Tuwamulike matajiri wa Simba, Yanga


Elius Kambili's picture

Na Elius Kambili - Imechapwa 25 July 2012

Printer-friendly version

ZAMANI matajiri wengi walibaki tu kuwa wafadhili wa michezo – walitoa fedha ili zisaidie katika usajili, nauli na hata malipo au mishahara.

Baadaye wakajitosa katika udhamini; hapo ndipo matajiri walitoa fedha kwa masharti kwamba timu zitangaze bidhaa mbalimbali au huduma zao. Lakini leo matajiri wote wanataka uongozi katika klabu. Kuna nini?

Baadhi ya matajiri wa Yanga na Simba ni kama Mohamed Viran ‘Babu’, Fadhal Kasim, Abbas Gulamali, na Azim Dewji aliyeifadhili Simba na baadaye klabu ya Sigara kabla ya Kajumulo
Yanga ilitangaza bidhaa kwa kuvaa jezi zenye nembo za Bobby Soap, Azamto, Sharuk’s; Simba walivaa jezi zenye nembo ya Highway, Maji Poa, Simba Cement, KK Sukari; Sigara ya Dewji ilitangaza dawa ya Dakika Tatu.

Katika kipindi chote ambacho wafadhili hao wamekuwa wakitoa fedha, kumekuwa na malalamiko ya fedha kuliwa.

Je, kelele za kuliwa kwa fedha ndiko kumesababisha matajiri hao kujitosa wenyewe kuongoza?

Ukweli, malalamiko dhidi ya viongozi kuwa wamekula fedha kuliwaudhi wafadhili wafanyabiashara, ambao taratibu wakaanza kujiondoa katika ufadhili wao katika soka.

Mathalani Dewji alijitoa Simba na kuanza kuidhamini Sigara iliyoachwa kipindi cha ubinafshaji wa mashirika ya umma. Ingawa Simba bado ilikuwa na wafadhili kama Mohammed Enterprises, mashabiki ambao pia walikuwa wanazisaidia timu bila mfumo wa udhamini kama ilivyokuwa kwa kina Dewji wakaibuka.

Mashabiki hao wanajikusanya na kuamua kuisaidia timu ifikie lengo kama kusajili au kuweka kambi ya maana hasa kipindi cha kuelekea mechi ngumu. Makundi hayo ni kama ya Friends of Simba na Yanga Family.

Baada ya kuwa karibu na timu kutokana na kitendo chao kusaidia, wanachama hao hasa wasiokuwa na mapenzi mema na timu hizo wakagundua kitu. Waliona mwanya wa wao kutengeneza fedha zaidi kupitia klabu hizo.

Walihama ghafla kutoka kuzisaidia timu hadi kuanza kuzikopesha kisha kulipwa kwa riba kubwa, hapo ndipo Simba na Yanga zilipofungiwa milango ya kujitegemea.

Watu hao waliona wakiziacha klabu hizo zijitegemee tu, hawatafaidika na chochote. Na kwa hofu kuwa nguvu yao inaweza kupunguzwa na wanachama wenye uelewa, wafadhili uchwara wakaibuka na kuingia katika timu kana kwamba nao ni viongozi kisha kushurutisha baadhi ya mambo yafanyike.

Wakatumia nafasi ya kusaidia timu kwa kuleta makocha wa kigeni na kuwalipa mishahara watakayo.

Wakawa wanasajili wachezaji wazuri wa ndani na nje ya nchi ambao wanawajibika zaidi kwao kuliko kwa viongozi.  Wachezaji hao wakawa wanafuata hata matakwa ya mabosi zao ya namna ya kucheza uwanjani hata pale walipoelekezwa kucheza chini ya kiwango katika baadhi ya mechi.

Baadhi ya wanachama waliobaini mambo yanayofanywa na wahisani hao, wakaanza kuhoji uhalali wa mambo hayo. Hao walionekana kuwa wasioitakia mema timu, kwani mashabiki wengi wanachotaka ni kuona timu inashinda tu, hawana mpango na kinachotokea nje ya uwanja.

Hapo ndipo matajiri hao taratibu wakaona ni vyema waingie wazima wazima katika uongozi wa timu hizo. Tayari sasa wameshika hatamu za uongozi, tena kwa ridhaa ya wanachama halali.

Nawaunga mkono wanachama wa Simba na Yanga kwa kuchagua viongozi wenye nazo kwani nina hakika wana nia nzuri ya kuona timu zao zinafanya vizuri kila siku kupitia watu hao. Tatizo wanaweza kuangushwa na watu hao.

Kinachonikwaza ni kwamba, hakuna tajiri hata mmoja anayeonekana kuweka mkazo wa timu hizo kujitegemea ndani ya muda mfupi ujao zaidi ya kuimarisha mazingira ya wao kutegemewa milele na milele. Tangu waingie madarakani hawajaweka wazi njia watakazofanya kuhakikisha timu hizo zinajitegemea. Kwa nini?

Mmiliki wa Azam FC pekee ndiye mwenye mtazamo mpana wa kuijenga klabu hiyo kuwa tishio – ina uwanja wake na mikakati endelevu.

Timu zinazomilikiwa na majeshi kama Polisi, Prisons, JKT Oljoro, JKT Ruvu na Ruvu Shooting ziko hoi kiufanisi na hata zinazomilikiwa na makampuni kama Kagera Sugar na Mtibwa Sugar hazina kipya kiuongozi.

Hapo ndipo matajiri wa Simba na Yanga wanaweza kufanya lolote. Wanasajili wachezaji kwa mamilioni ya shilingi huku wakiahidi kulipa mishahara mikubwa kuliko nguvu ya timu katika kutekeleza hilo, mwisho wa siku inayodaiwa ni klabu si mfanyabiashara.

Wengi wao wanafanya maamuzi mengi makubwa hata ya kusajili bila kufuata ushauri wa kitaalamu. Mashabiki wenye maneno mengi, hutulizwa kwa fedha.

Kwa kuwa timu zote hazina kanuni inayomlazimisha kiongozi binafsi kulipa mishahara, kuna uwezekano mkubwa mtindo wa kiongozi kuikopesha timu ukaendelea na klabu kama Simba na Yanga zikaendelea kuwa maskini hadi mwisho wa dunia hii.

Rai yetu ni kwamba matajiri waliopata bahati ya kuziongoza klabu zikiwemo za Simba na Yanga wanapaswa kuzitumikia timu kwa maslahi ya klabu hizo na kuweka mifumo huru ya kujitegemea ili wakimaliza muda wao wawe wamejiwekea heshima kubwa.

0713 801 699
0
Your rating: None Average: 4 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: