatwa na mengine kwa lugha ya Kiingereza: “HISTORIC MONUMENT… President Mwalimu Julius K. Nyerere Lived in this house after resigning from teaching and led the struggle for Independence from 1956-1960.”

Masikini akili za Watanzania. Nyumba hii imevunjwa. Sababu zinazotajwa ni kwamba kutekeleza mipango ya maendeleo ya eneo la Magomeni.

Kwani hayo maendeleo lazima yajengwe katika eneo hili la Magomeni-Usalama tu ambako kuna nyumba yenye historia iliyotukuka kwa taifa letu? Ukitafakari kwa kina, kuna sehemu nyingi za kujenga na kuleta maendeleo. Kinachosikitisha zaidi ni pale eneo hilo kubomolewa na kutelekezwa kwa kuzungushiwa mabati.

Kitu kinachoumiza zaidi moyo, ni taarifa za kweli kwamba eneo hilo sasa limekuwa kichaka ambacho vibaka wanatumia kama maficho.

Hata ile hadhi ya eneo lote la Maduka Sita imefutika. Inasikitisha. Kile kitengo cha kumbukumbu sasa kimeamua kuandika bango dogo kwenye nyumba ambayo Mwalimu aliijenga na hakuishi zaidi ya miezi mitano ya mtaa wa Ifunda.

Kumbukumbu zinasema eneo zima la Magomeni zamani lilijulikana kwa jina la ‘UNO’ yaani Umoja wa Mataifa kutokana na viongozi wote wa kitaifa kuwa wakiishi hapo. Mfano wa viongozi hao ni mzee Rashid Mfaume Kawawa, Oscar Kambona, mzee Saadan Abdul Kandoro ambao wote wameshafariki dunia. Hata familia ya kina mzee Sykes waliiishi hapo.

Wote hao walikuwa wanaketi na Mwalimu na kuzungumza naye wakiwa sehemu hiyo ya Maduka Sita. Ni wapi tena kumbukumbu kama hii itapatikana? Kuna uwezekano wa vizazi vijavyo kuja kuwa na taarifa kuwa Mwalimu Nyerere aliishi Kigamboni wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.

Je, tutakuja kubisha taarifa hizo? Ama kweli wamethubutu, wameweza na wanasonga mbele.

Nakumbuka wananchi kadhaa wenye uelewa wa jambo hilo walipiga kelele kulalamika. Hata hivyo, kama kawaida ya machozi ya samaki kuishia majini, hawakusikilizwa.

Hakuna aliyesikia kilio cha wananchi hao ambao walipolalamika mipango ya serikali kuvunja nyumba hiyo, waliungwa mkono na wanafamilia ya Mwalimu Nyerere kubembeleza nyumba hiyo isivunjwe. Masikini wee, “hawakusikilizwa.”

Kumbukumbu za John Speak, David Livingstone na kina Vasco da Gama, wakoloni wazungu mpaka leo zingali na hadhi ya aina yake katika maeneo walikopita – Kigoma, Bagamoyo na Ziwa Victoria.

Ni kituko tu kwamba kumbukumbu muhimu inayomhusu rais wa kwanza wa Tanganyika huru, mwasisi wa taifa letu, Mwalimu Nyerere, inatupwa. Bila shaka itafika hatua ya kuamini letu, kwamba Mwalimu aliishi Kigamboni, kabla ya kutua ikulu. Maana Kigamboni ni karibu na Magogoni-Feri.

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: