Tuufiche leo, tutaufunua kesho!


editor's picture

Na editor - Imechapwa 01 July 2008

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

UFISADI na ukosefu wa utawala bora ni matatizo yanayoitia doa serikali ya awamu ya nne iliyoingia madarakani kwa kaulimbiu ya 'ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya.'

Ni matatizo ambayo yalikuwa yakijulikana kabla ya Rais Jakaya Kikwete kupokea kijiti cha kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Desemba 2005.

Tatizo nguvu za wananchi kuyajadili na serikali kuyashughulikia zilikuwa dhaifu. Wananchi waliyajadili kwa uficho na serikali ikajitia hamnazo kuyarekebisha.

Inasikitisha hali ilikuwa hivyo wakati kiongozi aliyekuwepo awamu ya tatu ya uongozi wa nchi hii, Rais Benjamin Mkapa, aliingia kwa gia ya 'ukweli na uwazi' huku akiapa kumaliza rushwa.

Ni bahati mbaya sana utekelezaji wa sera hiyo uligubikwa na usiri mkubwa na ikatosha kuwa chanzo cha kuzorotesha hatua madhubuti za kurekebisha makosa yaliyokuwa yakitendeka ndani ya serikali na kwenye taasisi zake.

Kwa upande mwingine, udhaifu huo uliviza tu tuhuma za ufisadi na ukosefu wa utawala bora badala ya kuziangamiza kabisa. Zilikuwa tuhuma na zimebaki tuhuma vilevile.

Kipya kilichojitokeza ni kwamba mshindo wake unazidi kutingisha utawala kwa sababu ulishindwa kuziba ufa na haujaonyesha utayari kujenga ukuta.

Utawala hautaki ukweli usawiri wala hauko radhi kurekebisha. Uchafu unazidi kuganda na taifa linaangamia.

Tuliona viongozi walivyokuwa wakali waliposikia tuhuma zikitolewa kupitia vyombo vya habari. Walikasirika na kutoa matamshi yaliyolenga kuvunja moyo walalamikaji na hata kuwaamuru wazibe midomo yao.

Matatizo ya ufisadi wa kifedha na ufujaji wa raslimali za taifa, yametawala shughuli zote za serikali. Tuhuma nyingine ni zilezile za miaka iliyopita. Zinarudiwa kwa sababu hazikujibiwa wala waovu hawakudhibitiwa.

Kinachoitwa Meremeta, Tangold, IPTL, Songas, Mwananchi Goldmines, Kagoda Agriculture Ltd, Kiwira Coal Mines vilitajwa zamani. Vinatajwa leo na kelele kushamiri ndani ya Bunge ambako suluhu ingepatikana pangekuwa na uwazi na udhati.

Tuhuma zimeenea mitaani kwenye baraza za kahawa na karata na kwenye meza za pool. Zinajadiliwa kila siku kwenye vipindi vya mijadala katika vituo vya redio, televisheni na magazetini.

Hayo tunayafahamu. Ila sasa tunaposhuhudia hata Waziri Mkuu, kiongozi msaidizi mkuu wa Rais anayesimamia pia wajibu wa serikali ndani ya Bunge, anatoa kauli zinazokanganya, ndipo tunapopata hofu zaidi.

Hivi ni kweli Bunge kuelezwa wamiliki na shughuli za Meremeta na kampuni nyingine, pamoja na manufaa ambayo taifa lilipata kutokana nazo, ni kuchochea kufichuliwa siri za usalama wa nchi?

Kwani wabunge wameuliza mipango ya jeshi kuhusu vita au ya polisi wanavyotega wahalifu na waleta madawa ya kulevya? Kuuliza hatua za kutekeleza mapendekezo ya Bunge kuhusu mkataba wa Richmond na ufisadi wa EPA nayo ni kufichua siri za usalama wa nchi? Haya pia hayakuelezwa na visingizio ni vilevile vya 'tunakamilisha utaratibu.'

Wabunge wanalazimika kuuliza yote haya, kwa sababu wanabanwa na wananchi wanaotaka kufahamu raslimali zao, ikiwemo fedha zao, zinatumikaje.

Tunaona serikali inaendelea kuficha ukweli. Lakini upo tu na kama si leo, utajifunua kesho au keshokutwa. Ila kubwa zaidi ni: usipozibwa ufa leo, tutalazimika kujenga ukuta kesho.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: