Tuumizane kwa ukweli, siyo uwongo


Benson Msemwa's picture

Na Benson Msemwa - Imechapwa 23 June 2010

Printer-friendly version

UKWELI haujali mkubwa wala mdogo; haujali adui wala rafiki. Kwake watu wote ni sawa. Pia ukweli una tabia ya kulipiza kisasi kama ukipuuzwa.

Sasa si zama za kuwahadaa watu na kauli tamu za kuwafariji wakati maisha ni magumu.

Kuna mfumuko wa bei ni mkubwa, thamani ya fedha inashuka kwa kasi, huduma za jamii ni mbaya, rushwa ya kupindukia katika kila kona, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, matumizi ya kauli za vitisho na mengineyo.

Ni wakati wa kuwaambia Watanzania yote haya. Kuonyesha watawala wanakiri kinachoendelea na kuwashirikisha kutafuta ufumbuzi.

Viongozi wetu hawataki kuhubiri kweli hii; eti hawataki kuwakwaza Watanzania; eti wanaogopa kunyimwa kura wakati wa uchaguzi; hivyo wanakuja na takwimu zenye kuwafariji wananchi na ngojera ya “uchumi wetu unakua.”

Ukijaribu kudadisi na kuchokonoa kwa undani hapo utagundua mawazo ya viongozi wetu yamechoka, yamechoka kama wastaafu wa soka. Sasa wanapotosha badala ya kueleza ukweli.

Hakika huu sio wakati wa kufarijiana kwa uongo; ni wakati wa kuumizana kwa kuambizana ukweli, ndipo tutanusuru taifa letu.

Hebu tusikilize kiongozi. Anakuja na kauli za uchumi wetu unakua. Ukweli upo wapi hapo? Inawezekana uchumi wetu unakua kwa kuwa kima cha chini cha mshahara ni Sh. 80,000?

Au uchumi wetu unakua kwa kuwa watawala wameweza kuhama kutoka matumizi ya gari moja la kifahari hadi jingine la aina hiyohiyo?

Angalia hali za watumishi wengi wa umma, wahadhiri wa vyuo vyetu vikuu vya umma, manesi, walimu, askari na madaktari. Hawa ni watu muhimu sana ila nenda kawaulize wanalipwa nini?

Hawa hawana mama, baba, kaka, dada, wajomba, na shangazi kkatika utetezi na ulinzi kazini. Ni kiasi gani cha malipo wanapata pindi wanapostaafu?

Ni aina gani ya maisha wanayoishi mara baada ya kustaafu? Ni aibu tupu. Kwa nini huu usiwe wakati wa kuambizana ukweli na si kufarijiana kwa kauli za uongo?

Huwa najiuliza, hivi hakuna mikakati ambayo serikali inaweka ili kuboresha maisha ya wafanyakazi na wananchi kwa ujumla?

Ni nani anayesababisha hadi malimbikizo ya walimu yanakuwa makubwa kiasi cha serikali kuanza kuwapiga danadana kwenye malipo yao?

Hivi kama tungekuwa tunasema ukweli migomo kama ya shirikisho la vyama vya wafanyakazi (TUCTA) ingekuwepo?

Je, maandamano ya wazee wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyokufa zamani tungeyaona?

Ukweli ungetuepusha na ongezeko la wakwepa kodi kwa serikali yetu. Nani anayekalia kweli hiyo? Kwa nini anakuja na kauli za uongo kutufariji?

Kutokana na kutokuwa wa kweli ndio tunaona hizi vurugu za madereva wa daladala na hii kampuni ya MAJEMBE; vurugu za mgambo na wamachinga; jiji na watu wanaohamishwa kwenye makazi yao.

Ni kwa kuwa mamabo hayako wazi; watu wanajengewa hisia hasi (mbaya); wanaamua kukaidi; wanakuwa wakorofi, vurugu zinazuka, yote hayo ni watawala wetu kutotaka kuwa wakweli.

Kwa kuwa watawala wameshindwa kujenga misingi ya uwazi ya kuwajibika, kujiwajibisha na kuwajibishwa, basi watatumia nguvu, vitisho ili kupindisha ukweli.

Tuseme ukweli. Hivi hii mitaala yetu kuanza shule za msingi hadi elimu ya juu inaendana kweli na karne tuliyopo?

Inajenga udadisi na ubunifu kwa kizazi kilichopo? Inachochea uzalendo, maadili na uwajibikaji pindi mwanafunzi anapohitimu daraja husika?

Kweli hizi shule zetu za Mtakatifu Kayumba zitatuingiza kwenye ushindani na nchi nyingine chini ya hii dunia ya utandawazi?

Tuwe wakweli hapo na tusifarijiane kwa kauli za uongo. Hapa ndipo ninapozikumbuka shule za ufundi Iyunga, Ifunda, Moshi; zipo wapi sifa za shule hizo?
Nani ameziua?

Jitihada za kupata mbadala wa shule hizo zipo wapi? Yote hayo ndiyo yanayopelekea hadi sasa kushindwa hata kutengeneza vijiti vya kuchokonolea meno.

Hivi karibuni limeanza zoezi la kugawa vyandarua ili kukabiliana na malaria chini ya kauli mbiu yetu ya “malaria haikubaliki.”

Ukweli ni kwamba malaria inakubalika. Ukubwa wa chandarua ni kutosha kitanda cha futi tatu na nusu, kwa wale wenye vitanda vya futi sita hivyo vyandarua vitakuwa vikiogelea.

Wameshindwa kuwa wakweli. Hapa malaria inakubalika au mtu aingie gharama ya kutengeneza kitanda kingine kidogo cha mtoto cha kutosha hicho chandarua cha futi tatu na nusu.

Nani alimdanganya rais wetu kuwa malaria haikubaliki? Kwa mwendo huu kweli tutaweza kukwepa vifo vya watoto 18 kwa kila dakika tisini kutokana na malaria? Hivi ni kweli kwa vyandarua vya futi tatu na nusu malaria haikubaliki? Hapa kuna kasoro.

Inafika mahali kiongozi anatoa kauli kuwa ukitaka mambo yako yawe safi au kukunyookea njoo kwenye chama chetu (CCM).

Dadisi kiundani hapo. Huyo anataka watu waelewe kuwa sasa chama kimeshika utamu na si hatamu tena. Ukiwa mwizi, fisadi, jambazi, ilimradi upo kwenye chama chake, wewe mambo yako safi.

Kiongozi kama huyo anajenga jamii ya aina gani? Anataka watu wajifinze nini kutokana na kauli zake? Anapindisha ukweli, anawafariji watu kwa uongo, anapalilia kero kwa vizazi hata vizazi.

Kuna uhaba wa wahadhiri kwenye vyuo vyetu. Wengi wanafanya kazi kwa mikataba kwani walishastaafu kwenye utumishi wao. Hatujui mikataba yao na Mungu bali tunachojua ni mikataba yao na serikali.

Kiongozi wa serikali, waziri huyo, anathubutu kuudanganya umma eti tunao wahadhiri wa kutosha vyuoni. Ni aina gani ya uongo uliotukuka? Uko wapi ukweli? Watasema uwongo ilimardi wanyamazishe wasiyetaka aendelee kuwa mwalimu chuoni.

Tupo na kila aina ya rasilimali, lakini taifa letu ni ombaomba. Tujiulize, sisi ni ombaomba wakati tuna raslimali, je rasilimali zitakapokwisha taifa litakuwa vipi?

Hii hali ya utegemezi, kukopa na hata kuazima italipeleka wapi taifa? Kenya wameweza kukwepa utegemezi mkubwa kwenye bajeti yao, kwanini sisi Tanzania tushindwe?

Jamii ambayo haipo katika misingi ya ukweli ndiyo iliyojaa kauli za kulalamika kuanzia ngazi ya diwani hadi raisi. Kwa uwongo huu taifa haliwezi kuendelea.

0
No votes yet