Tutaifishe mitambo ya Dowans


Tundu Lissu's picture

Na Tundu Lissu - Imechapwa 23 February 2011

Printer-friendly version

SPIKA wa Bunge la Jamhuri, Anna Makinda hakuwa na sababu zozote za msingi kukataa kusudio la kujadili bungeni hukumu ya mahakama ya kimatifa kati ya usuluhishi wa migogoro ya kibiashara (ICC) kati ya serikali na makampuni ya Dowans Holdings S.A na Dowans Tanzania Limited.

Sababu ni mbili: Kwanza, hakuna mgogoro wowote kisheria, kati ya Dowans Holdings S.A. na Dowans Tanzania Ltd., kwa upande mmoja na shirika la umeme la taifa (TANESCO) kwa upande mwingine, unaosubiri  “uamuzi” wa mahakama kuu.

Mgogoro katika ya Dowans na TANESCO uliokuwa ICC ulimalizika 15 Novemba 2010, pale mahakama ilipotoa uamuzi wake.

Kwa mujibu wa aya ya 17 ya kifungu cha 14 cha mkataba, “uamuzi wa (wa) suluhishi utakuwa wa mwisho na utawafunga wadaawa na hautakatiwa rufaa. Mdaawa yeyote anaweza kuiomba mahakama yoyote yenye mamlaka kutoa hukumu kutokana na uamuzi wa usuluhishi…”.

Kwa mujibu wa aya hiyo, Dowans na TANESCO walifuta haki zao za “kuhoji au kupinga uhalali au utekelezaji wa makubaliano ya usuluhishi au wa kesi ya usuluhishi au uamuzi uliotolewa kwa mujibu wa kifungu hiki, ikiwa ni pamoja na pingamizi inayohusu mahali pa usuluhishi au usahihi/umuafaka (wa mahakama ya usuluhishi).”

Hivyo basi, hakuna kesi yoyote iliyoko mahakama kuu inayosubiri uamuzi, bali Dowans wamesajili uamuzi wao mahakama hapo ili kukidhi mahitaji ya kisheria!

Hoja ya kutaka Bunge lijadili hukumu ya Dowans iliwasilishwa kwa katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila na David Kafulila, mbunge wa NCCR- Mageuzi, katika jimbo la Kigoma Kusini, mkoani Kigoma.

Pili, kama hoja ya Kafulila ingeruhusiwa bungeni, ni wazi ingeleta mjadala na mgogoro mkubwa wa kisiasa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake.

Hii ni kwa sababu ya kuwepo kwa hisia kwamba suala la Dowans ni mwendelezo wa Kashfa ya Richmond ambayo iliitikisa serikali ya Rais Jakaya Kikwete hadi kupelekea kujiuzulu kwa aliyekuwa waziri mkuu Edward Lowassa na waliokuwa mawaziri wa nishati na madini, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi.

Kwa sababu hiyo, kama alivyosema aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa TANESCO, Dk. Idris Rashid katika ushahidi wake kwenye mahakama ya ICC, “... wananchi walikasirishwa zaidi wakati Kamati Teule ya Bunge ilipotuhumu serikali (katika ngazi ya wizara ya Nishati na Madini na Waziri Mkuu walihusika/kushinikiza mchakato ulioipa Richmond mkataba wa kufua umeme ijapokuwa ilijulikana kuwa haikuwa na uwezo wa kifedha wa kutekeleza makataba huo.”

Dk. Rashid anasema, “Kelele ziliongezeka kutokana na ukweli kuwa jiji la Dar es Salaam pekee lilikuwa linakatiwa umeme kwa saa 12 kila siku wakati Richmond ikiwa nyuma katika utekelezaji wa mkataba.”

Kutokana na hali hiyo, kama mjadala wa Dowans ungeruhusiwa bungeni wakati huu ambapo nchi inakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa umeme, huku warithi wa Richmond wakiwa wanadai walipwe mabilioni ya shilingi, ni wazi wananchi wangepandwa na hasira kama ilivyotokea wakati wa Richmond.

Katika mazingira hayo, watawala waliona bora kuzuia mjadala wa Dowans ambao kwa vyovyote vile, bado una mvuto kwa wananchi kwa kuwa wahusika wakuu wote wa Dowans ni wale wale walioshiriki ufisadi wa Richmond.

Moja ya mambo ambayo Kamati Teule iligundua katika uchunguzi wake ni kwamba mbunge wa Igunga (CCM), Rostam Aziz ndiye aliyemtambulisha kwa Salva Rweyemamu ambaye sasa ni mkurugenzi wa mawasiliano binafsi ya rais kwa Mohamed Gire, anayedaiwa kuwa mmiliki wa Richmond.

Kamati ya Mwakyembe ilipata ushahidi wa nyaraka uliomnyooshea kidole Rostam ambapo kampuni yake ya Caspian Ltd., anuani ya posta na ya makazi ya kampuni hiyo anayomiliki na na ndugu zake wawili na baadhi ya wafanyakazi wake walikuwa pia wafanyakazi wa Richmond.

Uamuzi wa ICC umetoa mwanga zaidi kuhusu uhusika wa Rostam katika masuala ya Richmond na Dowans.

Wakati Richmond ilisajiliwa Houston, Texas, Marekani 9 Novemba 2003, Dowans Holdings ilisajiliwa nchini Costa Rica, tarehe 1 Julai 2005.

Aidha, kwa hati ya uwakili (Power of Attorney) ya 28 Novemba 2005, Dowans Holdings ilimteua Rostam Aziz kuwa mwakilishi wa kuendesha shughuli zake nje ya Costa Rica.

Kwanza, kufuatana na taarifa ya uchunguzi wa mawakili wa TANESCO juu ya Dowans, kampuni hiyo ilikuwa na mtaji wa kuanzia wa dola za Kimarekani 100, haikuwa na mali yoyote isiyohamishika wala magari yaliyosajiliwa kwa jina lake, haikuwa na cheti cha mlipa kodi nchini Costa Rica na wala haikuonekana kuwa imewahi kufanya biashara yoyote nchini humo!

Pili, ushahidi wa Henry Surtees ambaye ni mfanyakazi wa Caspian Ltd., na ambaye kati ya mwaka 2006 na 2007 alipewa hati ya uwakili wa Dowans nchini Tanzania umemuunganisha Rostam Aziz moja kwa moja na makampuni ya Richmond na Dowans.

Katika ushahidi wake, Surtees aliiambia ICC kwamba wakati Tanzania ikikabiliwa na tatizo kubwa la umeme mwaka 2006, kampuni inayomilikwa na Mohamed Al-Adawi “ambaye aliwahi kufanya kazi na waajiri wangu (Caspian Ltd.) siku za nyuma iliniomba, kwa kupitia waajiri wangu, kuangalia matokeo ya kifedha na kibiashara ya mmoja wa miradi binafsi ya ufuaji umeme iliyokuwa inaendelea…Mradi uliokuwa unazungumziwa ni ule uliokuwa ukiendeshwa na (Richmond) kutokana na mkataba wa ufufuaji wa umeme kati yake na TANESCO.”

Akimzungumzia Rostam, Bw. Surtees aliieleza mahakama ya ICC, “... Akram na Jahangir Aziz, waajiri wangu katika Caspian Ltd. wana kaka yao, Rostam Aziz ambaye kwa wakati huo alikuwa mbunge na mwanachama wa ngazi ya juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwa nafasi yake, alielewa hali halisi ya tatizo la umeme na haja kubwa ya kuhakikisha kwamba mkataba wa (Richmond) unatekelezwa. Uelewa wake na nafasi yake ililipa kundi la Al-Adawi ufunguo katika wizara zinazohusika.”

Hata pale mawakili wa TANESCO walipombana Surtees ili aeleze sababu zilizoifanya Dowans kumpa Rostam hati ya uwakilishi, mfanyakazi huyo aliishia kusema, “hiyo ilitokana na barua ya mkopo (Letter of Credit) ya Dowans iliyokuwa inaandaliwa wakati huo na iliyohitaji Dowans kuwa na akaunti CRDB benki.” Katika mazingiara haya, zipo sheria kadhaa ambazo zinaweza kutumiwa na serikali kutaifisha mitambo hiyo. Tutazijadili sheria hizo katika toleo lijalo.

Mwandishi wa makala hii, Tundu Lissu, ni mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), mkoani Singida. Amejitambulisha kuwa msomaji wa siku nyingi wa gazeti hili. Anapatikana kwa simu Na. 0786 572571
0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: