Tutameza shubiri ya IPTL hadi lini?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 28 October 2009

Printer-friendly version

BAADA ya taifa kutumbikia tena kwenye giza kwa sababu ya mgawo wa umeme ambao unaelezwa kusababishwa na mambo manne, wiki iliyopita inasemekana Rais Jakaya Kikwete alishauriwa naye akakubali kuamuru kuwashwa kwa mitambo ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), mitambo ile ile ambayo amekuwa anahusishwa kuileta nchini.

Na ingawa ni kweli kama alivyowahi kusema mwaka 2005 kuwa hakusaini mkataba huo lakini anajivunia kushiriki mchakato wa kuileta IPTL, mzimu wa mkataba huo bado utamwandama hadi tatizo la umeme litakapopata ufumbuzi wa kudumu.

Mgawo wa sasa wa umeme unaelezwa kusabishwa na kupungua kwa maji kwenye mabwawa ya Hale, kuharibika kwa mtambo wa Kihansi, kuharibika kwa mtambo wa Songas na kuendelea kupungua kwa maji katika mabwawa mengine kutokana na ukame mfululizo.

Ni kama usemi wa mwenye njaa hachagui chakula, kwa maana hiyo tumefikishwa mahali kama taifa hatuna njia nyingine isipokuwa kukubali makali ya IPTL.

Kwa miaka mingi, habari zimeeleza kwamba umeme wa IPTL ni wa ghali kuliko inavyoweza kuelezwa kwa maneno ya kawaida; kwamba kwa siku moja tu ili mitambo yake yote 10 ifanye kazi na kuzalisha megawati 100 kwa saa 24, inabidi ibugie lita 500,000 za mafuta.

Gharama ya mafuta haya inakisiwa kuwa ni Sh. 600 milioni kwa siku. Hizi ni fedha nyingi kwa viwango vyovyote vile, hasa ikizingatiwa kwamba taifa kwa sasa linakabiliwa na changamoto nyingi na ngumu, mojawapo ukame ambao umeathiri sana sekta ya kilimo.

Kwa hali hiyo, kwa kuwa hakuna njia nyingine ya kupunguza makali ya mgawo wa umeme, serikali ambayo awali ilibariki mgawo huo imejirudi na sasa imeagiza mitambo ya IPTL iwashwe.

Uamuzi huu, pengine unaweza kufanana na kauli aliyowahi kuitoa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere miaka ya utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini kwamba kama wananchi wana njaa na nchi pekee ambayo chakula kinapatikana ni Afrika Kusini asingesita kununua chakula hicho.

Kauli hiyo ilikuwa na maana kwamba lipi jema kati ya kuendelea kuitenga Afrika Kusini kwa sababu ya siasa zao za ubaguzi, na uhai wa wananchi uliokuwa kwenye hatari ya kuangamia kwa sababu ya njaa?

Labda pia uamuzi huo ni sawa na kauli aliyopata kuitoa Rais Benjamin Mkapa wakati wa utawala wake, alipokuwa akitetea sera zake za ubinafsishaji na uwekezaji kutoka nje aliposema, “haijalishi paka ni wa rangi gani ilimradi anakamata panya,” aliponukuu msemo wa Wachina.

Kwa hiyo kujitumbukiza kwa IPTL kulikuwa hakuna mbadala walau kwa sasa, hilo linaweza kueleweka na pengine kuachwa hivyo lilivyo.

Lakini taabu moja inaibuka hapa ni kwamba licha ya tambo za rais Kikwete na wenzake wakati wanaingia madarakani, wameshindwa kabisa kuonyesha uwezo katika kutafuta suluhisho la kudumu la adha ya umeme. Walitutajia mikakati mingi, mmojawapo ukiwa mgodi wa Makaa wa Kiwira, kwamba ungeanza kuzalisha umeme mwishoni mwa mwaka 2006.

Kwamba ungezalisha megawati 200, ikianza kidogo kidogo. Kulikuwa na mkakati wa Richmond megawati 100; ulikuwapo Wartisilla, ulikuwapo wa Tegeta wa megawati 45, Kinyerezi megawati 200 kutaja kwa uchache tu.

Hadi sasa uhakika wa umeme katika mikakati hiyo upo kwa Wartisilla tu ambao sasa wanazalisha, Tegeta na tunaelezwa kwamba umeme wake hadi mwezi ujao. Mingine yote- Kiwira, Kinyerezi na Richmond - inakumbukwa kwa kashfa za wakubwa hao hao.

Kinachoumiza zaidi ni kwamba licha ya machungu haya ya IPTL tuliyoletewa na tunayolazimishwa, serikali ineonyesha unyonge ule ule wa miaka mingi; hakuna njia mbadala!

Kwa nini hakukuwa na mbadala? Jibu ni moja tu, kama taifa tulikwishaacha kufikiri kwa umakini na ujasiri wa kuthubutu siku nyingi. Tuliacha kwa kuwa kila mtu amegeuka mwanasiasa uchwara, hakuna anayejali kupiga hatua kuona tunavuka hatua moja hadi nyingine, kutoka hali duni hadi yenye nafuu zaidi, hakuna! Sote tumebakia kupiga debe, kuanzia juu hadi chini!

Tujaribu kujiuliza maswali machache. Inakuwaje gesi ya Songosongo iko Ubungo, lakini kama taifa hatuwezi kuwekeza kwa kujenga mitambo ya kufua umeme wa gesi? Inakuwaje gesi iwe Dar es Salaam bado tutaabike kama bado iko ardhini kule Songosongo?

Taifa hili liliimbishwa na kusadikishwa kwamba siku gesi ya Songosongo ikifika Dar es Salaam, kwa asilimia kubwa matatizo mengi ya umeme yatakuwa yamepungua. Ni jambo la bahati mbaya kwamba siku baada ya siku ukimuuliza mwananchi wa kawaida ni kwa kiwango gani gesi hii imepunguza makali ya machungu ya umeme, jibu liko wazi. Hakuna.

Tupige hatua mbele zaidi. Jiulize ni kwa kiwango gani basi gesi hii imesaidia kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa za viwandani ambako umma uliaminishwa kwamba kiasi cha asilimia 60 ya gharama za uzalishaji zilikuwa zinachangiwa na umeme wa Tanesco?

Jaribu kujiuliza kama saruji ya Wazo Hill au Mbeya au Tanga, ina tofauti yoyote ya bei? Zote zinauzwa bei sawa; hii ina maana kwamba hata wale wazalishaji wakubwa tulioambiwa kwamba wanatumia gesi kama nishati katika uzalishaji, hakuna tofauti ya maana na wale wasiotumia gesi hiyo kabisa.

Ndivyo ilivyo kati ya makampuni ya bia za Serengeti Breweries na Tanzania Breweries. Zote bei sawa, ingawa mmoja wao anatumia gesi.

Ninajaribu kurejea mifano hii kujenga hoja moja, kwamba kama taifa tumejipanga vipi kunufaika na rasilimali zilizopo nchini, ambazo kabla ya kuanza kutumika maisha yalikuwa ya dhiki kuu, lakini leo hii hali ni ile ile?

Nini hasa kinakwamisha mipango yetu, kiasi kwamba kila wakati hujikuta tukikimbizana na dharura? Wapo wapi wapanga mipango, je wametundika daluga zao wakisubiri kuelekezwa na wanasiasa nini cha kufanya?

Serikali hii inakamilisha ngwe yake ya kwanza ya miaka mitano mwakani. Kimsingi homa sasa ndani ya serikali hasa mawaziri ni uchaguzi. Sasa kama miaka mitano suluhu ya umeme haikuweza kupatikana licha ya gesi asilia kuwa hapo Ubungo, tunatarajie nini katika kukabiliana na changamoto nyeti za kitaifa kama tatizo la nishati ya umeme?

Tangu serikali ilipotakiwa kujadili na hatimaye kuinunua mitambo ya IPTL na kisha kuigeuza kutumia gesi asilia sasa ni mwaka wa tatu kama si wa nne, lakini ni hatua gani zimechukuliwa kama si kukimbizana mahakamani na kwenye mabaraza ya usuluhishi?

Niliwahi kusema huko nyuma, kwamba wakati wa Mwalimu Nyerere miundombinu ya umeme kutoka kokote yaliko mabwawa ya kuzalisha umeme ilijengwa kuingiza nishati hiyo kwenye gridi ya taifa, baada ya hapo, si awamu ya pili, ya tatu au ya nne inayoweza kueleza umma kwamba imefanya nini katika kusaidia nchi hii ipige hatua kwenye sekta ya nishati ya umeme.

Awamu zilizokuja baada ya Nyerere zimejipanga kugawana tenda ambazo kamwe hazijali maslahi ya taifa; ndivyo ilivyokuja IPTL, ikaja Kiwira, Richmond na nduguye Dowans.

Kila ninapopata fursa ya kuwaza najiuliza kama Nyerere angekuwa na utawala kama wa waliofuata, hivi leo nchi hii ingekuwa wapi? Tunajiuliza tena na tena tutakubali vidonge vichungu kama vya IPTL ya Kikwete hadi lini?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: